1.4 C
New York

Infographic| Isabel; Mwanamke tajiri zaidi Afrika anayeteswa na ufisadi

Published:

MIAKA nane iliyopita, jina la Isabel dos Santos liliteka vichwa vya habari ndani na nje ya Afrika baada ya binti huyo wa Rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo dos Santos, kutangazwa na Jarida la Forbes kuwa ndiye mwanamke tajiri zaidi barani humu.

Wakati huo, utajiri wa bibiye Isabel ulitajwa kufikia Dola za Marekani bilioni 3.5, akivuna fedha nyingi zaidi kutokana na kampuni za mafuta na mawasiliano alizokuwa akimiliki.

Hata hivyo, kila kitu kilibadilika mara tu mzee wake alipoondoka madarakani. Hapo ndipo Serikali iliyoingia madarakani mwaka 2017 ilipoanza kumkalia kooni Isabel, ikimtuhumu kwa madai ya ufisadi, hasa enzi zile za utawala wa baba yake.

Ikimaanisha, Isabel hana wa kumlaumu zaidi ya Rais wa sasa wa Angola, Joao Lourenco. Mara tu Lourenco alipoingia Ikulu, aliahidi kusimama kidete kwa ‘wapigaji’ wote. Isabel akaanza kuandamwa na kesi, achilia mbali mamlaka kushikilia mali alizokuwa nazo kwenye nchi mbalimbali.

Moja ya hatua kali dhidi ya Isabel ikawa ni kumng’oa kwenye wadhifa wa kiongozi wa kampuni ya mafuta ya Serikali, Sonangol.  Ikumbukwe, ni nafasi aliyopewa na baba yake mwaka 2016.

Mwaka 2019, Serikali ya Rais Lourenco ikaanza uchunguzi dhidi ya utajiri wa Isabel na hapo ndipo lilipozuka hilo la mali zake kushikiliwa. Si mali zake tu, bali hata za mumewe, Sindika Dokolo, zikawekwa chini ya ulinzi.

Hali ikawa tete zaidi mwaka jana kwa wawili hao, Isabel na Dokolo, baada ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Angola kuwafungulia mashitaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Wakati huo huo, Serikali ya Ureno nayo ikaunga mkono kile kilichokuwa kikiendelea Angola kwa kuanza kufichua na kushikilia mali zote za Isabel alizowekeza nchini kwao.

Hadi sasa, jarida la Forbes limebaini kuwa mali za Isabel zilizoshikiliwa nchini Angola pekee zinafikia thamani ya Dola milioni 300, wakati zile zilizo mikononi mwa Ureno na Uholanzi zikifikia Dola bilioni 1.3.

Kwa kupoteza Dola bilioni 1.6, hatimaye sasa Isabel ameporomoka kwenye viwango vya jarida la Forbes, kwamba si mwanamke tajiri zaidi Afrika kama ilivyokuwa awali.

Ripoti ya mwaka huu ya Forbes imemtema kabisa, ikimaanisha Isabel hayumo kwenye orodha ya matajiri kwa sababu kipato chake cha sasa ni chini ya Dola bilioni moja.

Kuhitimisha makala fupi haya, jarida la Forbes halioni Isabel atakavyoweza kurudisha utajiri aliopoteza kwa mali zake kushikiliwa, ingawa maisha yake hayajashuka kiwango cha kuitwa masikini.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img