2.6 C
New York

Wataalamu waonywa matumizi ya madini ya zebaki kuziba meno

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Wataalamu wa afya ya kinywa na meno kutoka nchi za Afrika Mashariki wameaswa kuacha matumizi ya dawa za kuziba meno zenye madini ya zebaki, maarufu kama dental amalgam, kutokana na athari zake kwa afya ya binadamu na mazingira.

Wito huo umetolewa katika maadhimisho ya miaka 10 ya Afrika ya kuziba meno bila kutumia dawa zenye zebaki, yaliyoanzishwa na mashirika ya kiraia 40 kutoka nchi 18, zikiwemo 13 za Afrika Mashariki. Maadhimisho hayo yanafanyika kuanzia Desemba 9 hadi 14, yakiongozwa na kauli mbiu: “Nchi Wanachama wa Mkataba wa Minamata wa Zebaki Watekeleze Matakwa ya Mkataba Huo.”

Katibu Mtendaji wa AGENDA for Environment and Responsible Development (AGENDA), Dorah Swai, alisema maadhimisho hayo pia yanatoa nafasi kwa wadau kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa plastiki.

Mkataba wa Minamata, uliopitishwa mwaka 2013 nchini Japan na kuridhiwa na Tanzania mwaka 2019, unalenga kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya athari za zebaki. Mkataba huo unazitaka nchi wanachama kusitisha matumizi ya dental amalgam kwa watoto chini ya miaka 15, wanawake wajawazito, na wanawake wanaonyonyesha, kutokana na madhara yake kwa ukuaji wa ubongo wa mtoto na mazingira.

Silvani Mng’anya, Afisa Programu Mkuu wa AGENDA, alisema zebaki inaweza kuingia mwilini kupitia mama mjamzito au maziwa ya mama, na kusababisha athari kama kupunguza uwezo wa kufikiri wa mtoto. Pia, zebaki hudumu kwenye mazingira kwa muda mrefu na kuingia kwenye mlolongo wa chakula kupitia samaki.

Tanzania imekuwa mstari wa mbele kwa kusitisha matumizi ya dental amalgam kwa watu wa rika zote tangu mwaka 2022. Bernard Kihiyo, Mkurugenzi wa Tanzania Consumer Advocacy and Research (TCAR), alisema, “Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinapaswa kuchukua hatua sawa ili kulinda afya ya kizazi kijacho na mazingira yetu.”

Kimataifa, nchi 151 zimekwisha kuridhia Mkataba wa Minamata, zikionyesha juhudi za pamoja za kukabiliana na changamoto ya zebaki duniani. Hii ni hatua muhimu kwa mustakabali wa afya na mazingira, huku wito ukiendelea kwa nchi wanachama kuharakisha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img