9.5 C
New York

Bajeti Kuu ya Serikali kuwezesha nishati safi ya kupikia

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amefungua Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika unaofanyika katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa Mei 14, 2024.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Wenyeviti Wenza, Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre wa pili kutoka kulia, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Akinumwi Adesina wa kwanza kulia pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (IEA), Dk. Fatih Birol wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika uliofanyika katika Makao Makuu ya UNESCO Jijini Paris nchini Ufaransa Mei 14, 2024.

Katika hotuba yake ya ufunguzi Rais Samia amesisitiza umuhimu wa nishati safi kwa Nchi za Afrika ili kudhibiti madhara yatokanayo na kadhia za kukosa nishati hiyo kama vile, uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa, unyanyasaji wa kijinsia na vifo kwa wanawake na watoto.

Aidha, amesema Tanzania imelipa kipaumbele suala la nishati safi ya kupikia ambapo imeongeza bajeti ya Serikali ili kuwezesha upatikanaji wa nishati safi kwa urahisi, gharama nafuu pamoja na uwekezaji katika teknolojia.

Vilevile itasimamia utekelezaji wa sera, mikakati na miongozo ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ustawi wa jamii.

“Serikali imelipa umuhimu suala la nishati safi ya kupikia ambapo katika kuyafikia malengo hayo bajeti kuu ya Serikali imeweka kipaumbele katika kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo sambamba na kuwainua wanawake,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongoza mkutano huo akiwa pamoja na wenyeviti wenza: Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Støre, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati, Dk. Fatih Birol na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Akinwumi Adesina.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo una lengo la kufanya matumizi ya nishati safi ya kupikia kuwa suala la kipaumbele katika agenda ya kimataifa; kuainisha hatua madhubuti za kisera zitakazoharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia; na kutoa fursa kwa washiriki kutoa ahadi za kifedha, sera, na ubia ili kufikia azma ya kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Kupitia mkutano huo, jumla ya ahadi za kiasi cha Dola bilioni 2.2 bilioni zimekusanywa ili kusaidia katika usimamizi wa sera na miongozo mbalimbali na uwekaji wa miundombinu itakayowezesha upatikanaji wa nishati safi.

Ikumbukwe, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia Mei 8, 2024 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuyafikia malengo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img