WATANI wa jadi, Simba na Yanga wanakutana Jumamamosi Desemba 11, 2021 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara(NBC Primier League) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Simba ndio wenyeji wa mchezo huo ambao waanamini kuwa wanaamini kama si Meddie Kagere basi Bernard Morrison walio kwenye ubora msimu huu watawapa furaha hivyo hivyo kwa Yanga kama si Fiston Mayele basi atakuwa Feisal Salum ambao si rahisi kukabika.
Hata hivyo, mchezo huu pamoja na mambo mengine unakutanisha mabenchi ya ufundi ambayo viongozi wake wamewahi kuhudumu kwenye vilabu ya Real Madrid na Fc Barcelona ambazo ni miamba inayoshiriki ligi kuu ya Hispania maarufu kama La Liga.
Upande wa Simba, Kocha wake Mkuu, Pablo Franco, yeye amewahi kuwa kocha msaidizi wa Real Madrid mwaka 2018.
Upande wa Yanga, Kocha wake Msaidizi Cedric Kaze, yeye amewahi kuwa kwenye Klabu ya Fc Barcelona akihudumu kama kocha wa vijana.
Hii ni sawa na kusema kwamba ‘El Classico’ kwa maana ya ‘dabi’ ya Hispania inahamishiwa Dar es Salaam hii leo, kila mmoja anasubiri kuona ni upande gani utakaoibuka na furaha hii leo kwenye dimba hilo la Benjamini Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.
Mbali na uhondo huo wa ‘El Classico’ pia mchezo huo unahusisha jumla ya mataifa 14 ya Afrika ikiwamo Tanzania, hii inamaana kwamba Simba na Yanga zimesajili wachezaji kutoka mataifa mbalimbali.
Upande wa Simba wa wenyewe una wachezaji kutoka mataifa 11 ikiwamo Tanzania, huku upande wa Yanga ukiwa na wachezaji kutoka mataifa sita ikiwamo Tanzania. Zaidi angalia usanifu wetu.