*Yasema unatishia uhai wa binadamu na bahari
Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Mei 23, ni Siku ya Kimataifa ya Kasa wa Baharini, Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimetoa onyo kali kuhusu kuendelea kwa vitendo vya uwindaji haramu wa kasa wa baharini nchini, vikisema kuwa hali hiyo si tu inaathiri uhai wa viumbe hao walioko hatarini kutoweka, bali pia inatishia maisha ya binadamu na uhai wa mazingira ya bahari.

Kwa mujibu wa JET, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye bahati ya kuwa na spishi tano kati ya saba za kasa wa baharini wanaotambuliwa duniani. Hata hivyo, kila moja ya spishi hizi imeorodheshwa na IUCN kuwa iko katika hatari ya kutoweka kutokana na vitendo vya binadamu.
“Uwindaji haramu wa kasa na matumizi yao kama chakula vinaendelea kufanyika licha ya kuwa kinyume cha sheria za nchi yetu,” amesema John Chikomo, Mkurugenzi Mtendaji wa JET. “Ni jambo la kusikitisha kuona jamii nyingine bado zinaamini kuwa nyama au mayai ya kasa yana uwezo wa kuongeza nguvu za kiume au kutibu maradhi, hali ambayo si ya kisayansi na sasa imeanza kugharimu maisha ya watu.”
Ameeleza kuwa tukio la hivi karibuni lililotokea Machi 2024 kisiwani Pemba, ambapo watoto wanane na mtu mzima mmoja walifariki baada ya kula nyama ya kasa, linapaswa kuwa funzo kwa jamii nzima. Watu wengine zaidi ya 70 walilazwa hospitalini kutokana na sumu ya chelonitoxism – aina ya sumu hatari inayopatikana kwenye baadhi ya kasa.
Mbali na hatari hiyo kwa binadamu, kasa pia wanakumbwa na changamoto nyingine nyingi ikiwemo kunaswa kwenye nyavu za uvuvi, uharibifu wa maeneo ya kutagia, na uchafuzi wa mazingira hasa wa plastiki. Takwimu kutoka ripoti ya State of the World’s Sea Turtles zinaonyesha kuwa kasa wasiopungua 1,000 hufa kila mwaka kwa sababu ya kumeza plastiki wakidhani ni chakula.

Chikomo amesema kuwa JET imekuwa ikishirikiana na mashirika mbalimbali ya uhifadhi kama Sea Sense kuelimisha umma kuhusu athari za uwindaji wa kasa na umuhimu wa kuwalinda kwa ajili ya vizazi vijavyo. “Kasa ni viumbe muhimu katika mfumo wa ikolojia ya bahari. Kupotea kwao kunaathiri moja kwa moja afya ya miamba ya matumbawe, samaki, pweza na hata ustawi wa uchumi wa jamii za wavuvi.”
Ameongeza kuwa JET imekuwa ikihamasisha waandishi wa habari kupitia mafunzo maalumu ya namna ya kuandika habari za uhifadhi wa kasa. Pia wamekuwa wakishiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kasa Duniani, mfano mwaka 2018 waliratibu shughuli hizo kijijini Chongoleani, Tanga, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
JET inatoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa kasa kwa kuacha uwindaji haramu na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapoona vitendo vya uharibifu wa bahari. “Kama jamii, tunapaswa kuchukua hatua sasa – kuwalinda kasa ni kuyalinda maisha yetu sote,” amesema Chikomo.