Na Mwandishi Wetu
Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk. Tulia Ackson, amemhakikishia ushirikiano Katibu Mkuu wa Jukwaa la Mabunge ya Nchi Wanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (FP-ICGLR), Dk. Deo Mwapinga katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.
Dk, Tulia ameyasema hayo leo Mei 8, 2025 wakati alipomkaribisha kufanya mazungumzo na Dk. Deo Mwapinga, ofisini kwake Bungeni, Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Tulia amempongeza Dk. Mwapinga kwa kuchaguliwa katika wadhifa huo muhimu wa kuliongoza Jukwaa hilo na kusisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kushirikiana na taasisi za kikanda kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo endelevu.

Dk. Mwapinga alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa FP-ICGLR Aprili 25, 2025 katika kikao cha juu cha Maspika wa Mabunge ambayo ni Wanachana wa Jukwaa hilo kilichofanyika Luanda, Angola.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jukwaa hilo ataongoza taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu , ikiwa ni nafasi inayoweza kurejewa.