*Zaidi ya watoto 600 wamenufaika na mpango huu
*Baadhi ya wazazi waliona nimegeuza watoto wao kitega uchumi
Na Tulinagwe Malopa, Gazetini
“Ilikuwa ni baada ya kujikuta mzazi wa mtoto wa kiume aliyejulikana kwa jina la Erick, aliyekuwa mlemavu wa viungo na akili kabla hajafariki mwaka 2005”.
Ni kauli ya Josephine Bakita baada ya kupata manyanyaso ya kila aina kweye jamii ikiwemo kupewa majina yanayoendana na udhaifu wa mwanae ndipo alipoona umuhimu wa kuanzisha kampeni ya kutetea watoto wenye ulemavu hasa katika jamii anayoishi.
“Nilianza kampeni hii ya kutetea haki za watu wenye ulemavu, baada ya mwanangu Erick na mimi mama yake kunyan yasika kwenye jamii kwa kuzomewa zomewa na kupewa majina yanayoendana na ulemavu ambao alikua nao mwanangu,” Ndivyo mama Bakita alivyoeleza dhumuni la kuanzisha kituo cha Kumbukumbu kwa ajili ya mtoto wake ya kuimarisha Elimu na kutoa marekebisho kwa watu wenye ulemavu (Erick Memorial Foundation for Education and Rehabilitation for Disabled-EMFRED) katika mazungumzo na www.gazetini.co.tz
“Baada ya kuona hali hiyo, nikaitupia mgongoni na kuona kwamba hii ni hali inayowapata wazazi wengine wote wenye kupata watoto wenye ulemavu,” anasema Mama Bakita na kufafanua kuwa amekuwa akitoa huduma ya kutetea haki za watoto wenye ulemavu kwa muda wa miaka 18 ndani ya Manispaa ya Morogoro na vijiji jirani.
Baada ya kuhudumia Manispaa ya Morogoro kwa muda mrefu na kuona matokeo chanya, Mama Bakita aliamua kuhamia kuhudumia familia zilizopo vijijini maeneo ambayo hayafikiwi na mashirika mengine kirahisi.
“Nilivoona miaka yote 18 ni hamasisho kubwa limefanyika Manispaa na Makao Makuu yake yamekuwa Morogoro, taasisi hii tukaona kwamba izingatie familia zilizopo vijijini ndani ambako hazifikiwi na taasisi nyingine zozote zile.
“Nilivoona miaka yote 18 ni hamasisho kubwa limefanyika Manispaa na Makao Makuu yake yamekuwa Morogoro, taasisi hii tukaona kwamba izingatie familia zilizopo vijijini ndani ambako hazifikiwi na taasisi nyingine zozote zile.
“Hivyo, katika kusajili, makao makuu ya taasisi ya EMFRED tukayaweka Wilaya ya Mvomero, tarafa ya Mvomero, kata na kijiji cha Mvomero maeneo mengine tunayoyahudumia ni Wilaya ya Gairo Kaskazini na Kilosa Kaskazini,” anasema Mama Bakita.
Ni changamoto gani anazopitia katika kazi hio?
Anasema pamoja na matokeo mazuri ambayo yamekuwapo ikiwamo kufanikiwa kusajili watoto 667 katika Wilaya za Mvomero, Kilosa na Gairo tangu kuanza kwa kituo hicho rasmi mwaka 2005, lakini anakiri kwamba kumekuwapo na changamoto anazopitia Mama Bakita katika uendeshaji wa kituo hicho.
Anataja miongoni mwa changamoto zinazoikabili kazi yake hiyo kuwa ni pamoja na uelewa finyu kwa familia zinazopeleka watoto wake katika kituo hicho na kusababisha wazazi kuona mama huyo anatumia changamoto za watoto wao kujinufaisha mwenyewe.
“Bado uelewa ni mdogo kwa baadhi ya wazazi na walezi wa watoto. Wakiona nimepata magunia kadhaa na misaada wanasema ‘Mama Bakita anajinufaisha kupitia migongo ya watoto wetu’ lakini kwasababu ni kazi ninayoofanya kwa moyo sijakata tamaa.
“Changamoto zingine ni pamoja na fedha za kutosha za kuendeshea kituo, vitendea kazi vya kusaidia watoto kukabiliana na changamoto zao na watendaji wa kuwasaidia watoto hawa,” anasema Mama Bakita.
Jitihada gani zimefanyika kukabiliana na changamoto hizo?
Kama wasemavyo Wahenga kwamba wa 100 hapati moja, ndivyo ilivyokuwa pia kwa
Mama Bakita kwani katika kukabiliana na changamoto zinazokabili watoto hao, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kusaidia kwa kuleta mahitaji mbalimbali na kulipia huduma muhimu ikiwemo mafunzo kwa walemavu wa viungo.
“Jitihada nyingine ni kuandikisha watoto katika mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) na mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu ambao umekuwa ukisimamiwa na kutekelezwa na Serikali,” anasema Mama Bakita.
Ikumbukwe kuwa ufanisi wa mfuko huo kwa Wilaya ya Mvomero haukua mzuri kwa miaka kadhaa iliyopita baada ya kukosa usimamizi mzuri kutoka mamlaka husika.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Uwajibikaji Utoaji wa Huduma kwa Jamii iliyotolewa na Taasisi ya Wajibu kutoka kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kiasi cha Sh bilioni 545 hazikutolewa kwa wananchi hivyo kurudisha nyuma jitihada za kupunguza umaskini kwa kaya maskini nchini kama ilivyokuwa lengo la Serikali.
Kwa sasa hali imebadilika baada ya uongozi kubadilishwa na uongozi uliopo kuhakikisha inasajili makundi yote yenye uhitaji wa mfuko huo.
“Huo mfuko upo na tumeshaufuatilia. Kuna vijana wetu kama 7 wameandikishwa, na tunamalizia hatua za mwisho ili waweze kunufaika nao,” anasema Mama Bakita akionekana mwenye matumaini makubwa na mpango huo.
Serikali inasemaje juu ya ufanisi wa mfuko huo?
Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III) Wilayani Mvomero, Mahija Mdoe, anasema katika awamu hii zoezi la uhailishaji linaendelea vizuri fedha zinaendelea kutolewa kwa walengwa licha ya changamoto ndogondogo zilizojitokeza.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na hali ya Jiografia ya Wilaya kutawanyika hivyo inasababisha walengwa kutokufikiwa na fedha kwa wakati.
Hivyo kulazimu kutumia usafiri wa pikipiki na kusababisha gharama za uendeshaji kuwa kubwa.
Pia Mdoe ameiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara ili kusaidia kufikisha fedha za walengwa kwa wakati huku akiitaja changamoto nyingine kuwa ni baadhi ya walengwa kutokuwa na elimu juu ya ujasiriamali, hivyo kusababisha kutumia fedha zao tofauti na matarajio ya mpango huo.
Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji wa TASAF wilayani humo, Khalid Mweta anasema kuwa mapokeo ya wananchi waliowengi ni mazuri.
“Mapokeo ni mazuri na muitikio ni mkubwa, tunajitahidi kuhakikisha tunaboresha mazingira ya upatikanaji wa fedha hizo.
“Uhitaji wa walengwa kuwepo kwenye mpango ni mkubwa kwani mabadiliko yalioanza kuonekana kwa baadhi ya wanufaika ni makubwa,” anasema Khalid.