21 C
New York

Infographic| Mambo unayopaswa kufahamu kuhusu TAWA

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority – TAWA) ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 na kutangazwa kwa amri (Order) ya Serikali iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 135 la tarehe 09 Mei 2014, pamoja na marekebisho yaliyochapishwa katika gazeti la Serikali Na. 20 la Januari 23, 2015.

TAWA ilianza kazi rasmi Julai 1, 2016 kwa kuchukua majukumu ya kiutendaji ya Idara ya Wanyamapori kuhusu usimamizi wa rasilimali ya wanyamapori nje ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Ngorongoro.

Aidha, TAWA inasimamia maeneo yenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 136,287.06 yanayojumuisha Mapori ya Akiba 27 (yenye ukubwa wa kilomita za mraba 97,187.06) na Mapori Tengefu 25 (yenye ukubwa wa kilomita za mraba 39,100).

Aidha, TAWA ni mwangalizi wa shughuli za usimamizi wa wanyamapori kwenye maeneo 21 ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori (WMA) zenye ukubwa wa jumla ya kilometa za mraba 28,223.13. Vilevile, TAWA ni msimamizi wa shughuli za ufugaji wa wanyamapori zinazohusisha mashamba (6), Bustani za Wanyamapori (29), Ranchi (5) na Breeding sites (30).

Kutokana na maboresho ambayo yamekuwa yakifanywa na TAWA katika maeneo yake mbalimbali kwasasa kiwango chake cha mapato kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Kaimu Kamishna wa Hifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, anasema kuwa kunaongezeko la watalii wanaofika kwenye mapori mbalimbali yaliyo chini ya mamlka hiyo kwa ajili ya kufanya utalii mbalimbali ukiwamo ule wa picha ambao umekuwa ni chanzo cha mapato.

Aidha, eneo jingine ni lile la uwindaji wa vitalu ambao pia umekuwa ni sehemu inayoingiza fedha nyingi.

“Mamlaka iliandaa mwongozo wa ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada Guidelines for Allocation of Hunting Blocks through Auctioning pamoja na mfumo wa kielektroniki wa kufanikisha ugawaji wa vitalu hivyo.

“Tangu kuanza kwa ugawaji wa vitalu kwa njia ya mnada mwaka 2019, TAWA imeendesha jumla ya minada saba (07) ya vitalu vya uwindaji iliyohusisha vitalu 100 hadi kufikia Machi, 2022. Katika awamu zote saba ambazo mnada ulifanyika, jumla ya vitalu 79 kati ya 100 viliuzwa kwa kiasi cha Dola za Marekani 9,798,000.

“Kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kuliko fedha ambayo ingepatikana kwa kuuza vitalu vyote 79 kwa njia ya kiutawala (administratively) ambapo zingepatikana fedha kiasi cha Dola za Marekani 3,306,000 sawa na ongezeko la asilimia 196.4. Mamlaka itaendelea kufanya awamu kadhaa za minada ya kielektroniki hadi hapo vitalu vyote vilivyopangwa kufanyiwa minada hiyo vitakapomalizika,” anasema Nyanda.

Akizungumzia eneo la utalii wa picha anasema kuwa kutokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwemo utoaji wa chanjo ya Uviko-19 na utangazaji wa utalii na kuvutia uwekezaji kupitia programu maalum ya “Tanzania – The Royal Tour” mwenendo wa utalii wa picha umeanza kuimarika.

“Katika mwaka wa fedha 2021/22, jumla ya watalii wa picha 158,108 walitembelea katika
maeneo yanayosimamiwa na TAWA. Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 76.2 ikilinganishwa na watalii wa picha 37,684 waliotembelea katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA kwa mwaka 2020/21.

“Kutokana shughuli za utalii (utalii wa picha na uwindaji) Mamlaka imekuwa ikitoa gawio kwa Halmashauri za Wilaya, Vijiji na maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya WanyamaporiWMAs. Kati ya mwaka 2016/17 – 2021/22, Mamlaka imetoa jumla ya Sh bilioni 37.79 kwa wanufaika hao. Sambamba na hilo Kanuni za uwindaji wa kitalii zinaelekeza kampuni zilizokodishwa vitalu vya uwindaji kuchangia shughuli za maendeleo kwa walau dola za Marekani 5,000 kwa kila kitalu kwa mwaka,” anasema Nyanda.

Akifafanua zaidi kuhusu mapato, Nyanda anasema kuwa vyanzo vikuu vya mapato kwa Mamlaka ni uwindaji wa kitalii na utalii wa picha.

Anasema kufuatia mlipuko wa Uviko-19, mapato kwa mwaka 2020/21 yalikuwa Sh bilioni 25.75
sawa na asilimia 47.46 ya makadirio ya lengo la kukusanya Sh bilioni 54.25 katika mwaka husika. Ingawa jukumu la kukusanya mapato linatekelezwa na TRA, TAWA ilikadiria kukusanya jumla ya Sh bilioni 61.1 katika wa mwaka fedha (2021/22) ambapo kwa mujibu wa mfumo wa MNRT Portal jumla ya Sh bilioni 49.5
zilikusanywa kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato sawa na asilimia 80 ya lengo. Kwa ujumla mwenedo wa makusanyo ya mapato yatokanayo na utalii umeanza kuimarika,” anasema Nyanda.

Pia anaongeza kuwa katika fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, maarufu kama fedha za Uviko-19, TAWA iliidhinishiwa Sh bilioni 12.9 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu, ununuzi wa Mitambo, magari na vifaa vingine vya utalii na doria.

“Utekelezaji wa miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali ambapo ujenzi wa barabara kilometa 336.2 kati ya kilometa 463.5 sawa na asilimia 72.5 umekamilika katika mapori ya Akiba Wami Mbiki, Kijereshi, Mkungunero, Lukwika Lumesule, Liparamba, Igombe na Rungwa.

“Aidha, ujenzi wa malango makubwa mawili kati ya manne katika Mapori ya Mkungunero na Swagaswaga umekamilika na malango mawili katika mapori ya Wamimbiki na Kijereshi yapo katika hatua za umaliziaji (Finishing). Vilevile, magari matatu kati ya sita yaliyoapngwa kununuliwa yalishapokelewa na magari matatu yaliyosalia yanatarajiwa kupokelewa Mwezi huu wa Septemba 2022 kutoka Wakala wa Huduma za Manunuzi Serikalini (GPSA),” anasema Nyanda.

Zaidi angalia mchanganuo wa mapato hayo yaliyokusanywa na TAWA kwenye usanifu wetu hapo juu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img