22.9 C
New York

Infographic| OSHA inavyosaidia kukuweka salama kazini

Published:

Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi unaimarika hususan sekta ya viwanda.

Hata hivyo, pamoja na kuwapo kwa ukuaji wa sekta ya viwanda na kuimarisha uchumi, suala la usalama na afya kwenye mazingira ya kazi ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha hali ya juu.

Hii ni kwa sababu kumekuwa kukiripotiwa matukio ya ajali mara kwa mara makazini kutokana na wahusika kutotimiza matakwa ya sheria hivyo kugharimu maisha ya watu.

Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), kupitia ripoti yake ya mwaka 2019, watu 7,500 hufariki dunia kila siku kutokana na mazingira yasiyo salama na afya kazini.

Kama hiyo haitoshi, ILO kupitia ripoti hiyo inasema watu zaidi ya milioni 374 hujeruhiwa au kuugua kutokana na ajali kazini au kufanya kazi muda mrefu.

Pia imefafanua kuwa watu 6,500 hufariki kutokana na magonjwa yanayowapata kazini huku 1,000 wakifariki dunia kutokana na ajali kazini kiwago ambacho ni sawa na asilimia tano hadi saba ya vifo vyote vinavyotokea duniani.

Hapa nchini, mamlaka iliyopewa jukumu la kuwakumbusha waajiri juu ya usalama na afya za wafanyakazi wawapo kazini ni Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

OSHA ambao ni wakala wa serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), imepewa jukumu la kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vilivyopo katika sehemu za kazi vinavyoweza kusababisha magonjwa, ajali na hata kifo ambapo imekuwa ikifanya hivyo kupitia usimamizi wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Khadija Mwenda ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, ambaye anasema kuwa lengo lao ni kuhakikisha wanazifikia sehemu nyingi za kazi kadri itakavyowezekana.

“Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) ni chombo cha kusimamia usalama na afya mahala pa kazi kwa kuhakikisha kwamba waajiri wote nchini wanaweka miundo na mifumo inayohakikisha usalama na afya mahala pa kazi vinalindwa.

“Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la idadi ya waajiri wanaotuma maombi kuomba kukaguliwa au mafunzo ya usalama na afya makazini mwao. Hiki ni kiashiria muhimu cha mafanikio. Taasisi ya OSHA inatia mkazo katika kuelimisha kuliko kuadhibu ili kuhakikisha kwamba waajiri wanawajibika bila shurti,” anasema Mwenda.

Anabainisha kuwa kwa kipindi cha OSHA imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2016/2017-2021/2022) ikiwemo kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,003 hadi 23,239 pamoja na idadi ya kaguzi za Usalama na Afya mahali pa kazi kutoka 96,000 hadi 784,000.

“Hivyo, ongezeko hili katika usimamizi wa sheria linamaanisha sehemu nyingi za kazi zimefikiwa, kaguzi zimefanyika, tathmini ya afya imefanyika kwa wafanyakazi walio wengi na hivyo kuendelea kuimarisha hali ya usalama na afya mahali pa kazi,” anasema Mwenda.

Mwenda anataja mafanikio mengine kuwa ni kuimarisha mifumo ya kiutendaji na usimamizi ndani ya taasisi, hali ambayo imesaidia kuondoa urasimu katika utoaji huduma na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji.

“Katika kufanikisha hili, tulifanya mapitio ya mlolongo wa biashara (Business Process Review) ili kubaini maeneo yanayoleta urasimu katika utekelezaji wa majukumu yetu na kupitia mapitio hayo, OSHA imefanikiwa kupunguza muda wa kutoa cheti cha usajili wa sehemu ya kazi kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na muda ya kushughulikia leseni ya kukidhi matakwa ya Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi kutoka siku 28 hadi siku tatu baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu,” anasema Mwenda.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda.

Jukumu la OSHA ni kupunguza ajali na magonjwa katika sehemu za kazi, lengo ambalo linatakiwa kwenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.

“Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, ilipendekeza kufutwa kwa tozo hizo ambapo Serikali iliridhia kufanya marekebisho kupitia GN. 719 ya Novemba 16, 2018 iliyofuta tozo mbalimbali zikiwamo ada ya usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya Sh 50,000 hadi Sh 1, 800,000.

“Pia ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi iliyokuwa ikitozwa Sh 2,000 ilifutwa; faini zinazohusiana na vifaa vya kuzimia moto ya Sh 500,000 ambayo ilikuwa inaingiliana na taratibu zinazosimamiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” anasema Mwenda.

Changamoto sugu

Kama ilivyo kawaida kwamba kila palipo na mafanikio basi changamoto hazikosekani. Hivi ndivyo ilivyo na kwa OSHA pia ambapo licha ya kupata mafaniko hayo bado kuna vikwazo vinavyoinyima usingizi taasisi hii nyeti katika kusukuma maendeleo kama anavyobainisha mtendaji mkuu.

“Hata hivyo, bado tunakabiliwa na changamoto kuu mbili ambazo kwanza ni uelewa mdogo miongoni mwa waajiri na wafanyakazi kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama na afya kazini, na yapili ni ukiukwaji wa masharti kwa kutozingatia viwango vya usalama na afya.

“Changamoto ya pili inatokana na imani isiyo sahihi miongoni mwa baadhi ya waajiri kwamba gharama za kuhakikisha usalama na afya mahala pa kazi ni kubwa sana, tofauti na hali halisi inavyoonesha.

“Utafiti umethibitisha kwamba faida zitokanazo na mazingira ya usalama na afya mahala pa kazi ni kubwa kuliko gharama,” anasema Mwenda.

Mikakati ya mbeleni

Mwenda anasema kuwa katika siku za usoni OSHA inatilia mkazo suala la kuongeza tija kwa kusimamia viwango vya usalama na kulinda afya ya mfanyakazi anapokuwa kazini ili kuongeza tija kwani ajali, madhara ya kiafya na vifo vinavyotokana na shughuli za kazi vikipungua, tija inaongezeka.

“OSHA inaanzisha mifumo shirikishi kati ya waajiri na taasisi ili kuhakikisha utekelezaji wa hiari wa masharti ya usalama na afya makazini. OSHA inatia mkazo uingizaji wa sekta isiyo rasmi yenye wafanyakazi walioajiriwa na waliojiajiri wenyewe katika masuala ya usalama na afya kazini, kwa kubuni mikakati na kuandaa programu maalum endelevu zitakazolinda usalama na afya ya wafanyakazi katika shughuli zote za sekta hiyo,” anasema Mwenda.

Anaongeza kuwa OSHA inachangia katika kuongeza ajira zenye staha kama ilivyoainishwa katika malengo ya milenia, hususan lengo Na. 8.

“HA inaongozwa na ajenda ya ‘Vission Zero’ ambayo baada ya miaka michache ijayo, HAKUNA majeraha na ajali sehemu za kazi; HAKUNA madhara na magonjwa yatokanayo na mazingira ya kazi; na HAKUNA vifo vinavyotokana na kazi.

“Tunataka waajiri na wafanyakazi waelewe uhusiano kati ya usalama na afya mahala pa kazi na kuongezeka kwa tija na uzalishaji; waajiri wanatambua kwamba gharama za kuhakikisha usalama na afya mahala pa kazi hazifikii ukubwa wa faida zinazopatikana; na wafanyakazi wanaona umuhimu wa kutumia vifaa kinga wanapokuwa kazini na/au kudai vifaa hivyo kwa waajiri wao pale ambapo havitolewi,” anasema Mwenda na kuongeza kuwa;

“Tukifanikisha hilo, tutachangia kuongezeka kwa pato la taifa kwa kuongeza tija na uzalishaji mahala pa kazi, na kuondoa mzunguko wa umaskini usio na mwisho kwa kupunguza au kutokomeza kabisa ajali, maradhi, ulemavu na vifo mahala pa kazi.

“Hivyo tutaendelea kuelimisha waajiri na wafanyakazi kuhusu uhusiano uliopo katika ya usalama na afya mahala pa kazi, kuongezeka kwa tija na uzalishaji, kukua kwa pato la taifa, na uwezo wa Serikali kutoa huduma bora za jamii,” anahitimisha Mwenda.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img