7.1 C
New York

Tuzo za EJAT 2023 zazinduliwa Dodoma

Published:

*Vipengele vya Gesi, Teknolojia na Sensa vyaondolewa sababu ya ufadhili

Na Faraja Masinde, Gazetini

Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za Umahiri za Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT), imezindua rasmi Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2023.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT, Kajubi Mukajanga(kulia) akizungumza wakati wa kutangaza Tuzo hizo, Kushoto ni Programu Ofisa kutoka Baraza la Habari Tanzania(MCT), Paul Mallimbo.

Akizungumza leo Jumatano Novemba 15,2023 wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT, Kajubi Mukajanga amesema tuzo za mwaka huu zitahusisha makundi mawili mapya na zitakuwa na jumla ya makundi 18 ya kushindaniwa ikilinganishwa na makundi 20 yaliyoshindaniwa kwenye EJAT 2022.

“Mwaka huu kuna makundi mawili mapya ambayo ni Habari za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Habari za Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto ambayo yameongezwa ili kushajiisha ubora wa uandishi habari katika maeneo hayo.

“Pamoja na nyongeza ya makundi hayo, makundi ya Habari za Gesi, Mafuta na Uchimbaji Madini, Habari za Sayansi na Teknolojia; na Habari za Sensa yameondolewa katika orodha ya makundi yatakayoshindaniwa katika Tuzo hizo.

“Hii ni kutokana na mwitikio mdogo wa uwasilishaji kazi kutoka kwa waandishi wa habari na kukosekana kwa ufadhili wa uhakika,” amesema Mukajanga.

Mukajanga amesema kazi zitakazoshindanishwa katika kuwania tuzo hizo za 15, ni zile zilizochapishwa au kutangazwa kati ya Januari na Desemba 31, 2023 huku akiwataka wale wenye kazi ambazo makundi yake yameondolewa kutumia makundi mengine.

“Waandishi wenye habari za maeneo haya ambayo wanaona kazi zao ni nzuri wanahimizwa kuziwasilisha kupitia makundi mengine kama Uchumi, Bishara na Fedha au Kundi la Wazi kutegemea na wakavyoshauriana na wahariri,” amesema Mukajanga.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img