1.6 C
New York

Watoto wanavyoyakabili mabadiliko ya tabianchi kwa kuotesha miti

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Watoto wa Tanzania wameonyesha juhudi kubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, wakihusishwa moja kwa moja kupitia miradi ya mazingira inayotekelezwa mashuleni.

Ushiriki wao sio tu kwamba unakuza uelewa wa umuhimu wa mazingira, bali pia unawapa nafasi ya kuchangia suluhisho la changamoto zinazotokana na tabianchi.

Ushiriki wa watoto katika masuala ya tabianchi kati ya Septemba na Oktoba 2024, watoto wa Tanzania walihudhuria mikutano ya utangulizi ya COP29 huko Baku, Azerbaijan, wakiwa sehemu ya mamia ya vijana kutoka mataifa 20, waliwasilisha mapendekezo yanayotaka serikali kuwashirikisha kikamilifu katika maamuzi yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.

WeWorld: Kichocheo cha ushiriki shuleni

Shirika la WeWorld limekuwa mstari wa mbele katika kusaidia watoto kushiriki katika miradi ya mazingira kupitia programu zake za Pamoja Tunaboresha Elimu, KITE, na MAMMIE.

Miongoni mwa wanufaika wa miradi hiyo ni pamoja na Shule ya Msingi Kawe, Dar es Salaam, ambako Klabu ya “Wakulima Chipukizi” imeanzishwa.

Watoto wanajifunza kulima mboga kama mchicha na nyanya, pamoja na kupanda miti 60, na wamedhamiria kuongeza miti mingine 50 ya matunda.

Miradi hii imeonyesha manufaa makubwa, ikiwemo kuboresha lishe ya watoto, kupunguza magonjwa yanayohusiana na tabianchi, na kuhifadhi mazingira ya shule.

Katika Shule ya Msingi Antakae, Muheza, mradi wa ECO School umeleta mwamko mpya.

Mwalimu Mkuu, Shaban Churi, anasema kuwa mradi huu una vipengele vya IVAC (Investigation, Vision, Action, Change) vinavyowawezesha watoto kutathmini changamoto za mazingira kwa vitendo.

Kupitia mradi huo, shule imeanzisha mpango wa kudhibiti mmomonyoko wa ardhi kwa kupanda nyasi na kuweka alama za kuhifadhi taka.

Pia, vibao vya maelekezo vimewekwa shuleni kusaidia wanafunzi na jamii kutunza mazingira.

Kwa mujibu wa Samweli Allen wa Nature Tanzania, lengo la miradi kama hii ni kusaidia shule kupata bendera ya kijani (Green Fly) inayotambua juhudi za mazingira duniani.

Mazingira shuleni yameboreshwa, afya za watoto zimeimarika, na uelewa wa thamani ya viumbe hai umeongezeka.

Mwajuma Hassan, mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Antakae, anasema, “Mazingira mazuri ya shule ni jukumu letu sote. Tunajitahidi kuelimisha wengine kuhusu utunzaji wa mazingira.”

Kwa kushirikiana na mashirika kama WeWorld na Nature Tanzania, watoto wa Tanzania wanajifunza na kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira. Juhudi hizi sio tu zinawapa elimu ya mazingira, bali pia zinawaandaa kuwa mabalozi wa tabianchi wa siku zijazo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img