7.1 C
New York

Elizabeth; Mama wa Watoto sita anayepambana na maisha Mvomero

Published:

Na Tulinagwe Malopa, Gazetini

“Acha…Si unaumwa wewe? Sina pesa mimi ya kukukimbiza hospitali sahivi,” Ni maneno ya mama anayemkataza mtoto wake kufanya michezo ya hatari inayoweza kumweka katika mazingira ya kuumia licha ya hali yake ya ugonjwa wa mapunye kichwani. 

Ni Elizabeth Yasini mama wa watoto sita anayepambana kutunza familia yake kupitia biashara ya mboga ambayo si chanzo imara cha kuwasaidia yeye na watoto wake. 

Baada ya siku isiyo na matumaini katika biashara yake ya mboga, mama huyo alisema uwezo wa kutunza watoto wake sio mkubwa hivyo angekua anapata msaada wa malezi kutoka kwa mzazi mwenzake ingekua afadhali. 

“Ni basi tu sipati ushirikiano kutoka kwa mzazi mwenzangu, ila sio kwamba nina uwezo wa kulea mwenyewe hawa watoto kulingana na kipato nilichonacho,” anasema Elizabeth akionekana mwenye uchungu mwingi.

Elizabeth ndiye mama na baba wa watoto wake baada ya kutelekezwa na mumewe ambaye hajulikani alipo kwa sasa. 

Tofauti na nyumba zingine zilizopo eneo hilo lililopo Wilaya ya Mvomero anapoishi Elizabeth, nyumba yake ni ya udongo ambayo haiko imara hasa nyakati za mvua kubwa zinazoweza kunyesha muda wowote. 

Elizabeth alianza kufanya biashara ya mboga baada ya kukosa fedha ya kununua dawa za kumtibia mtoto wake mdogo alipoumwa homa na kupelekea kuchuma mboga alizokua nazo shambani kwake kwenda kuuza ili apate pesa ya kumtibia mtoto wake. 

“Tulikua tunakula chakula ninachopata shambani ninapolima. Siku moja mwanangu alizidiwa usiku na sikua na hata sh 500 ya kumnunulia panado, ndipo nilipokumbuka nina mafungu matatu ya mboga shambani nikaenda kuuza nikamtibu,” anasema Elizabeth. 

Mama huyu anawakilisha kundi kubwa la wanawake na familia zinazoishi katika mazingira magumu kwa kukosa mahitaji muhimu hivyo kupelekea kuteseka kwa magonjwa, njaa na maradhi mengine. 

Mikakati iliyowekwa na Serikali kusaidia watu wenye hali duni 

Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, ni miongoni mwa mikakati inayopaswa kutiliwa mkazo na Serikali na wadau wa maendeleo ili kupunguza umaskini nchini. Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa Tanzania inayoguswa na Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambapo lengo la sera hiyo, ni kuwezesha na kutoa fursa za kiuchumi kwa Wananchi hasa wenye hali duni na makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwajibikaji Utoaji wa Huduma kwa Jamii iliyotolewa na taasisi ya Wajibu kutoka kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kiasi cha Sh 545 bilioni hazikutolewa kwa wananchi hivyo kurudisha nyuma jitihada za kupunguza umaskini kwa kaya maskini nchini.

Kiasi hicho cha fedha kinaonesha kukwamishwa kwa jitihada za kukomboa kaya zaidi ya 1,000 zenye hali duni ambapo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo nchini.

Ufaninisi wa mkakati huo

“Binafsi nasikia tu watu wanataja huo mfuko ila sijawahi kupata mwongozo wowote au kufuatilia kwasababu ya uoga wa kukosa vigezo vya kupata hizo fedha,” anasema Mwahija Mohammed mama wa watoto watatu na mume mmoja wanaoishi kwenye nyumba yenye hatari ya kuanguka muda wowote iwapo mvua kubwa itanyesha. 

Licha ya uhitaji kuwa mkubwa bado ufanisi wa mfuko huo sio mzuri kwasababu uelewa kuhusu taratibu na vigezo vya kupata pesa hauko wazi kwa wahitaji hivyo kupelekea pesa kushindwa kufikia wahusika kwa kiwango na muda uliopangwa. 

Nini mpango wa Serikali kunusuru kaya maskini kupitia mfuko huu?

Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini(TASAF III) wilayani Mvomero, Dedan Maube ametoa wito kwa jamii na hasa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini watambue kuwa msingi/Roho ya mafanikio ya mpango huo ni utimizaji wa masharti hasa ya Elimu na Afya.

Wanufaika wa mfuko huo wanasemaje?

Kwa niaba ya walengwa wenzao wa mradi huo kwa nyakati tofauti, Coleta Katomondo na Paulo Ilehao wamesema mradi huo kwao ni mkombozi kwani pesa hizo zimewasaidia sana na kuwawezesha kununua vyakula,kulima mashamba, kufungua miradi mbalimbali midogomidogo,kununua mahitaji ya shule kwa watoto wao kama vile sare za shule na kadhalika lakini pia umewawezesha kununua mabati kwa ajili ya ujenzi, hivyo wanaushukuru uongozi wa Wilaya kwa kuwatazama kwa jicho la karibu na wanaomba wilaya isiwachoke kuwasaidia kujikwamuia katika umaskini.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img