Na Faraja Masinde, Gazetini
Tanzania, kama zilivyo nchi zingine za Afrika, imeendelea kugubikwa na changamoto ya uhaba wa ajira, hasa kwa kundi la vijana na hiyo inatajwa kuwa moja ya sababu zinazowasukuma kwenda ughaibuni.
Machi 3, 2023, Serikali kupitia Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu, Patrobas Katambi, ilieleza kuwa vijana milioni 1.7 wenye uwezo wa kufanya kazi hawana ajira. Kiwango hicho ni asilimia 12.2 ya vijana wenye umri wa miaka 15-35.
Hata hivyo, haiishii kwa ‘vijana wa vijiweni’ tu, bali hata wengine wenye kazi zinazowapa kipato kizuri, bado wanaamini kuwa wangekuwa mbali zaidi endapo wangekuwa nje ya nchi.
Leo, hii, vijana, wakiwamo wahitimu wa vyuo vikuu, ambao ungetarajia kuona wakiwa chanzo cha mabadiliko chanya kwa jamii wanazotoka, wamemezwa na dhana kwamba ni rahisi kufanikiwa kimaisha ukiwa nje ya nchi.
Kwa takwimu zilizopo, vijana wengi wa Tanzania, kama ilivyo kwa Kenya, Uganda, Nigeria na Zimbabwe, kimbilio lao ni Afrika Kusini, ingawa matamanio makubwa (lakini yasiyowezekana kirahisi) ni kwenda barani Ulaya.
Katika hilo, wengi wanaeleza kushawishiwa na tamaa, hasa baada ya kuona wenzao waliokwenda nje ya nchi wakirudi wakiwa wamepiga hatua kimaisha.
Magdalena Mushi, msichana mwenye umri wa miaka 25 mkazi wa Dar es Salaam, ni miongoni mwa wanaosukumwa na tamaa ya kwenda ughaibuni, akiwa hana shaka kuwa huko ‘kutoboa’ ni rahisi kuliko hapa Tanzania.
Katika mahojiano yake na gazetini Magdalena anasema: “Unajua kaka yangu, nimekuwa nikiona vijana wengi wakienda nje ya nchi na kurudi na hela nyingi, ambapo wengine wamekuwa wakiishia kufanya anasa,” anasema Magdalena.
“Sijakata tamaa. Tayari nina hati ya kusafiria ila nimekuwa nikipata changamoto ya visa,” anasema Magdalena aliyehitimu kidato cha nne na kupata daraja la nne katika mtihani wake wa mwisho.
“Malengo yangu ni kwenda nje, hasa Ujerumani. Nitahakikisha napata fedha nyingi, aidha kwa kufanya kazi zaidi au mbinu nyingine yoyote ambayo ni halali. Naamini ipo siku nitafanikiwa kwani maisha ya hapa Tanzania ni magumu sana,” anasema Magdalena.
Kwa upande wake, Khamis Jongo (27), kijana mwingine wa Tanzania anayeishi Pretoria, Afrika Kusini, anasema aliondoka Tanzania mwaka 2019 baada ya kuvutiwa na mafanikio makubwa ya mjomba wake.
“Si kwamba nilikuwa na maisha magumu Tanzania. Hapana. Nilikuwa fundi magari mzuri tu. Niseme tu, mjomba wangu aliyekuwa akiishi Afrika Kusini ndiye aliyeniingizia tamaa ya kuja huku.
“Nakumbuka aliishi Afrika Kusini kwa miaka mitano tu lakini aliporudi Tanzania alikuwa amebadilika sana. Alikuwa na pesa, magari na akanunua nyumba za kutosha Tanzania.
“Hii ilinifanya nipate uchungu, ikizingatiwa kuwa nilikuwa nikiingiza kipato cha kawaida. Nikaona kazi yangu ya gereji itanichelewesha sana kufika alikofika mjomba,” anasema Jongo.
Dhana ya maisha bora nje ya nchi
Nuru Sanga, binti raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 33, aliwahi kuishi na kufanya kazi Ujerumani kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2015.
Akihojiwa na gazetini Nuru ambaye ni mjasiriamali wa biashara ya nguo za kiume Kariakoo jijini Dar es Salaam, anasema alipata fursa ya kwenda kujitolea katika Shirika la kusaidia watu wenye ulemavu nchini humo.
“Kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuwahudumia watu hao, ikiwamo kupika, kuwafulia nguo, kutandika kitanda, kuwatembeza, kuwafanyia usafi kwenye vyumba vyao, kuwaogesha na kuwalisha wale wasioweza kula peke yao,” anasema.
Je, ni kweli njia sahihi kwa vijana kupata maisha mazuri ni kwenda nje ya nchi? Nuru anajibu hilo akisema: “Si kweli kwamba mafanikio yanapatikana nje ya nchi.
“Binafsi siamini hivyo. Ila ninachofahamu ni kwamba wenzetu wanatumia muda mwingi kufanya kazi, ukilinganisha na hapa kwetu Tanzania.
Kwa upande wake, Nuru anaamini vijana wa Tanzania wanaweza kutimiza ndoto zao za kuishi maisha mazuri bila kwenda nje ya nchi.
“Hakuna tofauti ya maisha, hata ukiwa hapa nyumbani unaweza kufanikisha malengo yako. Kikubwa ni kuwa na mipango kwa kila unachokipata,” anasema Nuru.
Kwa upande mwingine, mtazamo wake hautofautiani na alionao mkufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Lugha ya Kijerumani cha Goethe cha jijini Dar es Salaam, Gaspa Buya, ambaye anaamini maisha ya Tanzania ni rahisi kuliko huko wanakokimbilia vijana.
Buya haoni haja ya vijana wa Tanzania kwenda nje kwani hata hapa nchini wanaweza kufanya kazi na kufanikiwa.
“Fedha anayolipwa kijana anayefanya kazi Ulaya aliyetoka Tanzania haina tofauti kubwa na anayoweza kupata hapa. Tena hapa kunakuwa na faida zaidi kwani maisha ya hapa ni rahisi, ukilinganisha na nchi kama Ujerumani.
“Ni muhimu vijana wakapambana tu hapa ili kufanikisha malengo yao ya kimaisha kuliko kudhani Ulaya kuna mambo mepesi au fedha za haraka,” anasema Buya.
Naye Raymond Mdende, mkufunzi mwingine wa Taasisi hiyo, anasema vijana wanakosea kujidanganya kuwa nje ya nchi kuna maisha rahisi.
“… Kama hufanyi kazi, hakuna sehemu ambayo unaweza kuona maisha ni rahisi, hata ukienda Marekani mambo ni yale yale.
“Ninachoweza kusema ni kwamba vijana wapambane, wafanye kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo yao na siyo kutegemea kwamba wataenda kupata urahisi wa maisha nje ya nchi,” anasema Mdende.
Hoja ya Mdende inaungwa mkono na simulizi ya Ambakyise Ruben, kijana anayejuta kwa muda mwingi alioupoteza nchini Ujerumani.
Ambakyise (30), anasema alifanya kazi ya kujitolea wa kipindi cha mwaka mmoja katika Shirika la Udiakonia la nchini humo.
“Kwa muda nilioupoteza, ni vema ningeutumia kujishughulisha na kilimo hapa nchini. Nilipokuwa kule, nilikuwa na malengo makubwa.
“Nilitaka nikirudi Tanzania ninunue ng’ombe wa kufuga, nijenge nyumba na nifungue duka kubwa la pembejeo za kilimo na mifugo.
“Hata hivyo, baada ya kufika Dar es Salaam na kubadilisha zile fedha (euro), nikaona ni tofauti na nilivyofikiri nikiwa kule. Nilijikuta nikiwa na milioni tano tu,” anasema Ambakyise na kuongeza:
“Nilichoweza kufanikisha ni kuweka umeme katika nyumba ya mama yangu, kununua ng’ombe mmoja na fedha nyingine kidogo iliyokuwa imebaki nikafungua duka dogo la pembejeo, ambalo nalo ‘limeshakufa’ kutona na mtaji kuwa mdogo.
“Ni tofauti kabisa na matarajio yangu, ambapo niliamini ningepata pesa nyingi Ulaya. Siamini kuwa maisha mazuri yako nje ya nchi. Ni bora vijana wakapambana hapa hapa kwa kujiwekea malengo.
Changamoto nje ya nchi
Jongo, ambaye awali aliiambia gazetini kuwa mjomba wake ndiye sababu ya yeye kwenda Afrika Kusini, anasema alipofika Afrika Kusini alibaini kuwa hakuna maisha rahisi, tofauti na alivyofikiri.
“Unajua wakati mjomba anarudi Tanzania kwa mapumziko, sikuwa najua kazi aliyokuwa anafanya. Hata yeye hakuwa akisema. Nilipokuja huku, ndipo nilipobaini kuwa anajihusisha na biashara za dawa za kulevya.
“Kwa kuwa sikutaka kuingia huko, nikawa natafuta kwa njia halali, ikiwamo kufanya biashara ndogondogo huko mitaani. Nikaiona tofauti kubwa ya kile nilichotarajia na hiki nilichokikuta Afrika Kusini,” anasema Jongo.
Ruben Dilunga (23), mkazi wa Durban, Afrika Kusini, anakiri kupitia nyakati ngumu katika maisha yake ya utafutaji nchini humo.
“Ughaibuni si sehemu ya kuja kwa kukurupuka,” anaonya Ruben, akiongeza kuwa ubaguzi kwa wageni ni sehemu ya maisha ya raia wa Afrika Kusini.
“Ni tofauti na nyumbani, ambako unatafuta ukiwa na amani. Huku ubaguzi ni mkubwa. Ni ngumu sana raia wa kigeni kupata kazi yenye kipato kizuri. Ndiyo maana, huku wageni wengi huishi kuwa wahalifu,” anasema Ruben.
Vilevile, Hassan Mwela (32), kijana mwingine wa Tanzania mwenye makazi yake Dubai, Falme za Kiarabu, ni kama anaunga mkono alichokisema Ruben, akisisitiza kuwa vijana wengi wanaoondoka nchini wanakabiliwa na mazingira magumu huko ughaibuni.
“Wengi tunatoka nyumbani (Tanzania) bila mipango. Kwa Afrika Kusini, ambako niliishi kwa miaka mitatu, vijana wenzangu wengi niliotoka nao Tanzania walikuwa wanalala mitaani au ufukweni.
“Mbaya zaidi, wengi waliondoka Tanzania kwa njia zisizo halali, hivyo maisha yao ya Afrika Kusini ni ya kuwakimbia polisi tu. Wanatumia muda mwingi kujificha kuliko kuingia kwenye mzunguko wa kuingiza kipato,” anasema.
Wakati huo huo, Nuru anayefurahia kukua kwa biashara yake ya nguo za kiume Dar es Salaam, anagusia uwepo wa ubaguzi katika malipo ya wafanyakazi wa kigeni Ujerumani alikokuwa akihudumia watu wenye ulemavu.
“Kinachoumiza zaidi ni kwamba wakati wewe unalipwa euro 400, mwenzako unayefanya naye kazi, ambaye ni Mjerumani analipwa euro 900 hadi 1,000.
“Mbaya zaidi, unakuta kazi uliyofanya ni kubwa na nzito tofauti na malipo. Ni kama unakuwa unafanyia shida tu, huku ukijua malengo yako ni yapi,” anasema Nuru.
“… Kuna wakati nilikuwa nakula mlo mmoja na kuna siku unakula chakula wanachobakiza wale unaowafanyia kazi ili tu uokoe fedha kiduchu unayolipwa,” anasema Nuru.
Katika hatua nyingine, Mwanahamis Hussein (52), ni mzazi wa watoto watatu mkazi wa Dar es Salaam. Mtazamo wake umejikita katika changamoto ya maadili, hasa kwa vijana wanaokuwa nje ya nchi kwa madai ya kutafuta maisha.
“Siwezi kuruhusu watoto wangu kwenda nje ya nchi. Vijana wetu wanapokuwa huko, wanaiga maadili yasiyofaa na yenye chukizo mbele ya Mungu.
“Huenda akafanikiwa kupata fedha alizokwenda kuzitafuta lakini mazingira ya huko yakambadilisha na kuwa tofauti na yule aliyetoka hapa,” anasema.
Mdende anaitilia mkazo hoja hiyo, akiwataka vijana wa Tanzania wanaokwenda nje ya nchi kuzingatia na kulinda utamaduni wao.
“Wengi wamekuwa wakibadilika pindi wanapokwenda nje ya nchi kwa kudhani kuwa kuishi au kuvaa kama wazungu ndiyo kuwa wa kisasa, jambo ambalo siyo sahihi hata kidogo,” anasema.
Ni ‘dhambi’ kutafuta maisha nje?
Mwela anayeishi Falme za Kiarabu, anaiambia gazetini kuwa si vibaya kwa vijana kwenda kujaribu maisha katika mataifa mengine.
“Katika karne hii ya 21, dunia ni kijiji. Si dhambi kijana wa Tanzania kutoka na kwenda kutafuta maisha. Kwa sasa mipaka iliyobaki ni ya kijiografia tu, hakuna kizuizi cha mtu kutoka eneo lake na kwenda kokote duniani. Hii ni fursa na vijana tunapaswa kuitolea macho.
“Hata hivyo, kinachotakiwa ni kujitambua tu. Huku ni ugenini. Ukiwa huku, kijana unatakiwa kutambua kilichokupeleka. Kila unachokipata, kiwe ni kwa ajili ya malengo ya kuja kukiendeleza nyumbani (Tanzania). Kinyume cha hapo, kijana atapata pesa lakini zitaishia huku huku.
Felix Kapama (45), Mtanzania anayeishi Doha, Qatar, tangu alipoondoka Tanzania miaka sita iliyopita, anaiambia Gazetini kwa njia ya mtandao kuwa haoni tatizo kwa vijana wa Tanzania kwenda nje ya nchi, ikiwa tu wanakwenda kubadili mazingira na si kutegemea makubwa zaidi.
“Ushauri wangu kwa wanaotamani kwenda nje, wasitarajie mambo makubwa ila waende tu kwa nia ya kufurahia kubadilisha mazingira. Kuhusu mafanikio, wasiwe na matarajio makubwa kwa sababu hata mimi niliishi kwa kujibana sana ili kupata cha kurudi nacho,” anasema.