1.7 C
New York

MAP| Wananchi Morogoro wanavyopambana na Malaria kwa watoto

Published:

*Ni mfereji uliopewa jina la ‘Aunty Malaria’ kwasababu ya uzalishaji wa mbu katika makazi yaliyo karibu

*Pamoja na ugumu wa mazingira hayo, wananchi wanajitahidi kufanya jitihada

Na Tulinagwe Malopa, Gazetini

Ni miongoni mwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Anatamani siku moja mazingira yanayozunguka makazi yake yabadilike ili awe na uhuru wa kumlaza mtoto wake mwenye umri wa miezi mitatu sasa hata nyakati za mchana.

Huyu ni Jestina Mkumbo, mama wa watoto wawili anayeishi katika kata ya Mwembesongo iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Mazingira yanayozunguka nyumba anayoishi, Jestina si rafiki kwasababu ya mfereji mkubwa wa maji yaliyotuama uliopewa jina la ‘Aunty Malaria’ kwasababu ya athari za maambukizi ambayo yamekuwa yakisababishwa na maji kwenye mfereji huo uliopo katika makazi ya watu.

Licha ya jitihada zilizofanywa na wakazi wa eneo hilo ikiwemo kukinga watoto na maambukizi ya Malaria na kukata nyasi zinazozunguka eneo hilo, bado wananchi wanapata maambukizi kuliko kawaida.

“Maambukizi bado yapo. Hapa mimi juzi tu nimetoka kumtibia mwanangu homa ya malaria. Kwahiyo kwakweli haya mazingira si rafiki sana kwetu,” anasema mkazi wa eneo hilo ambaye hakuwa tayari jina lake litajwe.

Takwimu zinasemaje?

Kwa mujibu wa Ripoti ya Uchambuzi wa Takwimu Muhimu (Tanzania in Figures 2018, 2019 & 2020) zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), watoto zaidi ya 1,000 wenye umri kati ya miezi 6-59, mkoani Morogoro, wameathirika na ugonjwa huo, katika kipindi cha miaka mitatu.

Hii ina maana kwamba watoto 343 wanaambukizwa ugonjwa huo kila mwaka.

Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa 30 yenye maambukizi ya Malaria yanayojirudia kila mwaka na ukishika nafasi ya sita kwenye maambukizi mengi ya ugonjwa huo katika kipindi cha miaka mitatu.

Jitihada za wananchi kutatua tatizo

Ili kupunguza athari za ugonjwa huo kwa watoto, wananchi wa eneo hilo hufanya jitihada za kuwakinga watoto ikiwemo kwa kuwawekea neti za mbu kila wanapowalaza na kusafisha mazingira yanayozunguka nyumba zao ili kupunguza mazalia ya mbu katika mazingira yanayowazunguka.

“Kwasasa namwekea tu mwanangu neti hata kama ni mchana, maana kwakweli homa kwa hapa ni kitu cha kawaida na watoto wadogo ndio inawapata kwa haraka sana,” anasema Jestina.

Ili kukabiliana na tatizo hili, kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), hatua mbalimbali ikiwemo kuua mazalia ya mbu katika madimbwi na kusafisha maeneo yenye majani mengi, ni miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kuchukuliwa ili kutokomeza maambukizi ya malaria katika makazi ya watu.

Hata hivyo, nyumba nyingi zinazozunguka eneo hilo zimezungushiwa nyavu za kuzuia mbu kuingia ndani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img