Na Mwandishi Wetu, Gazetini-Mwanza
Shirika la Together Development Initiative (TDI) lililopo Nyakato, jijini Mwanza, limechukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti 1,500 ya matunda, kivuli, mbao, na dawa katika Shule ya Msingi Nyamilama, wilayani Magu, pamoja na kuchimba kisima cha maji.
Miti hiyo itapandwa katika shule iliyopo Kijiji cha Lugeye, Kata ya Kitongosima, Magu, kupitia mradi wa mabadiliko ya tabianchi unaofadhiliwa na Shirika la Global Fund kutoka Marekani. Mradi huo umezinduliwa leo shuleni hapo, huku walimu na baadhi ya watendaji wa serikali katika kata hiyo wakipewa elimu ya uhifadhi wa mazingira.
Akizungumzia mradi huo Julai 9, Afisa Programu wa TDI, Gozbert Mutta, alisema lengo ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Kata ya Kitongosima na kuhakikisha hali ya hewa inakuwa ya kijani kwa kupanda na kuitunza miti. Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa ndani ya miezi mitano.
“Kupitia mradi huu, tutatoa elimu ya uoteshaji, upandaji na utunzaji wa miti kwa wanafunzi wa klabu za mazingira. Watapata elimu hiyo na kuwafundisha wenzao shuleni, huku jamii inayozunguka shule hiyo ikijifunza utunzaji wa mazingira na upandaji miti kupitia mfano wa shule hiyo,” alisema Mutta.
Mutta aliongeza kuwa kupanda miti 1,500 kutasaidia kutengeneza madawati ya shule, kuongeza oksijeni, kuboresha ufaulu wa wanafunzi, kutoa dawa za asili na kuongeza lishe, hivyo kupunguza utapiamlo.
“Tunategemea kujenga kisima cha maji ambacho kitasaidia kumwagilia miti hiyo ili ikue vizuri. Pia, maji hayo yatatumika na wanafunzi kupata maji safi na salama ya kunywa,” alieleza Mutta. “Katika mradi huu, tunategemea Kata ya Kitongosima itapata elimu ya kutosha na kupanda miti kwa wingi ili hali ya hewa iwe ya kijani na kuwa mfano kwa maeneo mengine.”
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Nyamilama, Faith Katunzi, alisema anaamini mradi huo utakuwa na faida kubwa kwa shule yake na aliomba utekelezwe kwa mafanikio ili kuboresha mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Shule yetu ina ukubwa wa ekari 33 na imekuwa ikijitahidi kupanda miti, lakini inakabiliwa na uhaba wa maji. Tunategemea kisima hiki kitasaidia sana,” alisema Katunzi na kuongeza kuwa: “Kisima kitasaidia pia wananchi na kutatua kero ya maji. Tukipata maji, tutapanda miti mingi na kuboresha mazingira yetu.”
Afisa Kilimo wa Kata ya Kitongosima, Theodora Sokone, aliomba jamii kushirikiana kuhakikisha mradi unaanza na kwenda vizuri, huku akiwataka kulinda na kutunza miti itakayopandwa ili kufikia malengo ya mradi huo.
Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyamilama, Amos Martin, alisema, “Tutaitunza miti hiyo kwa kuiwekea mbolea na kumwagilia mara kwa mara. Miti inatusaidia mambo mengi na tutatoa elimu kwa wazazi wetu wasikate miti hovyo ili kulinda mazingira yetu kwa vizazi vijavyo.”
Martin aliongeza, “Tunashukuru TDI kwa kutuletea miti na kisima cha maji. Tunaahidi kuitunza miti hiyo vizuri na kuhakikisha inakua.”