Na Mwandishi Wetu, Gazetini – Arusha
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) pamoja na Wakala wa Usalama na Afya mahalipa kazi (OSHA) wametoa wito kwa kampuni nyingine za madini kuiga mbinu na miongozi inayotumiwa na Geita Gold Mining Limited (GGML) katika kuzingatia kanuni za afya na usalama mahali pa kazi.
Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa taasisi hizo waliotembelea banda la GGML katika maonesho ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA) yanayoendelea kwenye viwanja vya General jijini Arusha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya OSHA, Dk. Adelhelm Meru alisema kinachooneshwa na GGML katika maonesho hayo kimedhihirisha ni kwa namna gani kampuni hiyo inaungana na serikali katika kudhibiti majanga migodini.
Alisema teknolojia hizo zinazohusu vifaa mbalimbali ikiwamo kifaa maalum cha ProLaser Speed Gun ni mifano michache ambayo inaweza kuigwa na kampuni nyingine katika kulinda afya na uhai wa wafanyakazi wao ajali zinazotokana na mwendo kasi
Naye Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhoka alieleza kufurahishwa na teknolojia zinazotumiwa na GGML katika utekelezaji wa majukumu yake kwani zimekuwa chanzo cha wafanyakazi kufanya kazi katika mazingira rafiki na salama kwao na kwa familia zao.
“Ninatamani viongozi wakubwa wanaoendelea kutembelea maonesho haya wapite katika banda ya GGML wajionee wenyewe teknolojia hizi tunazozingumzia,” alisema.
Alisema teknolojia hizo ni za kipekee na zinalenga kutekeleza kwa vitendo tunu ya kampuni hiyo ambayo ni afya na usalama mahali pa kazi.
Shughuli za Mgodi wa Dhahabu wa Geita zinahusisha uendesha wa mitambo mikubwa, malori na magari.
Kifaa hicho cha ProLaser Speed Gun kilichokuwa kinatumika kuelimisha washiriki wa maonesho hayo, husaidia kudhibiti mwendo kasi wa magari na kupunguza ajali.
Mratibu wa Usalama, Walter Marealle alifafanua kwa kutumia kifaa hicho GGML huweza kufutilia mwendo kasi wa magari ndani ya kampuni na kuwawajibisha madereva ambao hawazingatii taratibu.
Alisema kifaa hicho kinasaidia kupunguza ajali, majeraha na vifo hivyo kuendelea kuwaweka wafanyakazi katika hali ya usalama.
“Data zilizokusanywa na ProLaser Speed Gun pia inasaidia GGML kutambua maeneo ambayo mwendokasi ni tatizo na kuandaa hatua zinazolstahili kushughulikia suala hilo.
“ProLaser Speed Gun ni sehemu moja tu ya hatua zinazochukuliwa na GGML kuzingatia afya na usalama mahali pa kazi. GGML pia inatumia alama za wazi na alama za barabarani kumkumbusha kila mtu juu ya ukomo vya mwendo kasi na kutoa mafunzo ya udereva ili kuwapa waendeshaji wake maarifa na ujuzi muhimu wa kufanya kazi kwa usalama,” alisema.