3.2 C
New York

Wakazi wa kijiji cha Kondo waonywa kuhusu uharibifu wa misitu ya mikoko

Published:

Na Upendo Mosha, Gazetini- Bagamoyo

Wakazi wa kijiji cha Kondo, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, wameonywa kuacha tabia ya kuharibu misitu ya mikoko iliyopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi ili kudhibiti tatizo la uharibifu wa mazingira na mazalia ya samaki.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Uratibu na Ufuatiliaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF), Haika Shayo, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya mfuko huo inayotekelezwa katika wilaya hiyo, ambapo aliongozana na wadau wa maendeleo (wafadhili).

Shayo alisema tatizo la uharibifu wa mikoko katika eneo hilo lina athari kubwa kwa wananchi wa kijiji hicho ambao shughuli zao za kiuchumi zinategemea uvuvi. Alisisitiza kuwa hatua za kudhibiti hali hiyo zinapaswa kuchukuliwa mara moja.

“Tabia ya ukataji wa miti aina ya mikoko kando kando ya bahari imekuwa haijengi bali inabomoa, na waathirika wakubwa ni sisi wenyewe. Hivyo ni vema mkaacha na mkatunza mikoko,” alisema Shayo.

Mbali na hilo, Mkurugenzi huyo alitoa pongezi kwa juhudi ambazo zimeanza kuchukuliwa na wanufaika wa mfuko huo kwa kupanda mikoko zaidi ya 200,000 katika eneo lenye ukubwa wa hekta 12.

“Hii ni hatua ya kuigwa na kupongezwa kwani imeanza kurejesha uoto wa asili ambao ulikuwa umeharibiwa na kuanza kutoweka. Niwapongeze kwa hatua hii, na wenyewe mmekiri kwamba baadhi ya samaki adimu kama kaa wameanza kurejea baada ya mikoko hii kupandwa. Kwa maana nyingine, wananchi mtaendelea kunufaika moja kwa moja na uchumi wa buluu ambao serikali imekuwa ikiuhimiza,” alisema Shayo.

Aidha, aliwataka wakazi hao kuendeleza juhudi hizo kwa kupanda mikoko katika maeneo yaliyoathirika ili kuunga mkono juhudi za serikali za kufanya Tanzania kuwa nchi ya kijani na kuimarisha uchumi wa buluu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jafary Athuman, alisema wananchi walichukua hatua hiyo baada ya kuona athari za moja kwa moja za uharibifu wa mazingira ambao umeanza kukikumba kijiji hicho, ikiwemo mazalia ya samaki kutoweka na kuongezeka kwa kina cha maji.

Mwananchi wa kijiji hicho, Mwanaheri Maulid, alishukuru TASAF kwa kuingizwa katika mpango huo mwaka 2014 na kupongeza mfuko huo kwa ruzuku wanazotoa kwa walengwa. Alisema kwa upande wake ameweza kusomesha watoto wake na kufanya shughuli nyingine za kiuchumi.

“TASAF imetusaidia sana na tunaendelea kuona manufaa yake katika maisha yetu. Nawashukuru sana kwa msaada wao,” alisema Mwanaheri.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img