Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Pato la Taifa (GDP) ni kiashirio muhimu kinachopima thamani ya jumla ya bidhaa na huduma zinazozalishwa katika taifa kwa kipindi cha mwaka mmoja, hivyo kuonesha ukubwa na nguvu ya uchumi wa nchi.
Katika makadirio ya hivi karibuni ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) yaliyotolewa Aprili 2025, Tanzania imeendelea kuimarika na kujidhihirisha kama moja ya mataifa yanayoimarika kwa kasi kiuchumi barani Afrika. Ukuaji huu unatokana na uchumi wake mseto unaojumuisha sekta za kilimo, madini, miundombinu, na teknolojia inayokua kwa kasi. Eneo lake la kimkakati katika pwani ya Afrika Mashariki pamoja na mazingira ya kisiasa yaliyo tulivu vinaifanya Tanzania kuwa kivutio kikubwa cha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Mbali na Tanzania, mataifa mengine yaliyotajwa katika nafasi za juu za uchumi mkubwa barani Afrika ni pamoja na:
- Afrika Kusini, ikiongoza kwa Pato la Taifa la dola bilioni 410.34, ikiendeleza nafasi yake kama nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani.
- Misri, ikiwa nafasi ya pili kwa GDP ya dola bilioni 347.34, ikiinua uchumi wake kupitia sekta za kilimo, mafuta, gesi na utalii.
- Algeria na Nigeria zinashikilia nafasi ya tatu na nne mtawalia, zikichangiwa na rasilimali za mafuta, gesi na sekta ya huduma zinazokua.
Katika Afrika Mashariki, Kenya imeongoza ukanda huu kwa GDP ya dola bilioni 131.67, ikipiku Ethiopia ambayo imekadiria kuwa na pato la dola bilioni 117.46. Kenya imefanikiwa kutokana na soko lake linalochangamka, sekta ya fedha na utulivu wa kisiasa.
Ghana pia imepiga hatua kubwa, ikitumia fursa ya kuwa na akiba kubwa ya dhahabu, cocoa, pamoja na maendeleo katika sekta ya mafuta na gesi.
Makadirio ya IMF yanaonesha kuwa licha ya mataifa kama Afrika Kusini na Misri kuendelea kutawala uchumi wa bara, mwelekeo wa ukuaji wa mataifa kama Tanzania, Kenya, na Ghana unaashiria mageuzi makubwa ya kiuchumi Afrika kuelekea mwaka 2030.
NO | NCHI | PATO (DOLA BILIONI) |
1 | Afrika Kusini | 410.34 |
2 | Misri | 347.34 |
3 | Algeria | 268.89 |
4 | Nigeria | 188.27 |
5 | Morocco | 165.84 |
6 | Kenya | 131.67 |
7 | Ethiopia | 117.46 |
8 | Angola | 113.34 |
9 | Ivory Coast | 94.48 |
10 | Ghana | 88.33 |
11 | Tanzania | 85.98 |