1.4 C
New York

Visual| Miaka 40 ya UKIMWI: Namna Afrika ilivyotikiswa

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

Ni zaidi ya miaka 40 sasa tangu kuripotiwa kwa kisa cha Virusi Vya UKIMWI, hata hivyo bado ugonjwa huo umeendelea kuwa janga la afya duniani, hususan barani Afrika.

Kama inavyofahamika kwamba Afrika inabeba takribani 17.51% ya idadi ya watu duniani nyuma ya bara la Asia lenye 59.35%.

Hata hivyo, Afrika ndio imekuwa na mzigo mkubwa linapokuja suala la maambukizi ya VVU kwani inabeba sehemu kubwa ya jumla ya maambukizo yote ulimwenguni sawa na takribani watu milioni 28.5.

Aidha, zaidi ya hayo, 91% ya watoto wenye VVU wako barani Afrika.

Idadi hii kubwa ya maambukizo barani Afrika inachangiwa kwa kiasi kikubwa na upatikanaji duni wa huduma za afya, ngono zisizo salama na maambukizi makubwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hata hivyo, isivyo bahati zaidi ya 20% ya watu wanaoishi na VVU barani Afrika hawajui kwamba wameambukizwa. Kwa athari hii kubwa, hii ni dalili tosha ya hitaji la upatikanaji na uwezo wa kumudu upimaji wa VVU na matibabu katika bara la Afrika.

VVU/UKIMWI’ vinathiri bara la Afrika

Takwimu zinabainisha kuwa takriban nusu ya watu wazima wote wanaoishi na VVU duniani kote ni wanawake na wanawake kati ya umri wa miaka 10 na 24 wana uwezekano mkubwa wa kuambukizwa kuliko wanaume wa kundi moja la umri.

Ikumbukwe kuwa madhara ya VVU kwa wanawake, hasa barani Afrika, hayazingatiwi sana. Zaidi ya hayo, watoto milioni 1.7 kati ya umri wa miaka 0-14 kwa sasa wanaishi na virusi.

UKIMWI unaendelea kuathiri sekta ya elimu pia, huku watoto wakiacha shule ili kutunza wanafamilia wanaougua au kufanya kazi.

Zaidi ya hayo, kuelimisha watoto kuhusu VVU/UKIMWI na kuwafundisha jinsi ya kujilinda bado ni changamoto, hii ni kwa sababu watoto wa lika balehe wako hatarini zaidi kuambukizwa VVU.

Kiuchumi, virusi tayari vimepunguza viwango vya ukuaji wa uchumi wa kitaifa kwa wastani wa 2-4% kwa mwaka kote barani Afrika, na athari kubwa kwa usambazaji wa wafanyikazi, viwango vya uzalishaji na kutegemea bidhaa kutoka nje.

Athari za Uviko -19 kwa VVU/UKIMWI

Ni wazi kwamba janga la Uviko-19 limeleta changamoto mpya kwa wale wanaoishi na VVU/UKIMWI, na virusi hivi viwili lazima vishughulikiwe kwa pamoja.

Ripoti ya pamoja ya UNICEF na UNAIDS ilionyesha kuongezeka kwa viwango vya VVU kwa vijana wakati wa janga hilo, kutokana na kupungua kwa upatikanaji wa huduma za kinga kutokana na hatua za kuzuia Uviko -19.

Kwa watu wanaoishi na VVU pia wana uwezekano mkubwa wa kuambukizwa kesi kali ya Uviko-19 licha ya ugonjwa huo kutokuwa na makali zaidi kwa sasa.

Changamoto zilizosalia

Zaidi ya vipimo vya haraka, matibabu na hatua za kuzuia hata hivyo changamoto kadhaa za ziada zimesalia, zikiwemo:

Unyanyapaa dhidi ya VVU/UKIMWI huongeza usiri na ukanushaji, jambo ambalo linaweza pia kusababisha kuongezeka kwa maambukizi ya VVU na kuzuia utoaji wa huduma bora za matibabu. Kutokana na hili, bado kuna idadi ndogo ya watu ambao hutafuta kupima kwa hiari.

Pamoja na jitihada kubwa ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya Tume ya Kudhibiri UKIMWI(TACAIDS) za kuhakikisha kuwa kunakuwa na dawa za kutosha za kurefusha maisha (ARV) kwa watu wote wenye uhitaji wa dawa hizo, bado kumekuwapo na kukosekana kwa usiri baina ya watoa huduma jambo ambalo limeendelea kulalamikiwa.

Pamoja na jitihada hizo za serikali bado kumekuwa hakuna muitikio wa kutosha kwa watu wengi kujitokeza kupima na kutambvua hali zao jambo ambalo linarudisha nyumba udhibiti wa janga hilo kama yalivyo malengo ya Kidunia ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 ugonjwa huo inabaki histori.

Pia unyanyapaa ni kati ya vikwazo vinavyoelezwa na baadhi ya watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi(WAVIU), hivyo ni eneo jingine linalopaswa kutupiwa jicho na serikali.

Katika sura nyingine serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususan sekta binafsi imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa inakusanya fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa Ukimwi(ATF) lengo likiwa ni kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhiri.

Kwani kama inavyofahamika kwamba katika mapambano ya Ukimwi Tanzania inategemea asilimia 94 ya fedha kutoka kwa wafadhiri huku yenyewe ikibaki na asilimia 6 tu jambo ambalo halina afya hata kidogo katika mapambano haya licha ya ukweli kuwa kama nchi tuko sehemu nzuri.

Kwanini huduma za upimaji ni muhimu?

Hii ni kwa sababu zaidi ya asilimia 40 ya watu wanaoishi na virusi barani Afrika bado hawajui kuwa wameambukizwa, jambo linaloashiria hitaji la huduma za upimaji zinazoweza kupatikana kwa bei nafuu.
Hii ikihusisha pia mazingira rahisi na rafiki kwa mtu kufanya vipimo vya VVU.

Mbinu za ushindi kwa Tanzania na Afrika

Ni bayana kuwa Afrika bado ina safari ndefu katika kushinda vita dhidi ya VVU/UKIMWI, licha ya kuwapo kwa dalili njema kwa nchi kama Tanzania ambayo imefikia hatua nzuri ya malengo yake.

Mfano katika maambukizi mapya Utafiti wa mwaka 2021 uliotolewa na UNAIDS unaonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI ambapo takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yamepungua kutoka 68,000 mwaka 2020 hadi 54,000 mwaka 2021.

Aidha, idadi ya vifo imepungua kutoka watu 32,000 mwaka 2020 hadi 29,000 mwaka 2021 huku changamoto kubwa ikiendelea kubaki kwa vijana.

Kulingana na UNAIDS, vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 28 ya maambukizi mapya huku kati ya kundi hilo asilimia 73 wakiwa ni vijana wa kike.

Sambamba na hilo serikali za Afrika zinapaswa kujitolea kuimarisha mipango inayoongeza uwezo wa watu binafsi, hasa wanawake na watoto, ili kujilinda. Pia kukomesha unyanyapaa unaozunguka virusi pia ni muhimu.

Ili kufanikisha hili, serikali za Afrika ikiwamo Tanzania zimeendelea kutoa elimu na kujenga uelewa kwa makundi muhimu ili kushirikiana katika kupaza sauti kupinga unyanyapaana kuhamasiaha watu kwenda kupia VVU na kutambua hali zao.

Hali ya Unyanyapaa

Matokeo ya Utafiti wa Unyanyapaa na Fahirisi ya mwaka 2021 yanaonyesha kuwa Kitaifa: unyanyapaa wa bianafs ni 6.4%.

Aidha, Mjini na Vijijini: Mjini wanaathiriwa zaidi kwa 7.1% na Vijijini kwa 4.8%. Sambamba na hayo, Matokeo yanaonyesha zaidi kuwa, Kitaifa: unyanyapaa umepungua kutoka 28.0% mwaka 2013 hadi 5.5% mwaka 2021.

Mkoa wa Kilimanjaro ndio unaongoza kwa kuwa na 19.5% ukifuatiwa na Tanga 10.5%. Upande wa kimkoa, mkoa wa Mtwara unaongoza kwa kuwa na 27.4% ukifuatiwa na Geita wenye 26.6%.

Mwishoni mwa Juni, mwaka huu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, George Simbachawene alizindua ugawaji wa vishikwambi zaidi ya 4,000 kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kwenye Halmashauri 18 nchini, ili kufundishia elimu ya kujikinga na VVU, Afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia na stadi za maisha ili kupunguza maambukizi ya VVU kwa wasichana balehe na wanawake vijana.

Ni wazi kuwa kupitia mradi wa Timiza Malengo kwa wasichana balehe na wanawake vijana, utawezesha kuwafikia vijana ambao tayari wako nje ya mfumo wa elimu ambao wakati mwingine imekuwa ni ngumu kufikiwa ikilinganishwa na wenzao walioko shuleni.

Hii ni sawa na kusema kwamba serikali inajitahidi kufikisha elimu kila sehemu ili kupunguza maambukizi ya VVU kadri itakavyowezekana kama si kumaliza kabisa janga hilo ifikapo mwaka 2030.

Tacaids pia mbali ya kutumia vyombo vya habari pia imekuwa ikihusisha viongozi wa dini ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa ni sauti kuu kwa waumini wao katika madhehebu mbalimbali na hivyo kusaidia kuchochea jamii kujitokeza kupima VVU na kupiga vita unyanyapaa.

Pia tume imekuwa ikijitahidi kuwahusisha watu wenye VVU katika utoaji wa huduma, kukabiliana na mahitaji ya watu wanaonyanyapaliwa.

Mfano katika Utafiti za unyanyapaa na ubaguzi nchini wa mwaka 2021 tume iliwatumia WAVIU jambo ambalo linasaidia kuibua changamoto na majibu halisia kutoka kwa wahusika wenyewe.

Hivyo, yote kwa yote tunahitaji kushikamana kama taifa kila mmoja kwa nafasi yake katika kuhakikisha kuwa janga la UKIMWI linasalia kuwa historia ifikapo mwaka 2030.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img