1.6 C
New York

MAP| Usajili wa Watoto Tanzania

Published:

Na Faraja Masinde, Gazeti

Kwa miaka ya nyuma suala la usajili wa watoto na kupata vyeti vya kuzaliwa ilikuwa siyo kipaumbele cha wazazi walio wengi, madhara ya hatua hiyo yalikuja kuonekana baadae pale vilipokuwa vinahitajika vyeti hivyo.

Wapo walioshindwa kufanikisha mambo yao mengi kutokana tu na kutokuwa na cheti cha kuzaliwa.

Ni sababu hiyo na nyingine nyingi ndiyo iliisukuma Serikali mwaka 2013 kupitia Wakala Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuja na Mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano nchi nzima bila malipo.

Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa watoto wote walio na umri chini ya miaka mitano wanasajiliwa lakini sambamba na lengo hilo pia inatazamia kusajili kwa wale wote waliko shule ya msingi.

Hadi sasa RITA kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Maendeleo imefanikiwa kufikia mikoa 23 kupitia mpango huo kama unavyoona kwenye usanifu wetu hapo juu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Angela Anatory akizungumza kuhusu Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano anasema kuwa lengo ni kuhakikisha kila mtoto ambae hajasajiliwa, anasajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa.

Anabainisha kuwa mbali na kufungua mlango wa haki ya kutambuliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, mpango huo umekuwa na matokeo makubwa ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizokuwa zinaikabili Serikali na wananchi kuhusiana na usajili wa vizazi.

Aidha, amesema mpango huo utahakikisha kwamba kila mtoto atakayezaliwa kuanzia siku mpango huo umeanza kutekelezwa anasajiliwa ndani ya muda mfupi baada ya tukio la kizazi kutokea.

“Chimbuko la mpango huu ni uwepo wa kiwango kidogo cha wananchi ambao wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa hapa nchini kutokana na sababu mbalimbali zilizosababisha wananchi kushindwa kusajili vizazi hivyo basi serikali na wadau kuamua kubuni mpango huu unaoenda kutatua changamoto zilizopo katika mfumo wa awali.

“Mpango wa Usajili wa Watoto unaleta maboresho yafuatayo katika Mfumo wa Usajili; moja, kusogeza huduma za usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi na huduma kupatikana katika vituo vya Tiba vinavyotoa huduma ya Mama na Mtoto na katika Ofisi za Watendaji Kata.

“Pili, kuondoa ada ya cheti kwa watoto wanaosajiliwa kupitia Mpango huu hivyo nyaraka hiyo kutolewa BILA MALIPO. Tatu, kuimarisha mfumo wa kutuma na kuhifadhi taarifa za waliosajiliwa kwa kutumia TEHAMA ambapo simu ya kiganjani iliyowekwa programu maalum hutumika,” anasema Anatory.

Kwa muji wa Anatory, mpango huo mpaka sasa umetekelezwa katika mikoa 23 ya Mwanza, Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Geita, Shinyanga, Lindi, Mtwara, Simiyu, Morogoro, Pwani, Mara, Dodoma, Singida, Ruvuma, Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Rukwa na Katavi na Tabora.

“Kwa ujumla Mafanikio ya utekelezaji wa mpango huu katika mikoa iliyotangulia ni makubwa na mpaka sasa zaidi ya watoto 7,549,878 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa, hivyo kuongeza kiwango cha usajili kutoka asilimia 13 mwaka 2012 na kufikia asilimia 65 mwaka 2021.

“Hii ni sawa na kusema kwamba zaidi ya nusu ya watoto nchini wamepata haki yao ya msingi ya kutambuliwa na taarifa zao kuingizwa katika mfumo rasmi wa utambuzi wa serikali,” amesema Anatory.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Shalini Bahunguna anabainisha kuwa dhamira ya UNICEF kwa Serikali na kutambua msaada mkubwa kutoka kwa serikali ya Canada na TIGO katika kufanikisha mpango huo muhimu unaolenga kusajili watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano na kuwapatia cheti cha kuzaliwa kama moja ya haki za msingi.

“Haki ya kusajiliwa baada ya kuzaliwa imeainishwa katika Mkataba wa Haki za Mtoto, na tunapongeza maendeleo ya Tanzania kuhakikisha haki hii inapatikana kwa kila mtoto,” anasema Bahuguna huku akitoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwa mfumo wa usajili wa vizazi unapangwa na kufadhiliwa katika ngazi ya taifa, mikoa na wilaya na kuhimiza kuwa uandikishaji wa raia unaunganishwa katika kazi za kawaida za halmashauri za wilaya na mikoa ili kuendeleza mafanikio makubwa katika mfumo huu wa kitaifa,” amesema Bahuguna.

Upande wake Mkurugenzi Mwandamizi na Mkuu wa Ushirikiano, Kamisheni Kuu ya Canada, Helen Fytcheambao ambao ni sehemu ya wafadhili wa mpango huo anasema kuwa nchi hiyo inahakikisha upatikanaji wa huduma na haki muhimu, hasa kwa wanawake na wasichana.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img