Ni kama ugonjwa wa Uviko-19 umeanza kusahaulika miongoni mwa Watanzania na hivyo watu hawaoni tena haja ya kuchanja chanjo kujikinga na mafua hayo makali, jambo ambalo si kweli.
Kwa maneno mengine unaweza kusema kuwa watu wanachukulia poa ilihali maisha ya watu yanapotea.
Wapo wanaosikika wakisema kuwa hawaoni haja tena ya kuchanja kwa kuwa ugonjwa huo tayari umeshapoteza nguvu si kama awali.
“Mimi sioni tena haja ya kuchanja hizo chanjo zao maana tayari waliochanja wanatosha, ingekuwa kuna umuhimu basi tungeendelea kuhimizwa juu ya kuchanja kila wakati.
“Lakini sasahivi wewe mwenyewe si unaona kimya tu hamna tena mtu anayehamasisha na maisha yanaendelea kama kawaida, kwa hiyo hata mimi sioni tena sababu ya kuchanja kwanza chanjo zenyewe sio nzuri na sio vitu vya kuendekeza kwa hiyo niacheni…pia bado mimi sijazeeka kiivo hadi nichanje chanjo,” anasema Judith Minja(32) Mjasiriamali na mkazi wa Jiji la Kibiashara la Dar es Salaam.
Hayo yanajiri katika kipindia ambacho takwimu haziko upande wa Tanzania kwani kasi ya uchanjaji chanjo ya Uviko-19 nchini bado sio ya kuridhisha.
Hadi kufikia Aprili 3, 2022 Tanzania ilikuwa imepokea jumla ya dozi 11,233,374 huku idadi ya Watanzania waliojitokeza kupata chanjo hizo wakiwa ni 3,318,374 pekee hivyo bado mlima ni mkubwa.
Hii ni sawa na kusema kwamba idadi ya chanjo ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wanao chanja, jambo ambalo linaashiria kuwa bado kuna nguvu kubwa inatakiwa kufanyika katika kuhamasisha Wanzania kupata chanjo hizo.
Kiwango hicho cha uchanjaji ni sawa na asilimia 10.79 lengo likiwa ni kuwafikia Watanzania 30,740,928 kati ya Watanzania wote 57,637,628 (kwa mujibu wa makadirio ya ofisi ya Taifa ya Takwimu-NBS).
Aidha, kama hiyo haitoshi, hadi kufikia Aprili 3, 2022 Watanzania ambao walikuwa wamethibitika kuambukizwa ugonjwa huo tangu ulipoingia nchini Machi 2020 walikuwa 33,842 huku waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo wakifikia 803, hii itoshe tu kusema kwamba UGONJWA UPO hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha kuwa unapata chanjo ya uviko-19.
Hatari zaidi Dar es Salaam
Wizara ya Afya ya Tanzania inakiri kuwa kulingana na mwenendo wa ugonjwa huo tangu uliporipotiwa nchini mwaka 2020 Mkoa wa Dar es Salaam ndio umekuwa ukionyesha kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ikilinganishwa na maeneo mengine.
Mfano, katika ripoti ya wizara ya afya iliyotolewa na Waziri wake , Ummy Mwalimu Aprili mwaka huu, inaonyesha kuwa mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuwa na maambukizi zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine.
“Katika kipindi cha Machi 5 hadi Aprili 3, mwaka huu kuna jumla ya visa vipya 116 vya waliothibitika kuwa na maambukizi kati ya watu 25,890 waliopimwa sawa na asilimia 0.45.
“Aidha, mkoa wa Dar es Salaam umeendelea kuwa na idadi kubwa ya watu waliothibitika kuwa na maambukizi watu 70 sawa na asilimia 60.3 ya visa vyote,” anabainisha Waziri Ummy.
Wasiochanja wanapata shida zaidi
Ummy nasema katika kipindi hichohicho wagonjwa wapya 22 walilazwa.
“Wagonjwa hawa wote walikuwa hawajachanjwa, aidha siku ya Aprili 3 wagonjwa mahututi walikuwa wawili na wote walikuwa hawajapata chanjo yoyote ya kujikinga na uviko 19. Pia vifo vitatu viliripotiwa, viwili kutoka Dar es Salaam na kimoja Mwanza,” anabainisha Ummy.
Mwenyenendo wa uchanjaji chanjo ya uviko 19 hapa nchini unaonyesha kuwa idadi imekuwa ikiongezeka kila kunapotangaza kampeni mpya ya uchanjaji, miongoni mwa kampeni hizo ni pamoja na ile ya Mkoba, Ujanja ni kuchanja na nyingine.
Hii ni sawa na kusema kwamba serikali inapaswa kuja na kampeni zaidi au kuzipa nguvu zile zilizopo ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi.
“Kwa sasa wasio chanja tunawapelekea walipo, hii ina faida na tunaweza hata kuyafikia makundi maalumu wakiwamo walemavu na wazee.
“Kwani si rahisi sana wakati mwingine mtu kufika kituoni kwajili ya chanjo ya uviko, hivyo inahiyajika nguvu ya ziada kuwafuata huko waliko,” anasema Waziri Ummy ambaye anasisitiza kuwa lengo ni kufikia asilimia 70 ya kundi lililopangwa.
Kidole kwa Serikali
Lakini Maxwell Rogers(45) yeye anailaumi Serikali na mamlaka zake kwa kusema kuwa yenyewe ndio imechocchea zoezi la uchanjaji kuwa gumu kutokana na kupunguza hamasa, huku akitoa mfano.
“Unajua bwana hili jambo la chanjo ya corona serikali yenyewe ndio imesababisha liende taratibu, unafikiri kama wangeendelea na ile kasi waliyokuwa nayo mwanzo sasahivi tungekuwa wapi.
“Labda nikukumbushe, unakumbuka wakati ule hamasa zilikuwa nyingi sana karibu kila chombo cha habari, lakini siku hizi hakuna na hiyo ilikuwa ikisukuma watu wengi kwenda kupata chanjo.
“Unakumbuka wakati flani serikali ilikuja na mpango kwa mashabiki wanaoingia uwanjani ukichanja unaingia uwanjani bure, fikiria mpango huo ungeendelea hadi hii leo, kama hivi Klabu ya Simba ilivyokuwa ikishiriki michuano ya kimataifa na kuujaza uwanja unadhani tungekuwa wapi?
“Ukiacha hilo, hivi serikali inaona hasara gani kwenda pale kigamboni kwenye pantoni ikatangaza kwamba ukichanja utapita bure kwa wiki nzima unadhani hilo zoezi lingeshindikana? au kwenye usafiri wa mwendokasi utasafiri bure siku nzima, ni nani ambaye angekataa ofa hiyo?, maisha sasahivi ni magumu hamna mtu ambaye angekataa jambo jema kama hilo lazima wangechanja tu,” anasema Maxmilian.
Uviko-19 ni nini?
Virusi vya korona ni kundi kubwa la virusi ambayvo kwa kawaida hupatikana miongoni mwa wanyama na vinaweza kusababisha ugonjwa kwa wanyama na binadamu.
Kwa binadamu, virusi vya korona husababisha magonjwa ya kupumua kama vile homa ya kawaida isiyo na dalili kali na Dalili za Upumuaji za Middle East (Middle East Respiratory Syndrome (MERS) na Dalili Kali na Hatari za Upumuaji (Severe Acute Respiratory Syndrome (SARS).
Virusi vilivyopatikana hivi karibuni husababisha Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.
Mtu yeyote anayekumbana na virusi vinavyosababisha UWIKO-19 yuko hatarini.
Hata hivyo, watu wa umri mkubwa, na wale walio na hali nyingine za kiafya kama vile shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na ugonjwa wa kisukari au wale ambao kinga ya mwili imedhoofika, kama vile watu walio na VVU/UKIMWI au saratani, wako katika hatari zaidi na wana uwezekano mkubwa wa kupata dalili kali.
Zingatia
Daima unakumbushwa kupata dozi kamili ya chanjo kwa wakatiili kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19, kuepuka mikusanyiko siyo ya lazima, kuvaa barako kwa usahihi na wati wote unapokuwa kwenye maeneo yenye mkusanyiko pia kufuniko mdomo na pua kwa kitambaa safi wakati wa kukooa.
Jambo jingine ni kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huu au kupiga SIMU BURE namba 199.