8.5 C
New York

“Tunataka wasichana wafikie ndoto zao maishani”

Published:

Na Malima Lubasha, Gazetini

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania la wilayani Serengeti mkoani Mara linahifadhi wasichana 171 katika nyumba salama ili kuwaepusha na ukeketaji katika maeneo ya Butiama na Mugumu.

Aidha, mbali na kukimbia ukeketaji pia wapo waliokimbia ndoa za utotoni, ubakaji, vipigo na mazingira hatarishi.

Mkurugenzi wa Shirika hilo la Hope for Girls and Women in Tanzania,Rhobi Samwel amebainisha hayo hivi karibuni katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti wakati akiwasilisha taarifa kuhusu shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo kwa kuomba madiwani kukomesha vitendo wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana.

Amesema tangu kuanza kwa shirika hilo mwaka 2017 lengo kuu ni kuondoa ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike na mwanamke, kuondoa mila kandamizi, kutoa uhifadhi kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, kuwaendeleza kielimu watoto wa kike ili wafikiea ndoto zao na kuwajengea uwezo katika ufundi na ujasiriamali ili waweze kujipatia kipato chakuendeshea maisha yao.

Kwa mujibu wa Samwel, tangu shirika hilo lianzishwe limepokea na kuwahudumia wahanga 4,368 ambao walikuwa na kesi za ukatili wa aina tofauti tofauti ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni, ubakaji, vipigo na manyanyaso ambapo waliweza kupata huduma za chakula, matibabu, ushauri wa kisaikolojia, malazi na mahitaji ya kielimu.

Amefafanua zaidi kuwa kupitia vituo vya nyumba salama Butiama na Mugumu wahanga wa ukatili wa kijinsia wanaoendelezwa kielimu kufikia ndoto zao  hawajawahi kwenda shule.

Amesema kwa wasichana hao waliopo darasa la kwanza ni 7, shule ya msingi kutwa 46 bweni 4, sekondari kutwa 47 Bweni 12, ufundi na ujasiriamali 30 ambapo elimu ya vyuo vya kati na chuo kikuu ni 10.

Aidha, katika kujenga mahusiano baina ya wahanga na wazazi na walezi wao kutokana  na kuhifadhiwa nyumba salama kwa muda, katika kipindi cha mwaka 2022 waliweza kuwaunganisha wahanga 237 na familia zao baada ya familia hizo kuridhia na kujiridhisha na mazingira kuwa yako salama.

Kwa mwaka 2023 wahanga 43 wameunganishwa na wazazi na walezi wao wakiwa wamepta elimu na ufundi wa aina mbalimbali.

Alisema kwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii wilaya na Dawati la jinsia wilaya ya Serengeti waliunganisha wahanga hao na familia zao kupitia nyumba salama ya Mugumu na Butiama ambapo wahanga hao walitokea wilaya za Rorya, Butiama, Serengeti, Arusha na Tarime.

Kulingana na Mkurugenzi huyo kituo kinakabiliwa na changamoto ambazo ni jamii na baadhi ya wazazi kuendelea kushikilia mila na desturi ya ukeketaji, ndoa za utotoni kwa faida yao, baadhi ya watu kubeza shughuli zao na kuwatolea matusi ya aina mbalimbali, ufinyu wa eneo na fedha za ujenzi wa kituo.

Aidha, ameomba ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji, Polisi Wilaya, Madiwani na wadau mbalimbali kuendelea kusaidiana na kituo hicho kukomesha ukatili huo wa kijinsia katika maene yao ili watoto wa kike na wanawake waweze kufikia ndoto zao katika maisha.                                                              

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img