21 C
New York

Tembo, Simba watesa wananchi Serengeti

Published:

Na Malima Lubasha,Gazetini-Serengeti

Wakazi wa Kata ya Nagusi, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wameelezea hofu na wasiwasi mkubwa kutokana na ongezeko la matukio ya uvamizi wa wanyamapori, hususan tembo na simba, kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika makazi yao, hali inayosababisha uharibifu wa mazao, mifugo na kuhatarisha usalama wao.

Akizungumza na Gazetini, Diwani wa Kata hiyo, Andrew Mapinduzi, amesema vijiji vya kata hiyo vinakabiliwa na changamoto kubwa ya wanyamapori kuvamia mashamba na maeneo ya malisho ya mifugo, huku simba wakisogea karibu na makazi ya watu na kuua mifugo, na tembo wakiharibu mazao mashambani.

“Kwa sasa sina takwimu kamili za mifugo au watu walioathirika moja kwa moja, lakini hali ni mbaya. Simba wanavamia mazizi na kula mifugo, huku tembo wakiharibu mashamba,” amesema Mapinduzi.

Ameeleza kuwa changamoto hiyo inatishia maisha ya wakazi wa kata hiyo, hivyo kuomba serikali iingilie kati kwa kuchukua hatua madhubuti. Miongoni mwa maombi yake matatu kwa serikali ni: Kutafuta suluhisho la kudumu la wanyama hao kuvamia makazi ya watu. Kuweka uzio wa umeme (fensi) kama ilivyofanyika katika maeneo ya kaskazini ya hifadhi ili kuwazuia tembo na simba kuingia kwenye vijiji vya kata ya Nagusi na kuboresha utoaji wa kifuta machozi kwa waathirika wa uharibifu huo, akisema fidia hiyo imekuwa ikichelewa kufika na haitolewi kwa uhalisia kulingana na uharibifu halisi wa kila mkulima au mfugaji.

Watoa taarifa wa wanyamapori katika vijiji vya Singisi na Iharara, Rashid Manota na Jumapili Mahega, wamesema kuwa wamekuwa wakishirikiana na wananchi kufuatilia mienendo ya wanyama hao na kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji ili hatua zichukuliwe kwa haraka na mamlaka husika.

“Tembo wanavamia mashamba na kuharibu mazao, simba nao wanavamia mazizi na maeneo ya malisho usiku na kuua mifugo. Taarifa zote za uharibifu zipo ofisi za vijiji,” amesema Mahega wa kijiji cha Iharara.

Aidha, Manota wa kijiji cha Singisi amesema kuwa wiki mbili zilizopita, mnyama aina ya kiboko alivamia kijijini hapo, lakini kwa kushirikiana na TAWA na Grumeti Reserves walifanikiwa kumrudisha salama hifadhini kabla hajaleta madhara.

Wakizungumza kwa pamoja, watoa taarifa hao wamesisitiza kuwa uvamizi wa wanyamapori umeathiri sana sekta ya kilimo na ufugaji katika kata hiyo, hali inayotishia usalama wa chakula kwa wakazi ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji.

Hali hiyo imekuwa ikijirudia katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Serengeti. Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alitembelea kijiji cha Makundusi ambapo pia wakazi walilalamika kuhusu tembo na simba kuvamia makazi yao na kusababisha uharibifu wa mali.

Kufuatia malalamiko hayo, Kanali Mtambi aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kupitia Idara ya Wanyamapori kuanzisha kituo maalum cha ufuatiliaji wa wanyama wakali na waharibifu ili kudhibiti matukio hayo na kuwalinda wananchi na mali zao.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img