2.9 C
New York

Infographic| Ukeketaji bado haujaisha

Published:

Ukeketaji ni kitendo cha kimila kinachotekelezwa na baadhi ya jamii ambapo sehemu ya nje ya via

Ukeketaji ni kitendo cha kimila kinachotekelezwa na baadhi ya jamii ambapo sehemu ya nje ya via vya uzazi vya mwanamke huondolewa, huchanjwa, hukatwa ama huharibiwa kabisa kwa sababu zisizo za kitabibu.

Ukeketaji unatambulika kama mojawapo ya aina ya ukatili wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za wanawake na watoto wa kike.

Februari 6, ya kila mwaka, Tanzania huungana na mataifa mengine Duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji kwa Wanawake na Watoto wa kike. Historia ya ukeketaji imeendelea kuwepo kwa takribani karne 21 sasa.

Ilipofika mwaka 2003 Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha Februari 6, ya kila mwaka kuwa siku rasmi ya maadhimisho ya kutokomeza ukeketaji Duniani.

Kwa upande wa Tanzania maadhimisho haya yameanza kufanyika mwaka 2010.
Maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa Serikali na Wadau wa masuala ya Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana hususan ukeketaji kujitathmini hatua iliyofikiwa katika kutekeleza afua za kutokomeza ukeketaji nchini.

Hii ikiwa ni pamoja na mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa afya hizo.
Aidha, kubadilishana uzoefu wa namna bora zaidi ya kukabiliana na vitendo vya ukeketaji unaofanywa na baadhi ya jamii zetu hapa nchini.

Kichocheo kikuu cha vitendo vya ukeketaji hapa nchini ni MILA NA DESTURI za baadhi ya makabila katika jamii za kumvusha rika mtoto wa kike kutoka usichana na kuwa mwanamke kamili.

Jamii inayokeketa huamini kuwa msichana aliyekeketwa anakuwa tayari kuolewa, sababu hii imepelekea ongezeko la mimba na ndoa za utotoni.

Sababu nyingine ni mila ya kutambika ikiwa pamoja na kutii masharti ya mizimu ya baadhi ya jamii kuamini kuwa ukeketaji huondoa mikosi katika familia.

Vilevile, zipo sababu za kiuchumi ambapo ngariba na wazee wa mila hulipwa fedha au vitu ili kutimiza azma hiyo.

Kadhalika, wazazi wa watoto wanaokeketwa huwa na matarajio ya kuwaoza mabinti zao kwa lengo la kupata kipato kupitia mahari inayotolewa.

Hata hivyo jamii inapaswa kutambua kwamba kumvusha rika mtoto wa kike kutoka usichana na kuwa mwanamke kamili siyo lazima kumkeketa.

Aidha, jambo muhimu zaidi hapa ni jamii inapaswa kuelewa kuwa mila na desturi hii ni hatari kwa msichana hivyo tuiache.

Kwani iko wazi kwamba mwanamke anaweza kuolewa anapofikisha umri wa miaka 18 na si baada ya kukeketwa.

Ukeketaji kwenye baadhi ya jamii zetu ni chanzo cha ndoa na mimba za utotoni.
Hivyo, tuzuie vitendo vya ukeketaji katika jamii ili tumlinde mtoto dhidi ya mimba na ndoa za utotoni ambazo zimesababisha kuharibu malengo na ndoto za watu wengi.

Ikumbukwe kwamba, utajiri hauwezi kuupata kwa kukeketa au kumuoza binti yako, fanya kazi halali na kwa bidii utajiongezea kipato wewe na familia yako. Mlinde na mwendeleze mtoto wa kike kwa faida yako na ya Taifa.

Msichana akikeketwa anapata msongo wa mawazo na kuathiri matendo yake katika kipindi chote cha maisha yake. Ni jambo la busara iwapo tutamlinde ili afikie maono yake.

Sote ni mashahidi kwamba ukeketaji unaweza kusababisha kupoteza damu nyingi na kupelekea kupoteza maisha. Ni hatari kwa usalama wa msichana na mwanamke.

Hata hivyo changamoto kubwa kwasasa ni kuwa ukeketaji umekuwa ukifanyika kwa siri na hauzingatii kanuni za afya na hivyo msichana au mwanamke aliyekeketwa anakuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Virusi vya UKIMWI.

Kama hiyo haitoshi,ukeketaji ni chanzo mojawapo cha ugonjwa wa fistula yaani kutokwa na haja ndogo bila kujizuia mara baada ya kujifungua. Tuache kukeketa kumlinda mwanamke dhidi ya ugonjwa wa fistula.

Hivyo ni muhimu kwa jamii yetu kuchukua tahadhari katika kuhakikisha kuwa ukeketaji unafika ukomo. Zaidi angalia usanifu wetu hapo juu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img