1.6 C
New York

Mabadiliko ya tabianchi yanavyotishia ustawi wa ndoto za watoto Tanzania

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto inayoendelea kuathiri maisha ya watu duniani kote, hasa watoto ambao ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini zaidi.

Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine yanayoendelea, inakabiliwa na athari mbaya za tabianchi, ikiwemo ukame, mafuriko, na maporomoko ya ardhi.

Tukio la maporomoko ya ardhi, katika Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara, Desemba 2023, ni moja ya kilelezo cha athari hizo ambapo liliibua mjadala kuhusu athari hizi na jinsi zinavyoathiri watoto nchini.

Mvua kubwa zilizosababisha maporomoko hayo ziliharibu makazi, shule, na miundombinu mingine. Watoto 36 walipoteza maisha kati yao wakiume wakiwa 16 na wa kike 20. Kando na hao waliopoteza maisha watoto wengine 62 walijeruhiwa ambapo kati yao wakiume walikuwa 28 na wa kike 34.

Athari za maporomoko hayo zitaendelea kuwa moja ya kielelezo kibaya cha mabadiliko ya tabianchi kwa watoto, kwani wengine 56 waliathirika ikiwamo kisaikolojia.

Watoto kama sehemu ya wahanga wakuu walishuhudia namna ambavyo walibaki bila makazi kwani athari hizo zilisababisha nyumba 1,150 kusombwa na maji huku miundombinu kadhaa iliyokuwa ikiwezesha watoto kwenda na kurejea shule ikiharibiwa vibaya hatua iliyosababisha shule tatu kufungwa na hivyo kuacha masomo yao shakani kwa muda usiojulikana.

Watoto wamekuwa miongoni mwa makundi yasiyoweza kujinusuru kwa haraka, wanakumbwa na hatari kubwa katika majanga kama haya na hatimaye kuacha majonzi kwa familia.

Sambamba na haya tunaona ni kwa namna gani mabadiliko ya tabianchi yanavyotishia ndoto za watoto wengi kutimia.

Naman Joshua (siyo jina lake halisi) mwanafunzi wa darasa la sita, ni miongoni mwa watoto waliothirika sana na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa Desemba 2023. Tukio hilo, lililoharibu makazi na miundombinu muhimu, lilibadilisha maisha ya Naman kwa njia nyingi, kuanzia elimu, afya, hadi kisaikolojia yake.

Anasema tukio hilo litadumu maishani mwake daima kwani familia yao ilipoteza makazi kutokana na maporomoko hayo, na waliishi katika makazi ya muda kabla ya serikali kuwajengea nyumba mpya zilizozinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hivi karibuni.

“Nilikuwa napenda sana kwenda shule kila siku, lakini sasa nashindwa kujifunza vizuri kwa sababu ya mazingira magumu, kwani shule yetu ni kati ya zilizoharibiwa vibaya, hivyo inakuwa changamoto, ukiacha hilo hata nyumba yetu imeondoka na hatuna sehemu ya kuishi tena,” anasema Naman anaye soma darasa la sita katika moja ya shule zilizoko wilayani humo.

Shule nyingi zimeharibiwa na majanga yanayohusiana na tabianchi. Katika Hanang, shule kadhaa ziliharibiwa, hali iliyosababisha watoto kuacha masomo au kuhama makazi yao.

Kukatizwa kwa elimu si tu kunavunja ndoto za watoto bali pia kunadhoofisha juhudi za kitaifa za maendeleo.

Serikali inapaswa kuwekeza katika miundombinu imara ya shule na makazi inayoweza kuhimili majanga ya asili. Pia, elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi inapaswa kutolewa shuleni na katika jamii.

Watoto na familia wanapaswa kufundishwa jinsi ya kutambua ishara za hatari na kuchukua hatua za kujikinga.

Sambamba na haya, Tanzania inapaswa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kupata teknolojia na rasilimali za kupunguza athari za tabianchi. Juhudi za kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa zinapaswa kuimarishwa.

Tukio la maporomoko ya ardhi Hanang linatoa tahadhari kuhusu hatari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto nchini. Majanga kama haya yanaharibu mazingira, kuathiri afya, elimu, na mustakabali wa watoto.

Athari hizo ndizo zinalisukuma Shirika la WeWorld kusaidia watoto kushiriki katika miradi ya mazingira kupitia programu zake za Pamoja Tunaboresha Elimu, KITE, na MAMMIE.

Miongoni mwa wanufaika wa miradi hiyo ni pamoja na Shule ya Msingi Kawe, Dar es Salaam, ambako Klabu ya “Wakulima Chipukizi” imeanzishwa.

Watoto wanajifunza kulima mboga kama mchicha na nyanya, pamoja na kupanda miti 60, na wamedhamiria kuongeza miti mingine 50 ya matunda. Miradi hii imeonyesha manufaa makubwa, ikiwemo kuboresha lishe ya watoto, kupunguza magonjwa yanayohusiana na tabianchi, na kuhifadhi mazingira ya shule.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img