Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Mustapher Siyani, amepongeza ushirikiano unaoendelea baina ya Mahakama na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), akisema ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hizo mbili za serikali.

Dk. Siyani alitoa pongezi hizo alipokuwa akifungua mafunzo maalum kwa Watendaji wa Mahakama Kanda ya Kati, yaliyobeba kauli mbiu: “Nafasi ya Teknolojia na Akili Bandia Mahali pa Kazi (Fursa na Mapinduzi)”, yaliyoandaliwa na OSHA kwa kushirikiana na Mahakama Kuu – Divisheni ya Kazi, na kufanyika katika Ukumbi wa OSHA jijini Dodoma kuanzia Aprili 23 hadi 24, 2025.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na zaidi ya washiriki 100 wakiwemo Majaji Wafawidhi, Majaji, Wasajili, Manaibu Wasajili, Mahakimu, Watendaji wa Mahakama, na Wasaidizi wa Majaji.
Katika hotuba yake, Jaji Kiongozi alisema:
“Niwashukuru OSHA kwa kuendelea kuwezesha mafunzo haya kwa watumishi wa Mahakama. Kwa kumbukumbu zangu, mwezi Desemba mwaka jana tulikutana hapa hapa kwa mafunzo kama haya. Mwendelezo huu ni jambo la kuigwa na Taasisi nyingine,” amesema Dk. Siyani.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo, akibainisha kuwa mada zilizotolewa—ikiwemo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na matumizi ya teknolojia ya akili bandia—zina umuhimu mkubwa kwa watumishi wa Mahakama ambao ni wadau muhimu katika utoaji wa haki.
Aliongeza kuwa dunia inaelekea kwenye matumizi makubwa ya teknolojia, hivyo Tanzania haiwezi kujitenga na mwelekeo huo, hasa katika sekta ya Mahakama.
Akihitimisha hotuba yake, Dk. Siyani aliwashukuru washiriki kwa kujitolea muda wao kuhudhuria mafunzo, huku akitarajia kuwa maarifa waliyoyapata yataongeza ufanisi na tija katika utendaji kazi wao.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu – Divisheni ya Kazi, Dk. Yose Mlyambina, alisema Mahakama Kuu inaendelea kujivunia uhusiano mzuri uliopo baina yao na OSHA, uhusiano ambao umekuwa ukizidi kuimarika na kuwavutia wadau mbalimbali wa sekta ya haki kazi.
Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alisema mafunzo hayo yana faida maradufu kwa watumishi wa Mahakama kwani siyo tu yanawajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya kama wafanyakazi, bali pia yanawasaidia katika kushughulikia kesi zinazohusu masuala hayo.

Mafunzo haya ni mwendelezo wa mafunzo yaliyotolewa awali Desemba 16-17, 2024, yaliyohusu Usalama, Afya, Haki na Wajibu kwa Watu Wenye Ulemavu.