Na Faraja Masinde, Gazetini
Hadi sasa Tanzania imefanikiwa kutoa chanjo ya Polio kwa Watoto 27,952,164 wenye umri chini ya miaka mitano.
Idadi hiyo ni baada ya kukamilisha awamu tatu za chanjo kati ya nne zilizopagwa kutolewa ndani ya mwaka huu.
Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amebainisha kuwa watoto 14,690,597 wenye umri wa chini ya miaka mitano kutoka mikoa ya Tanzania Bara wamechanjwa dhidi ya polio katika awamu ya tatu ya chanjo kuanzia Septemba 1-4, mwaka huu.
Kwa ujibu wa Waziri Ummy katika awamu ya tatu ya chanjo dhidi ya polio ililenga kuwapa chanjo watoto 12,386,854, lakini wamefikiwa watoto 14,690,597 wamechanjwa sawa na asilimia 118.6.
Kwa mujibu wa Serikali, awamu ya nne ya utoaji chanjo dhidi ya polio na ya mwisho itaanzia Novemba 2022.
Amesema chanjo dhidi ya polio kwa watoto ilifuatia ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa Februari 2022 kuhusu mlipuko wa virusi vya polio nchini Malawi ambapo wagonjwa wawili waliripotiwa na Msumbiji ambapo visa vinne viliripotiwa.
Tanzania ilikamilisha awamu ya pili ya chanjo ya nyongeza dhidi ya polio Mwezi Mei 2022 na kufikia jumla ya watoto 12,131,049 ikiwa ni zaidi ya lengo la kufikia watoto 10,295,316, sawa na asilimia 117.8.
Idadi hiyo inafanya watoto waliopata chanjo ya polio hadi sasa kuwa 27,952,164, idadi hiyo inajumhisha watoto 1,130,261 waliopata chanjo hiyo awamu ya kwanza Machi, mwaka huu sawa na asilimia 115.
Tanzania ilithibitishwa kuwa haina polio Mwaka 2015 baada ya miaka mingi kupita bila kuwa na maambukizi mapya ya polio. Aidha, Tanzania haijagundua kisa cha polio tangu mwaka 1996.
“Tuna kila sababu ya kuwalinda watoto wetu dhidi ya polio,” anasisitiza Waziri Ummy.
“Tuna kila sababu ya kuwalinda watoto wetu dhidi ya polio,” anasisitiza Waziri Ummy.