8.3 C
New York

Infographic| Ugumu uliopo mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini

Published:

Tanzania imekuwa ni kati ya nchi zinazopambana kwa dhati kuhakikisha kuwa inafikia sehemu nzuri ya udhibiti wa dawa za kulevya kama si kumaliza kabisa vita hiyo.

Katika kulifanikisha hilo jududi mbalimbali zimekuwa zikichukulia na Serikali katiia kuhakikisha dawa za kulevya zinakoma kabisa kwani siyo tu kwamba zinaathiri familia bali nguvu kazi ya taifa kwa ujumla.

Katika kulifanikisha hilo ndio maana serikali ikaunda Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) ambayo imekuwa ikifanya kazi nzuri ya kudhibiti dawa hizo hapa nchini.

Kwani takwimu zinaonyesha kwamba kwa mwaka 2020 jumla ya kilo 13,230.23 za Bangi, kilo 11,804.87 za Mirungi, kilo 4.52 za Cocaine na kilo 349.81 za Heroin zimekamatwa.

Aidha, katika ukamataji huo jumla ya kesi 7,361 zimefunguliwa zikihusisha watuhumiwa 9,265 ambapo watuhumiwa 751 ni wanawake na watuhumiwa 8,514 ni wanaume. Pia imefanikiwa kufanya ukaguzi katika makampuni 106 yanayojihusisha na uingizaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya katika vituo vya Forodha vya Tarakea, Holili, Namanga, Tunduma, Kasumulo, Mabamba, Manyovu na makampuni ya kusafirisha vifurushi.

Aidha, Mamlaka pia imeweza kuzuia uingizwaji wa kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe
kinyume na sheria kiasi cha kilo 57,600 kwa mwaka 2020.

Hata hivyo Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI ya mwaka ya Shughuli zilizotekelezwa kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022 inabainisha kuwa bado kuna changamoto lukuki zinazoikabili DCEA.

Kamati hiyo imebainisha kuwa DCEA tangu kuanzishwa kwake imekuwa haitengewi bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa na Kulevya, Kamati imebaini kuwa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mamlaka imekuwa haitengewi bajeti kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

“Mojawapo ya athari za kutotengewa fedha za maendeleo ni kuwepo kwa changamoto ya vituo vichache vya kliniki za kutolea dawa ya methadone kwa waraibu wa dawa za kulevya ambapo huduma hiyo ya tiba inatolewa kwa baadhi ya hospitali za Mikoa ya Dar es Salaam, Songwe, Mbeya, Tanga na Arusha,” imeeleza taarifa hiyo iliyowasilishwa Bungeni Februari 10, 2022.

Aidha, taarifa hiyo inabainisha kuwa kutokuwepo kwa Sera ya Taifa ya Kupambana na dawa za kulevya ni suala lenye uzito mkubwa na hivyo linahitaji msukumo wa ziada.

“Elimu kuhusu matumizi na madhara ya dawa za kulevya na uelewa mdogo juu ya madhara ya dawa za kulevya na njia sahihi za kupambana na tatizo la dawa za kulevya miongoni mwa wananchi/jamii bado haijawafikia wananchi wengi na hivyo kuongezeka kwa vitendo vya utumiaji dawa za kulevya na kuongezeka kwa unyanyapaa miongoni mwa waraibu walioacha matumizi ya dawa hizo pindi wanaporudi katika familia zao.

“Kukosekana kwa mfumo maalum katika ngazi ya jamii kwa ajili ya kuwatambua waraibu wa dawa za kulevya. Kwa sababu hiyo kunakuwa na upungufu wa mwitikio wa Kitaifa wa kupambana na tatizo hilo, hii ni pamoja na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu matumizi na madhara ya dawa za kulevya kama ilivyofanyika kwa mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU/UKIMWI,” inafafanua.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa tatizo la dawa za kulevya linavuka mipaka ya nchi na hivyo huhusisha mataifa mbalimbali na kwamba Mamlaka bado inayo kazi kubwa ya kufanya katika kuhakikisha kuwa jambo hilo linadhibitiwa.

“Mamlaka pia inahusika katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuongeza jitihada za kikanda na kimataifa katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya duniani.

“Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka katika kupambana na dawa za kulevya na kukamilisha Mwongozo wa Uanzishwaji na Uendeshwaji wa Nyumba za Upataji Nafuu (Guidelines for Management of Sober Houses in Tanzania); Kamati imebaini kuwa bado hakuna Nyumba za Upataji Nafuu za Serikali.

“Kamati inaona ipo haja ya Serikali kuona umuhimu wa kuchukua hatua ya kujenga nyumba za upatajinafuu kwa ajili ya waathirika wa dawa za kulevya ili kuipunguzia jamii gharama zinazotozwa na asasi za kiraia,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, imefafanua changamoto nyingine ambayo imekuwa mwiba katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kuwa ni uwepo wa ukubwa wa mipaka ya nchi ardhini na baharini na kuongezeka kwa njia za vipenyo zisizo rasmi huchangia kufanya doria au udhibiti wa uingizwaji wa dawa za kulevya kutofanyika kwa ukamilifu.

Kamatai hiyo imeishauri serikali kuanzisha Ofisi za Mamlaka za Kanda zitakazoimarisha udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.

“Pia ni ushauri wa kamati kwamba DCEA kuanzisha maabara yenye uwezo wa kufanya tafiti na utambuzi wa dawa za sasa na bidhaa mpya zinazoingizwa sokoni, kwani utafiti unaonesha kwamba kumekuwepo na ongezeko kubwa la Magonjwa ya Akili, UKIMWI, Kifua Kikuu na Homa ya Ini miongoni mwa waathirika wa dawa za kulevya na hivyo kuathiri tiba miongoni mwao na jamii
kwa ujumla, hivyo serikali ionea umuhimu wa kuchukua hatua za kuongeza huduma za tiba ili kuwafikia waathirika,” imeeleza taarifa hiyo.

Unaweza kuangalia usanufu wetu hapo juu kuona baadhi ya changamoto hizo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img