8 C
New York

GGML yaja na teknolojia za kisasa maonesho ya OSHA Arusha

Published:

Na Mwandishi Wetu, Arusha

KATIKA kuelimisha wananchi na washiriki wa maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi namna ya kuzingatia usalama wawapo katika shughuli zao, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeleta vifaa mbalimbali vya kisasa ili kutoa fursa kwa washiriki hao kujifunza teknolojia za kisasa za uokoaji.

Afisa usimamizi wa tabia na uimarisha miamba, Innocent Lusuva akiwapatia maelezo baadhi ya maofisa wa jeshi la polisi waliotembelea banda la GGML katika maonesho ya OSHA na kujifunza namna rada inayofuatilia mienendo ya kuta za miamba katika uchimbaji, inavyofanya kazi.

Hayo yamebainishwa na Meneja Usalama kutoka GGML, Isack Senya wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho hayo yanayofanyikakwenye viwanja vya General Tyre jijini Arusha na kuratibiwa na wakala wa usalama na afya mahali pa kazi (OSHA).

“Kama kawaida GGML kwa kutambua umuhimu wa afya na usalama kazini na ikiwa ni tunu yetu ya kwanza, GGML ina wawakilishi zaidi ya 45 kwenye maonesho haya wanaotoa elimu mbalimbali kuhusu masuala ya afya na usalama kazini,” alisema Senya.

Senya alisema katika maonesho hayo wamekuja na vifaa mbalimbali ikiwamo rada maalumu ambayo ina uwezo wa kutambua ukuta ambao una udhaifu au unaoweza kuanguka pindi shughuli za uchimbaji mgodini zikiendelea. Alisema rada hiyo hutoa ripoti mapema ili kuondoa watu kwenye maeneo husika iwapo ukuta au mwamba huo unataka kuanguka.

“Kifaa hiki kinaangalia eneo la uchimbaji na kinavyozunguka kinapiga picha za satellite. Picha hizi zinarejeshwa kwenye mfumo na kuona kama kuna mwenendo wowote wa ukuta unaoweza kuleta athari, inamtahadharisha mtalaamu na kuchukua hatua stahiki.

Daktari wa GGML aliyebobea katika magonjwa yatokanayo na kazi, Cretus Karwan akimpatia vipimo mmoja wa vijana waliotembelea banda la GGML na kupatiwa huduma za awali za upimaji wa afya katika maonesho ya OSHA yanayoendelea jijini Aruha.

“Rada hii ilisaidia sana mwaka 2007 ambapo kulitokea maporomoko makubwa sana ya ukuta lakini kutokana na kifaa hiki, yalibainika mapema na kuchukua hatua stahiki ikiwamo kudhibitiwa,” alisema.

Alisema pia timu ya GGML imekuja na mambo mengi zaidi na tofauti kulingana na kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “mabadiliko ya tabia nchi na athari usalama na mazingira.

“Tumeona madhara mbalimbali yaliyotokana na mabadiliko ya tabia nchi hivyo tumeona ni muhimu sasa kuhakikisha elimu zetu tunazotoa zinajikita kwenye maeneo hayo,” alisema na kuongeza pia katika banda hilo wanatoa huduma za awali za afya ikiwamo upimaji wa magonjwa ya kisukari na presha.

Mbali na rada pia alisema GGML wameleta boti ya uokoaji majini, vifaa vya uokoaji katika uchimbaji chini ya ardhi pamoja na kutoa elimu kuhusu majanga makubwa na vidhibiti majanga ambayo yanaweza kuepukwa.

Alisema katika maonesho hayo tayari wameshatoa mafunzo ya namna ya kujikinga na kukabiliana na majanga ya moto kwa akina mama lishe 50 wa mkoani Arusha pamoja na kuwagawia mitungi ya gesi ya kupikia.

Pia alisema wanatarajia kutoa mafunzo kwa madereva pikipiki kuwaelimisha namna ya kuzingatia usalama pindi wawapo katika shughuli zao.

Alisema kutokana na mifumo imara ya udhibiti majanga pamoja na kuzingatia masuala ya afya na usalama kazini kwa muda wa zaidi ya miaka 14 sasa ndani ya GGML hakuna kifo kilichotokea kutokaa na shughuli hizo za uchimbaji.

Ofisa wa idara ya manunuzi na mikataba akimpatia maelezo mmoja wa wananchi wawaliojitokeza kutembelea banda la GGML katika maonesho ya OSHA na kujifunza namna kuzingatia usalama katika shughuli zao za kila siku.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img