1.4 C
New York

Infographic| Tunayofahamu kuhusu hali ya Saratani nchini

Published:

*Mapambano ya saratani ya mlango wa kizazi yaendelea

“Kupima saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake ndio mpango mzima…tupambane tuishinde isiue mtu. Mko wapi akina mama…kina Dada mko wapi?,” ni ujumbe unaotolewa na Dk. Lucia Laurian ambaye ni Daktari kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, wakati akitoa elimu kwenye mamia ya wakazi waliokusanyika kwenye gulio la kila Jumatatu katika mji mdogo wa Kemondo uliyo kilometa chache kutoka mjini Bukoba.

Ujumbe huo wa Dk. Lucia ambao umeambatana na mifano kadhaa ya maisha halisi na namna ya kuyakabili majukumu, unaonekana kuwaingia baadhi ya wananchi waliokusanyika kwenye gulio hilo linalouza bidhaa mbalimbali za nyumbani ikiwamo nguo na mahitaji mengine muhimu.

Hata hivyo, kwa nyuso na mshangao wa wananchi hao wa Kemondo wanawake kwa wanaume zinaonyesha dhahili kuwa hawana wanalolifahamu juu ya saratani ya mlango wa kizazi.

Kuwapo kwa mazingira hayo ndiyo kunalisukuma Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughuliki Uwezeshaji Wanawake (UN-WOMEN) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya AMWAVU pamoja na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kutoa elimu kwa wananchi hawa wa Kemondo na maeneo mengine ya Mkoa wa Kagera.

Gasper Lutainulwa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Wanawake wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI mkoani Kagera (AMWAVU) lenye makao makuu yake mjini Bukoba ambaye anasema kuwa dhamira kubwa ya mpango huo ni kuhakikisha wanaunganisha sauti ya pamoja ya wanawake hasa wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI (VVU) waweze kutetewa pia kupiga vita unyanyapaa kwa kuamini kuwa hiyo ni changamoto kubwa kuliko hata UKIMWI wenyewe.

Hata hivyo, pamoja na hayo, AMWAVU ambayo hadi sasa ina wanachama 75, inahimiza kampeni ya saratani ya mlango wa kizazi.

Je kwa nini saratani ya mlango wa kizazi?

Gasper anasema mradi huo una uhusiano mkubwa na VVU na kwamba mwanamke anyeishi na maambukizi hayo yuko kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani kutokana na kinga zake kuwa ndogo.

“Lengo kubwa hasa la mradi huu ni kuhakikisha tunatoa elimu jumhishi, tunahamasisha na kuikumbusha jamii dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi na kuwahimiza kufika kwenye vituo vya afya ambavyo serikali ndani ya mkoa wa Kagera imesogeza huduma za uchunguzi wa saratani katika hituo hivyo.

“Hivyo, kazi yetu ni kuhakikisha tunaingia katika jamii na kuwakumbusha wanawake kwenda kufanya uchunguzi wa saratani kwani tunaamini kwa kufanya hivyo tutanusuru asilimia 85 ya wanawake wanaoishi na VVU ambao wako kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa aina hii ya saratani,” anasema Gasper na kuongeza kuwa:

“AMWAVU kwa kushirikiana na TACAIDS na wafadhiri wa mradi huu UN-WOMEN lengo letu katika mkoa wa Kagera ni kuhakikisha tunatoa elimu na kuikumbusha jamii juu ya umuhimu wa kwenda kupima na kuchunguzwa dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi kwani kama mtu anabainika kuwa na dalili za saratani tunalazimika kushughulikia rufaa yake ili apatiwe matibabu.

“Mradi huu unaotekelezwa mkoa mzima wa Kagera ukilenga zaidi wanawake wanaoishi na VVU hasa maeneo ya vijijini, hivyo tunategemea watajitokeza kwa wingi na watakaobainika kuambukizwa watalazimika kuanza matibabu haraka iwezekanavyoilikuwaepusha na kupoteza maisha,” anasema Gasper.

SOMA PIA: https://gazetitz.wordpress.com/2021/10/28/infographic-jitihada-za-kutokomeza-saratani-ya-mlango-wa-kizazi-tanzania/

Hamasa kwa Wananchi

Akiendelea kutoa sababu za umuhimu wa wanawake mkoani humo juu ya kuona umuhimu wa kujitokeza kujua hali zao kuhusu saratani ya mlango wa kizazi.

Dk. Lucia anasema kuwa ni muhimu kwa kina mama kufika hospitali kwa ajili ya kuchagua aina ya uzazi wa mpango hatua ambayo anasema kuwa itamsaidia mama kujiepusha na magonjwa nyemelezi ikiwamo saratani kutokana na kuchoka hatua inayochangiwa na kuzaa mara kwa mara.

“Lakini pia niwakumbushe akina mama kufikia kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kuchagua njia bora ya uzazi wa mpango ambayo itakuwa na faida kwa afya yako kukuwezesha kupata mtoto kwa muda utakaopanga.

“Kwani lengo letu ni kwamba pamoja na wewe kupata watoto lakini ubaki ukiwa na afya yako nzuri bila kukuingiza kwenye hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi,” anasema Dk. Lucia.

Dk. Lucia anasema iwapo mwanamke atasimama kwenye nafasi yake kwa kujua afya yake itamsaidia kujikinga siyo tu na saratani ya mlango wa kizazi bali hata VVU na magonjwa mengine.

Kukosa maamuzi pia ni sababu

Aidha, Dk. Lucia anabainisha sababu nyingine ambayo inaweza kusababisha mwanamke kupata saratani ya mlango wa kizazi kuwa ni pamoja na umaskini.

“Kuna wakati kutokana tu na umaskini mwanamke anajikuta kipata saratani ya mlango wa kizazi, kwani kukosa fedha kunachochea baadhi ya wanawake kushawishika kirahisi na hatimaye kufanya mapenzi bila kutumia kinga na matokeo yake kupata mimba bila kutarajia zinazosababisha mama kuchoka zaidi.

“Hivyo niwatake wanawake msidanganyike na maneo kama hayo, yaani umaskini wako usikupelekee kupata saratani ya mlango wa kizazi ambayo unaweza kuiepuka kwa kufanya kazi kwa bidii ikiwamo ujasiriamali na kujiunga na vikundi mbalimbali,” anasema na kusisitiza kuwa hakuna haja ya mama kupoteza maisha kwa saratani ya mlango wa kizazi ambayo ingeweza kuepukika,” anasema Dk. Lucia.

Wananchi wanasemaje?

Lyidia Josephat ambaye ni mkazi wa Kemondo mkoani Kagera kwanza anawashukuru waratibu wa mpango huo kwa kusema kuwa umemfungua mwanga yeye pamoja na jamii inayomzunguka.

“Nimejifunza kwamba saratani ya mlango wa kizazi inaambukizwa kwa njia ya kujamiiana, hivyo nawaambia akina mama kwamba waendelee kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

“Hivyo, elimu hii inayotolewa imenisaidia kwani awali sikutambua kuwa mwanaume ni sehemu ya sababu ya kupata saratani ya mlango wa kizazi, hivyo tumepata elimu na tutaendelea kuchukua tahadhari ikiwamo kwenda kufanyiwa uchunguzi.

“Pia nawashauri wanawake wenzangu kupuuza uvumi ambao umekuwa ukienezwa kwamba kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kuna madhara hapana,” anasema Lyidia.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kemendo mkoani Kagera, anasisitiza kwa kuwakumbusha wanaume kuwa wawahimize wanawake kwenda kufanyiwa uchunguzi juu ya saratani ya mlango wa kizazi.

“Kwa kuwa sisi wanaume ndio tumekuwa chanzo cha saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake basi ni muhimu nasi kuchukua hatua muhimu ya kujilinda,” anasema Mwenyekiti huyo.

Zaidi ya wanachama 30 kutoka shirika la AMWAVU wamejengewa uwezo juu ya kuhamasisha wanawake kwenda kuchunguza saratani ya mlango wa kizazi mkoani Kagera.

Upande wake, Mratibu wa Programu za UKIMWI na Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uwezeshaji wa Wanawake, (UN-WOMEN), Jacob Kayombo, anasema kuwa kutokana na taarifa kutoka wizara ya afya na wadau wengine, wameona nibudi kutoa mchango katika eneo la saratani ya mlango wa kizazi kwa kina mama ikiwa kusaidia kufanikisha juhudi za serikali.

Takwimu zikoje?

Ikumbukwe kwamba kila ifikapo Februari 4, Tanzania imekuwa ikiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Saratani Duniani.

Takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (International Atomic Research on Cancer-IARC) na Shirika la Afya Duniani(WHO) za mwaka 2018 zinaonyesha kuwa kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1 na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki dunia kutokana na saratanikila mwaka.

Kiwango hicho ni sawa na asilimia 50. Aidha, zaidi ya watu milioni 43.8 wanaishi na saratani duniani.

Kama hiyo haitoshi, kwamujibu wa WHO asilimia tano ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi duniani unachangiwa na maambukizi ya UKIMWI.

Kama hiyo haitoshi, saratani ya mlango wa kizazi ni ugonjwa wanne uoatjiri zaidi wanawake, ambapo kwa mwaka 2018 pekee ilikadiriwa wanawake 570,000 walipatiwa matibabu huku 311,000 wakipoteza maisha kutokana na aina hiyo ya saratani.

Kwa hapa nchini takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa saratani ya ya mlango wa kizazi ni ugonjwa wa nne kushambulia watu zaidi.

Aidha, katika kila watu 100,000 basi 59.1 wameambukizwa saratani ya mlango wa kizazi, huku Mkoa wa Kagare ukionekana kuwa miongoni mwa maeneo ambayo ugonjwa huo unaongezeka zaidi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img