15.8 C
New York

Baraza la tiba asili na tiba mbadala latakiwa kutumia tafiti kuleta mchango sekta ya afya

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amelitaka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini kujikita katika tafiti za dawa za tiba asili na mbadala na kuzitumia tafiti hizo ili zilete mchango kwenye sekta ya afya.

Waziri  huyo ameyasema hayo wakati akizindua Baraza jipya la Tiba Asili na Tiba Mbadala leo Aprili 25, 2025 jijini Dodoma.

Amesema ufanyaji wa tafiti hizo na kutoa ushahidi wa kisayansi utasaidia Tanzania kujipambanua ili kutoa wa huduma za tiba asili na tiba mbadala ndani na nje ya nchi.

Aidha, amelitaka baraza hilo kusimamia majukumu yake kwa weledi na kudhibiti wanaotaka kukiuka sheria na taratibu za tiba asili na tiba mbadala kwa kuwachukulia hatua stahiki.

Amelielekeza baraza hilo kuhakikisha linauhisha daftari la wataalam wa tiba asili na tiba mbadala waliosajiliwa na kufanya ukaguzi shirikishi na kuelekezana juu ya umuhimu wa kuwa na leseni hai.

“Kuna uwepo wa dawa nyingi sokoni kuliko dawa zilizosajiliwa hivyo ni vyema kuhamasisha dawa hizi zote zisajiliwe ili kugundua kiwango cha dawa tulizonazo, tukiifanya hii kazi vizuri tuna uwezo wa kuokoa wananchi wengi,” ameeleza.

 Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Grace Magembe ameeleza kuwa baraza hilo limekuwa na mafanikio ya kuongeza watoa huduma na kufikia 59,278, vituo 293 na dawa za asili zilizosajiliwa zimeongezeka na kufikia 157.

“Watanzania waliowengi kabla ya kwenda kutafuta matibabu hospitali wanaanza na matibabu ya tiba asili kwa hivyo hii ni tiba ambayo ipo ndani ya utoaji wa huduma za afya ndani ya nchi yetu,” amesema Dk. Grace.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala Prof. Japhet Otieno amesema amepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mhagama na kuahidi kuyafanyia kazi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img