8.3 C
New York

Serikali kuandaa Muongozo mpya kupunguza migongano ya binadamu na wanyamapori

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Serikali imeanza kuandaa Muongozo mpya wa kuhakikisha kuwa inapunguza changamoto ya migongano kati ya binadamu na wanyamapori huku ikiwawezesha wananchi kunufaika na uhifadhi wa misitu na shoroba

Hayo yamebainishwa leo Mei 14, 2024 wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za mazingira Tanzania (JET) wanaotekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira uliofanyika katika ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC) Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Picha ya pamoja.

Akizungumza katika mdahalo huo Afisa Wanyamapori Mkuu na Mratibu Maliasili, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Hawa Mwechaga, amesema kuundwa upya kwa Muongozo huo kunalenga kupunguza wingi wa miongozo, sheria na kanuni ambazo zimekuwa zikiwabana wananchi wanaozunguka misitu na kusisitiza kuwa utarahisisha utekelezaji wake kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijiji.

“Tunakuja na Muongozo mwingine wa kuhakikisha kwamba raslimali uliyonayo inakufanya wewe uinuke kiuchumi pia utasaidia wananchi kuwaona wanyamapori na misitu kama fursa badala ya changamoto kama ilivyo hivi sasa.

“Awali, kulikuwa na changamoto kwamba wananchi wanazungukwa na misitu au hifadhi lakini wanachangamoto na kuna miongozo na sera nyingi zinazowabana, hatua ambayo ilikuwa ikisababisha ukataji miti kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi,” amesema Hawa.

Amesema katika kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika, Tamisemi imeanza kuwashirikisha wananchi waliojirani na shoroba na misitu kujiinua kiuchumi huku wakihifadhi mazingira.

Afisa Wanyamapori Mkuu na Mratibu Maliasili, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Hawa Mwechaga(kushoto) akizungumza wakati wa mdahalo huo, kulia ni Dk. Fortunata Msofe kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.

“Mfano, kule katika Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi kuna misitu ya Tongwe Mashariki, Tongwe Magharibi na mlima Mtakata wenye vijiji nane kwasasa wananchi wananufaika kupitia biashara ya kaboni ambapo kwa mwaka huu 2024 wamepata gawio la Sh bilioni 14.

“Tumefanya vile sababu kule ndani kuna sokwe ambao wako hatarini kutoweka pia kuna ushoroba ambao unasaidia wanyamapori waweze kuingia ndani ya hifadhi zetu ikiwamo ile ya Gombe, hivyo Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na wadau kama USAID kupitia mradi wao wa Tuhifadhi Maliasili tunawawezesha wananchi kupata fedha na kuboresha maisha yao.

“Utaona kwamba kule Tanganyika kupitia kaboni wananchi waidi ya 250 wamepata ajira, wakazi wote wa vijiji nane wamepata bima ya afya, zahanati ya kisasa na fursa nyingine nyingi, hivyo eneo hili la biashara ya kaboni pamoja na kuwa jipya kwetu kama nchi lakini ni fursa kwa wananchi wetu na nafasi nyingine ya kulinda wanyama wetu,” amesema Hawa.

Ameongeza kuwa hekta milioni 21 za misitu iko kwenye ardhi za vijiji, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2015, kati ya hizo, hekta milioni 3.5 zinamilikiwa na halmashauri pamoja na misitu mingine inayomilikiwa na jamii.

Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana Waziri wa Maliasili na Utalii, Angela Kairuki alisema Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TFS, TAWA, TANAPA na Ngorongoro (NCAA) ilipokea zaidi ya kampuni 25 za kigeni zilizoonyesha nia ya kufanya biashara ya kaboni kutoka nchi za Kenya, Russia, Singapore, Marekani, Canada, Marekani (UAE), Uswisi, Uingereza, Estonia na Italia ambapo baadhi ya hizo tayari wameshaingia makubaliano ya awali (MoU) na mazungumzo yanaendelea kupitia taasisi husika na chini ya usimamizi wa National Carbon Monitoring Center-NCMC.

“Maeneo yanayotarajiwa kuwekeza ni pamoja na Misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu, Misitu ya Vijiji, Miradi ya Upandaji Miti, Hifadhi za Jamii za Wanyamapori, Misitu ya Hifadhi na Hifadhi za Taifa, Uwekezaji husika unakadiriwa kuwa zaidi ya Dola bilioni 20 kwa mwaka,” alisema Waziri Kairuki.

Aidha, akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam mapema leo Waziri wa Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira), Dk. Suleiman Jafo amesema hadi sasa kampuni 44 zimeshajisajili kuwekez katika biashara hiyo.

“Mpaka sasa kampuni 44 zimeshajisajili kufanya biashara ya kaboni nchini kazi inayoanywa na kituo cha SUA mkoani Morogoro,” amesema Dk. Jafo.

Akizungumzia katika mdahalo huo kuhusu mkakati wa Serikali wa kuongoa Shoroba, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Fortunata Msofe, alisema kati ya shoroba 61 zilizotambuliwa Serikali imelenga kuongoa shorioba 20 ambapo kati ya hizo mbili ziko hatua ya mwisho.

“Katika shoroba 20 za kipaumbele hadi sasa shoroba mbili za Nyerere Selous-Udzungwa na ile ya Kwakuchinja inayounganisha mbuga ya Tarangire na Lake Manyara ambazo ziko katika hatua ya mwisho na hii ni kutokana na juhudi kubwa ambazo zimefanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wakiwamo USAID kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili.

“Shoroba nyingine zilizobaki tunaendelea kukuasanya nguvu ya fedha kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha kuwa nazo tunazikamilisha kama tulivyopanga,” amesema Dk. Fortunata.

Akizungumzia mdahalo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET), John Chikomo, amesema lengo ni kuendelea kuwengea uelewa wa kutosha waandishi wa habari kuhusu migongano ya binadamu na wanyama pori na uelewa wa namna ambavyo tunaweza kuishi na wanyama kwa kutegemeana.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img