15.3 C
New York

Sima apendekeza maboresho haya wizara ya elimu

Published:

Na Ramadhan Hassan, Gazetini- Dodoma

Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima (CCM), ameishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuzingatia maeneo matano muhimu ya kipaumbele katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2025/2026, ili kuimarisha mfumo wa elimu nchini, hasa katika maeneo ya elimu ya ufundi, ajira kwa walimu na maandalizi kwa wanafunzi watakaohitimu darasa la saba mwaka 2027.

Akichangia bungeni leo Mei 13, 2025, wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, Sima amesema elimu ya ufundi inapaswa kupewa kipaumbele kwa kuongeza bajeti yake ili kuwawezesha vijana wengi kupata ujuzi wa kujitegemea.

“Nashauri Serikali kuongeza bajeti kwa elimu ya ufundi kwa kuwa vijana wengi wanahitaji ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa,” amesema.

Ajira kwa walimu wa kujitolea

Katika hoja yake ya pili, Sima amesema kuna haja ya Serikali kuweka mpango maalum wa kuwaajiri walimu wa kujitolea ambao tayari wamekuwa wakitoa huduma hiyo kwa muda mrefu bila ajira rasmi. Ameeleza kuwa kundi hilo linapaswa kupewa kipaumbele ili kuongeza nguvu kazi ya walimu nchini.

Maandalizi ya kidato cha kwanza 2028

Mbunge huyo pia ameonya juu ya changamoto inayoweza kutokea mwaka 2028, wakati wanafunzi wa kwanza walioanza darasa la awali bure mwaka 2021 watakapofika kidato cha kwanza. Kwa mujibu wa takwimu, kundi hilo linatarajiwa kuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Nataka kuiomba Serikali ifanye maandalizi mazuri kwa ajili ya kuwapokea hawa watoto watakaokuwa kidato cha kwanza mwaka 2028. Watakuwa wengi na wasipopangiwa walimu wa kutosha, watakosa haki yao ya msingi ya elimu,” amesema Sima.

Bajeti ya vyuo vya ufundi

Sima amehoji uamuzi wa Serikali wa kutenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 64 vya ufundi na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe, akieleza kuwa bajeti hiyo haijaainisha fedha kwa ajili ya vifaa vya kufundishia pamoja na ajira kwa walimu watakaofundisha katika vyuo hivyo.

“Tunajenga majengo lakini hatuoni bajeti ya vifaa wala walimu. Hili linahitaji kupitiwa upya ili vyuo hivi viweze kutoa mafunzo bora na yenye tija,” amesema.

Matumizi ya satelaiti kwa maendeleo ya kilimo

Katika pendekezo lake la tano, Mbunge huyo ametaja Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), akishauri kifanye mageuzi ya matumizi ya teknolojia ya satelaiti kuelekezwa kwenye sekta za kilimo na mazingira badala ya kuangazia taarifa za wanyamapori pekee.

“DIT wana mpango wa kurusha satelaiti yao mwaka ujao. Ningependa kuona inatumika kusaidia sekta ya kilimo na mazingira, hasa katika kukusanya taarifa muhimu za hali ya hewa, udongo, na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Wito wa kuongeza ajira kwa walimu

Mbunge huyo amehitimisha mchango wake kwa kuitaka Serikali kuongeza idadi ya walimu wapya ili kukidhi ongezeko la wanafunzi linalotokana na mabadiliko ya sera ya elimu bila malipo kuanzia awali hadi sekondari.

“Sera mpya ya elimu inaongeza idadi ya wanafunzi, hivyo kuna haja kubwa ya kuajiri walimu wapya na kuhakikisha wanapatiwa mazingira rafiki ya kazi ili kuongeza ufanisi,” amesema Sima.

Bunge linaendelea na mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img