4.1 C
New York

‘Watoto 340 watelekezwa’ ndani ya miezi 12 Songwe

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Takwimu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa 2022-2023 wanawake 340 wenye watoto walitekezwa na wenza wao huku wengine 17 wakipigwa na wenza wao.

Hii ni sawa na kusema kwamba watoto 340 wamelazimika kukosa malezi ya baba na mama kwa pamoja jambo ambalo halina afya katika ustawi wa mtoto na familia kwa ujumla. Kwa maneno mengine ni kwamba kila mwezi watoto 28 wanatelekezwa ikiwa ni wastani wa watoto 7 kila wiki.

Mbali na wanawake hao, wasichana 54 wameripotiwa kubakwa wilayani humo ndani ya kipindi hicho.

Ikumbukwe kuwa matukio hayo yote ni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja yakihusisha wilaya moja pekee ya Mkoa wa Songwe kati ya nne zinazounda mkoa huo ambazo ni, Songwe, Mbozi, Momba na Ileje yenyewe.

Lucy Mwani kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Ileje Idara ya Maendeleo ya Jamii anasema kuwa katika kipindi hicho halmashauri kupitia Ustawi wa Jamii ilipokea jumla ya matukio 55 ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto kubakwa hali ambayo jamii inapaswa kushirikiana kupinga vitendo hivyo.

Mkuu wa Wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, akizungumza hivi karibuni juu ya matukio hayo anakiri kuwa kumekuwa na changamoto ndani ya wilaya hiyo.

“Kwakweli takwimu za watoto kufanyiwa ukatili kwa Ileje ndani ya mwaka mmoja zimekuwa za kutisha licha ya wengine kutobainika, jamii inatakiwa ishirikiane, elimu itolewe ili watoto waepushwe na magonjwa ya kuambukizwa, mimba za utotoni na kulawitiwa kwa watoto wa kiume.

“Watoto 55 ni wengi sana na hapo kumbuka kuwa ni Wilaya ya Ileje pekee na siyo mkoa mzima, jamani ni aibu sana na huenda kuna wengine ambao wamefanyiwa ukatili na hawajabainika, hivyo kazi kubwa inapaswa kufanyika ikiwamo kuongeza kasi ya kufichua matukio haya kwa kulipoti ustawi wa jamii,” anasema Mgomi.

Jamii ielimishe watoto

Mgomi anasema kuwa jamii inapaswa kuelimisha watoto kutambua namna wanavyoweza kufanyiwa ukatili na kuwambia wapi wanapaswa kulipoti ili wahusika wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.

“Sisi wazazi na walezi tutenge muda kuzungumza na watoto kujua maendeleo yao na kuwapa ujasiri wa kukataa na kukemea kwani wasipofanya hivyo wataharibiwa ndoto zao,” anasema Mgomi.

Sifa Leonard ni mwanafunzi wa shule ya wasichana Ileje aambapo anasema kuwa kuongezeka kwa ukatili dhidi ya watoto kunatokana na baadhi yao kukosa elimu ya malezi na namna ya kukabiliana na vishawishi.

Wanaume kutaka kulelewa ni sababu

Mkazi wa Songwe Godbless Ngodo anasema kuwa baadhi ya matukio ya wanawake kutelekezwa wakiwa na watoto na wenzi wao yanachochewa kwa sehemu kubwa na wanaume ambao huanzisha uhusiano na wanawake hao kwa ajili ya kujipatika kipato na pindi wanapobainika kuwa wenzi wao ni wajawazito hutokomea kusikojulikana.

“Unajua kaka matukio haya ya watoto kutelekezwa hapa Ileje yanachochewa zaidi na wanaume, unajua wanaume wa huku baadhi yao hawapendi sana kujishughulisha hivyo unakuta kwamba wanataka kulelewa na wanawake, lakini pindi tu inapobainika kuwa mwanamke aliyenaye amepata ujauzito basi hutoweka na kwenda kuanzisha uhusiano na mwanamke mwingine.

“Hii ni moja ya tabia inayochochea kuendelea kuwapo kwa matukio haya ya watoto kulekezwa, jambo la msingi ni jamii kupewa elimu ili kusaidia kudhibiti aina hii ya ukatili kwani unapomtelekeza mama na mtoto hata ustawi wa mtoto huyo achilai mbali elimu unakuwa umeviweka shakani, hii kwa maeneo mengine tunasema kwamba akina baba hawa wanakimbia malezi kwa watoto wao na kuacha mzigo huo kwa akina mama,” anasema Ngodo.

Waziri Mkuu

Mei 14, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika hafla ya Mtoko wa Mamailiyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani aliitaka jamii ishirikiane na akinamama katika malezi ili kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania.

“Akinababa washirikiane na akinamama katika malezi ya watoto kwani kidole kimoja hakivunji chawa. Sote tumelelewa na akinamama zaidi, lakini akinababa tunapaswa vilevile kujipa muda na kufuatilia mwenendo wa tabia ya mtoto kuanzia asubuhi mpaka usiku,” alisema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa jamii kuheshimu na kuthamini mchango wa mama katika malezi. “Kama wahenga walivyosema, kuzaa siyo kazi ila kazi ni kulea mwana, tushirikiane na akinamama wote katika malezi ili kwa pamoja tuweze kujenga jamii yenye maadili ya Kitanzania,” alisema Majaliwa na kuongeza kuwa;

“Ninatambua kuwa mama zetu katika karne hii wanafanya shughuli nyingi za kiuchumi kwa ajili ya ustawi wa familia na Taifa kwa ujumla. Niwasihi sana muendelee kuwa vinara katika suala la malezi ya watoto,” alisisitiza Waziri Mkuu.

Sambamba na hayo, Waziri Mkuu aliwataka wazazi na walezi wajitambue kuwa wao ni taasisi muhimu tena ya kwanza katika malezi ya mtoto. “Timizeni wajibu wenu, shirikianeni na taasisi za kiserikali ili kukuza na kuimarisha maadili kwa watoto wenu pamoja na kutenga muda wa kuwafuatilia ili kujua changamoto zao na kuwelea ipasavyo.

Mhariri Mkuu wa Clouds na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Joyce Shebe anasema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuuelimisha umma kuhusu maadili na malezi kupitia makala na vipindi maalum ambavyo vitalenga kukabiliana na changamoto za watoto za wakati huu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img