Na Faraja Masinde, Gazetini
TAFITI mbalimbali za afya zimethitisha kuwa chanjo huzuia takribani vifo milioni mbili hadi tatu kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa chanjo duniani.
Aidha, wakati tafiti zikieleza hayo, asilimia 86 ya Watanzania wenye umri wa kuanzia miaka 18 walikuwa wamepata chanjo kamili ya Uviko-19 hadi kufikia kufikia Desemba, mwaka jana.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Afya kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Desemba 2022 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma.
“Ndani ya miezi sita, tumefanya vizuri kwenye utoaji wa chanjo dhidi ya Uviko-19, tumeweza kufikia asilimia 86 ya Watanzania wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kupata dozi kamili ya chanjo dhidi ya Uviko-19, ukilinganisha na asilimia 24.7 hadi kufikia Juni, 2022,” anasema Waziri Ummy.
Akizungumzia kiwango cha dozi za Uviko-19 zilizotumika hadi sasa, Ummy anasema hadi kufikia Desemba 31, 2022, jumla ya dozi 46,848,520 zilikuwa zimepokewa, ambapo dozi 41,581,670 zilikuwa zimesambazwa nchi nzima, huku kiasi cha chanjo zilizosalia kwenye bohari ya kutunzia chanjo kikiwa ni 5,266,850, zote zikiwa ni aina ya Johnson & Johnson.
Aidha, kwa mujibu wa Waziri Ummy, hivi karibuni Wizara itazindua ‘Booster’ ya dozi ya Uviko-19 ili wananchi waweze kuongeza kinga zaidi dhidi ya ugonjwa huo na kusema kuwa ni hiari kwa mtu yeyote kwenda kupata chanjo hiyo.
Wanaume na chanjo
Hata hivyo, wakati hali ikiwa hivyo, bado msukumo ni mdogo kwa wanaume, ambapo wengi wao hawaoni uharaka wa kupata chanjo ya Uviko-19.
Mathalan, takwimu za Wizara ya Afya za Agosti, mwaka jana, zinaonesha kuwa kiwango cha uchanjaji kwa wanaume kiko chini, ikilinganishwa na wanawake.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha takwimu hizo, Kaimu Mratibu – Elimu kwa Umma na Ushirikishaji Jamii wakati wa Dharura (RCCE), Juliana Mshama, alisema tangu kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo Julai 28, 2021, kwa kuzinduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kiwango cha uchanjaji kwa wanaume kimekuwa cha kusuasua.
“Mwenendo wa uchanjaji wa chanjo ya Uviko-19 kwa mtazamo wa jinsia unaonekana kwamba bado wanaume wako nyuma, ukilinganisha na wanawake.
“Mfano, takwimu za mwisho za uchanjaji zinaonesha kuwa kiwango cha wanawake waliochanja ni asilimia 54, ikilinganishwa na asilimia 46 ya wanaume. Hivyo, utaona kwamba bado kundi la wanaume liko nyuma,” anasema Juliana.
Jackson Maxmilian (46), mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam, anasema: “Mimi sikupata chanjo ya Corona kutokana na habari nyingi tulizokuwa tunazisoma kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo ya kuambiwa utageuka ‘zombie’ endapo ungechanja.”
Kwa upande wake, Juma Hussein (45), anasema kuchanja hakukuwa kipaumbele kwa sababu hakuugua ugonjwa huo na hana mpango wa kusafiri kwenda nje ya nchi.
“Niwambie hizi chanjo walikuwa wanazikimbilia wafanyabiashara wanaokwenda nje ya nchi mara kwa mara. Sasa ukiniangalia mimi sina hata huo mpango wa kwenda nje na sijawahi kuugua huo ugonjwa, naanzaje kukimbilia chanjo hizo?” anahoji Hussein.
Godlisten Maipo, mkazi wa Kijichi, Dar es Salaam, naye ana hoja ya aina hiyo, akisema taarifa za madhara za chanjo alizozipata kupitia simu janja yake (smart phone) zilimfanya asione umuhimu wa kuchanja.
“Mara nilisikia chanjo zinasababisha mwanaume kuwa tasa (kushindwa kuzalisha). Pia, tukaambiwa chanjo hizo ni mbinu za wazungu kutupunguza. Kwamba ukitumia unaishi kwa muda mfupi tu,” anasema.
Wakati huo huo, Mashimba Joseph (74), mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, anasema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Dk. John Magufuli, haikuonesha kutilia uzito chanjo ya Corona, hivyo naye hakuona tija ya kuchanja.
“Utakumbuka, wakati ule Hayati Magufuli aliweka wazi msimamo wake juu ya chanjo, akisema ni njama za wazungu kutuibia. Hii iliwafanya Watanzania wengi, wakiwamo wanaume, kuona chanjo haina tija. Nikiri kwamba nilipuuzia kuanzia kipindi kile na hadi leo sidhani kama itatokea kuchanja,” anasema Mashimba.
Naye mtaalamu wa afya katika Zahanati ya Omec ya Gongo la Mboto, Dar es Salaam, Anastazia Kapinga, anasema idadi ya wanaume kuwa ndogo katika uchanjaji inatokana na saikolojia ya kundi hilo.
“Kisaikolojia, wanaume wana asili ‘yaku-reason’. Sisemi wanawake wanakurupuka, bali nachotaka kieleweke ni kwamba wanaume hupenda kujiridhisha zaidi, kabla ya kukubali au kukataa jambo.
“Ninaamini, endapo elimu itaendelea kutolewa kwa kiwango cha juu, basi wanaume nao wataanza kuingia katika uchanjaji. Kwa asili, huwa wanapenda kujiuliza mara kadhaa, kabla ya kukubali jambo,” anasema Anastazia.
Huku chanjo ikikabiliwa na ‘upinzani’ kutoka kwa wanaume, Mwajuma Ramadhan (36), mkazi wa Kinondoni Biafra, Dar es Salaam, ana mtazamo tofauti.
“Unajua mimi ni mama, hivyo ni jukumu langu kuhakikisha nyumbani kwangu kuko salama. Chanjo ilikuwa ni kinga kwa ajili ya wanangu. Fikiria mimi kama ningeumwa, nani angewapikia watoto wangu? Nani angewaandaa kwenda shule?” anasema Mwajuma.
Katika hatua nyingine, Johari Joseph (41), mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, naye anaungana mkono hoja ya kuchanja, akisimulia namna Uviko-19 ilivyogharimu maisha ya mume wa jirani yake.
“Wakati watu wanahamaishana kuchanja, niliwaambia majirani zangu kuwa ugonjwa huu ni mbaya na sisi tuna watoto, hivyo ni bora tupate chanjo.
“Wachache waliniunga mkono na wengine, akiwamo mume wa jirani yangu, waligoma kabisa kuchanja. Matokeo yake baada ya siku kadhaa alianza kujisikia vibaya na tuliishia kumpoteza, hili lilikuwa fundisho kwa wengi,” anasema Johari.
Sera ya Taifa ya Afya
Sehemu ya Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 inahimiza kuhamasisha wananchi kuhusu maradhi yanayoweza kuzuilika, ili waweze kuyatambua na kutafuta mbinu za kuyadhibiti.
Kwa upande mwingine, Sera ya Afya inahimiza elimu kwa kila mwananchi ili aelewe kuwa anawajibika moja kwa moja kuitunza afya yake na ile ya familia yake.
Katika hilo, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, anatolea mfano mwenendo wa chanjo ya Uviko-19 nchini akisema: “Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika utoaji wa chanjo kwa walengwa.
“Tumefikia hatua nzuri katika mapambano dhidi ya Uviko-19. Kama tulivyotokomeza Ndui, Magonjwa ya Dondakoo, Kifaduro, Polio na Pepopunda, tutafanikiwa pia kumaliza Uviko-19. Mtu ambaye hajapata chanjo ana hatari ya kuwaambukiza wengine kwa sababu hana kinga kamili ya mwili,” anasema.
WHO
Dk. Boniface Makelemo ni Mwakilishi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya duniani (WHO) anaisifu Tanzania kwa namna ilivyopiga hatua katika utoaji chanjo ya Uviko-19.
“Tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua thabiti zinazochukuliwa kupunguza athari za magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,” anasema na kuongeza:
“Tunaona utoaji wa chanjo ya Uviko-19 ukiwa na mwamko mkubwa, ambapo asilimia kubwa ya Watanzania wamepata chanjo. Haya ni mafanikio makubwa na juhudi hizi za Serikali zinapaswa kuendelea kuungwa mkono,” anasema Dk. Makelemo.
Anaongeza kuwa WHO na Umoja wa Mataifa (UN) na washirika wao wote wa chanjo wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujitolea rasilimali watu na fedha zinazohitajika ili kuinua kiwango cha uchanjaji.