1.6 C
New York

Serikali yatenga Bilioni 45.1 kudhibiti migongano ya binadamu na wanyamapori 

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Serikali imetenga Shilingi bilioni 45.1 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kudhibiti migongano baina ya binadamu na wanyamapori nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kudumisha usalama kwa jamii zinazopakana na maeneo ya uhifadhi. 

Akizungumza hivi karibuni, jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Wanyamapori, Anthonia Raphael, alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali kuhakikisha changamoto za migongano hii zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu. 

“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jumla ya shilingi bilioni 45.1 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mikakati na mipango iliyowekwa kudhibiti migongano hii,” alisema Anthonia, wakati wa majadiliano yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ). 

Afisa Mkuu wa Wanyamapori, Anthonia Raphael, akizungumza wakati wa majadiliano hayo.

Alifafanua kuwa hadi Oktoba 2024, kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kimelipwa kwa wananchi 4,142 kutoka wilaya 14 zikiwemo Tunduru na Namtumbo kama fidia ya madhara yaliyosababishwa na wanyamapori. 

“Wizara inashirikiana na wadau mbalimbali kupitia Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori (2020-2024), ili kukabiliana na changamoto mpya zinazoibuka,” aliongeza. 

Fidia kwa waathirika 

Katika mwaka wa fedha 2023/2024, mpango wa kifuta jasho na kifuta machozi uliwezesha malipo ya shilingi bilioni 3.1 kwa wananchi 14,959 waliopata madhara, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazao na majeraha. Fidia hiyo ilitolewa kwa halmashauri 53 za wilaya, zikiwemo Liwale, Nachingwea, Tandahimba, Morogoro Vijijini na Mvomero. 

Mikakati mipya 

Wizara pia imepanga kuimarisha utekelezaji wa mkakati wa kuhifadhi shoroba za wanyamapori (2022-2026) na kuboresha mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi. 

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dk. Fortunata Msofe(aliyesimama) akiwasilisha mada wakati wa majadiliano hayao.

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dk. Fortunata Msofe, alisema serikali inalenga kushirikiana na jamii katika kudhibiti migongano hiyo kwa kutoa elimu kuhusu mbinu za kupunguza athari na kuelekeza faida za uhifadhi. 

“Pia tunatoa elimu ya mbinu za uhimilivu ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao huku wakidhibiti migongano na wanyamapori,” alisema Dk. Msofe. 

Hali ilivyo 

Takwimu za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) zinaonyesha ongezeko kubwa la matukio ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu. Kwa mfano, mwaka 2022/2023 matukio yaliongezeka hadi kufikia 2,817 kutoka matukio 833 mwaka 2016/2017. 

Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru, aliwahimiza waandishi wa habari kutumia nafasi yao kuhamasisha mabadiliko kwa manufaa ya jamii na mazingira. “Wanahabari wana nafasi kubwa mno katika kuchochea mabadiliko na kuwahamasisha wadau kuchukua hatua,” alisema. 

Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru.

Migongano baina ya binadamu na wanyamapori siyo tu inasababisha athari kwa maisha ya watu bali pia inadhoofisha juhudi za uhifadhi wa maliasili, hatua inayolazimu jitihada za pamoja kuipatia suluhisho.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img