1.6 C
New York

Visual| Ugumu wa maisha unavyosukuma vijana kwenye janga la UKIMWI

Published:

Na Faraja Masinde, Gazetini

“Nilivyompigia simu akanitumia meseji akisema kuwa ‘Ushawahi kuona wapi mdomo uliooza ukatoa jino salama‘ nilimuuliza unamaanisha nini akaniambia wewe unamaradhi, nikamjibu kuwa nitatimiza ndoto zangu na nitafanya mambo mengi makubwa ambayo hutaamini,” anasema Consolata Mkomwa, kutoka Mtandao wa Vijana wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI (NYP+).

Unyanyapaa ni nini?

Kwa mujibu wa Mwongozi wa Kitaifa wa kuhusu kupunguza Unyanyapaa na Ubaguzi katika Program za Virusi Vya UKIMWI uliotolewa na Serikali Februari 2009, unautofasri unyanyapaa kuwa ni;

“Unyanyapaa unaohusishwa na Virusi Vya UKIMWI unaweza kuelezewa kama ni “mchakato wa kupunguza thamani” ya mtu ama akiwa anaishi na Virusi Vya UKIMWI ama anahusiana na Virusi Vya UKIMWI na UKIMWI.

“Unyanyapaa huu mara nyingi unaanzia katika misingi ya unyanyapaa kwenye ngono na utumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga sindano—ambazo ni njia kuu mbili kuu za kupata Virusi Vya UKIMWI. Ubaguzi hufuatia baada ya unyanyapaa na ni kutendewa visivyo sawa na kwa isivyostahili kwa mtu kutokana na hali halisi ama ya kudhaniwa juu ya hali yake ya uambukizo wa Virusi Vya UKIMWI.

“Ubaguzi unatokea wakati ambapo utofautishaji unafanyika dhidi ya mtu unaopelekea kutendewa visivyo sawa na isivyostahili kwa misingi ya kuwa miongoni au kuhisiwa kuwa miongoni mwa kundi fulani.” (UNAIDS:Jarida la maelezo halisi ya unyanyapaa na ubaguzi, Desemba 2003.

Aidha, kupitia mwongozo huo tunaelezwa kuwa Unyanyapaa na ubaguzi (unaoelezewa kama vitendo vinavyochukuliwa na watu ama taasisi kutokana na unyanyapaa) unaweza kujitokeza katika mlolongo wa manma nyingi zikiwemo: za kutengwa na kutoshirikishwa kijamii (m.f. kutengewa vyombo vya chakula, kutengwa wakati wa matukio ya kijamii) ikijumuisha kufanyiwa vurugu, maneno (m.f. kutetwa, kupachikwa majina ama kunyooshewa vidole).

“Kupoteza utambulisho na hadhi (m.f. kupoteza heshima katika familia na jamii); na taasisi (m.f. kufukuzwa kazi, nyumba au wateja). Unyanyapaa unaweza pia kuwepo kwa ndani na kuathiri jinsi watu wanavyofikiria juu yao wenyewe,” inaeleza tafsiri hiyo.

Ilikuwaje kwa Consolata

Simulizi ya Consolata inaanzia katika changamoto za maisha ya kila siku alizozipitia miaka kadhaa nyuma wakati akisaka elimu yake kwenye moja ya vitongoji vinavyounda Jiji la Mbeya akiishi na mama yake mzazi.

Kwa mujibu wa Consolata, wakati akiwa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Mwakibete miaka kadhaa nyuma kwenye moja ya shule zilizoko jijini Mbeya, ndipo alipokutana na ugumu wa maisha ambao mwisho wa siku ulimtumbukiza kwenye Virusi Vya UKIMWI.

“Njia yangu ya kusaka elimu haikuwa nyoofu tangu nikiwa shule ya msingi, kwani nyumbani tulikuwa tukikabiliwa na changamoto kadhaa katika kuhakikisha kuwa tunafanikisha maisha ya kila siku,” anasema Consolata.

Kwa maneno yake mwenyewe, Consolata anasema kuwa, hali ya maisha ilikuwa ngumu zaidi baada ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza, mazingira ambayo yalifanikisha kumshawishi kuanza ngono katika umri mdogo baada ya kuangukia mikononi mwa dereva wa Lori ambaye aliishia kumkimbia huku akimuachia ujauzito na UKIMWI juu.

“Nilivoanza kidato cha kwanza kwa kweli nyumbani kulikuwa na mazingira magumu kidogo ndipo nilipoanza kujihusisha na mahusiano. Nilipoanza uhusiano nilikutana na Kaka mmoja hivi ambaye alikuwa ni dereva wa lori aina ya Tipa…tukafanya mapenzi hadi nikapata ujauzito,” anasimulia Consolata huku akiwa mwenye kujiamini na aliyejaa matumaini tele.

Consolata anasema kuwa baada ya kunasa ujauzito huo ndio ilikuwa tiketi ya dereva huyo kuondoka kwenye viunga vya Mkoa wa Mbeya kwa kuhofia kuangukia kwenye mkono wa dola ambapo pasi na shaka angetupwa jela kwa kifungo kisichopungua miaka 30.

“Yule kaka baada ya kusikia kuwa mimi ni mjamzito akawa ameacha kazi na kuhama kabisa mkoa wa Mbeya, baadaye kuja kupima nikagundulika kuwa nilikuwa na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI,” anasema Consolata.

Sehemu hiyo ya simulizi ya Consolata ni kielelezo tosha kwamba Jamii bado inatumia udhaifu wa wasichana na ukosefu wa kipato kufanya ngono zembe ambazo zinasababisha maambukizi mbalimbali ikiwamo UKIMWI.

Sasa tuendelea na Consolata…

Haikuwa rahisi kujikubali

Anasema baada ya kukutwa na maambukizi hayo ya UKIMWI alikaa muda mrefu sana haki kuja kuikubali hali hiyo huku akijiona kama mtu wa tofauti kutokana na lugha za unyanyapaa zilizokuwa zikiendelea mtaani kwa watu wenye VVU.

“Kwa mara ya kwanza nilijiona mimi niwatofauti na wenzangu kwa ni kwa zile lugha za mitaani wakishakuona wanakwambia pale nyota imewaka, marehemu mtarajiwa, hata ukikaa na wenzio utasikia wanaambiwa mkuwa ‘hujui kwamba yule ni mgonjwa’.

“Lakini baadaye nilipoanza kupata elimu kutoka kwenye makundi ya uelimishaji rika nikawa najikuta niko vizuri naendelea kutumia dawa ARV (Dawa za kufubaza makali ya VVU) na hadi sasa naendelea vizuri,” anasema Consolata.

Hatima ya Ujauzito

Kukimbiwa na mwanaume aliyempa ujauzito pamoja na kukutwa na maambukizi ya VVU bado haikuwa shida kwa Consolata kushindwa kulea mimba yake na kujifungua.

Kwani Mwenyezi Mungu alimbariki watoto mapacha ambao hawakuwa na maambukizi, hata hivyo, mtoto mmoja ambaye ni Doto alifariki dunia miezi kadhaa baadaye.

“Nilifanikiwa kujifungua salama na Mungu alinibariki nikapata watoto mapacha, hata hivyo, kama tunavyojua kwamba aliyejuu ndiye mwenye uwezo wa kutoa na kutwaa, maisha ya Doto haya kuwa marefu kwani alifariki dunia hivyo nikawa nimebaki na mtoto mmoja ambaye ni Kulwa,” anasema Consolata.

Maisha na Dereva

Consolata anasema kuwa baada ya kujifungua salama aliamua kusahau madhira ya kukimbiwa na baba mtoto wake huyo na kuamua kumsaka tena kwenye namba yake ya simu kwa ajili ya kutaka kupata msaada wa malezi kwa mtoto wao huyo.

“Yule bwana ambaye nimezaa naye niliamua kuanza kumtafuta kwenye simu kwa ajili ya kutoa matumizi ya mtoto ushirikiano wake haukuwa mzuri.

“Siku ya kwanza alinitumia SMS akaniambia kuwa yuko ‘bize’ na kazi mara hana fedha na majibu mengine ya ovyo akisema hana fedha zikiwamo kejeli,” anasema Consolata huku akisisitiza kuwa kwa wakati ule hakuelewa sababu ni nini hadi kujibiwa vile.

…wewe unamaradhi…

Consolata anasema kuwa mara baada ya kuendelea kumsumbua mzazi mwenza huyo kwa ajili ya kuchangia sehemu ya gharama za malezi ndipo bwana huyo alipomnyanyapaa kwa kumweleza kuwa mdomo uliooza hauwezi kutoa jino zima.

“Kuna siku mtoto alikuwa anaumwa nikampigia simu lakini hakupokea badala yake akanitumia SMS anasema; ‘Ushawahi ona wapi mdomo uliooza ukitoa jino salama?’ nikamuuliza unamaanisha nini? akanijibu kuwa ‘wewe unamaradhi’ sikuchukia kwa kuwa tayari nilikuwa tayari nimepata elimu ya NYP+ ingekuwa kule mwanzo ningeumia.

“Namimi nikamjibu ‘namshukuru Mungu katika haya maradhi yangu niliyonayo naweza kukulelea mtoto wako na anaendelea kula na kulala vizuri, alafu mimi ndoto zangu hazijaishia hapa nitafanya mambo mengine mengi ambayo hutaamini, kama mtoto atakua na taendela kuishi vizuri’ hakunijibu hiyo meseji hadi leo,” anasema Consolata.

Hata hivyo, wakati ukitafakari kuhusu unyanyapaa huo aliokutana nao Consolata hebu mfikirie, Nwilanti Mwamwaja ambaye yeye anasema kuwa amekuwa akitumia dawa za ARV kwa miaka 16, na kwamba awali alitengewa vitu vyake ikiwamo sahani.

“Siyo hivyo tu, bali nilitengewa dodoki langu, sahani yakulia chakula, hivyo hata sahani ikiwa chafu nitaambiwa niitumie hivyo hivyo, nilikuwa napigwa mpaka utadhani kilimo cha mchicha kiko kwenye makalio yangu na nilikuwa nakamuliwa malimao kisha napigwa, lakini nashukuru kwamba kwa sasa nimeweza kupata sehemu sahihi ambapo nakaa vizuri,” anasema Mwamwaja kijana mwenye umri wa miaka 25 tu.

Vipi kuhusu shule

Consolata anasema kwa sasa wazo la kusema kwamba atarudi na kukaa darasani analiona ni zito kidogo badala yake anatamani kupata msaada wakuwezeshwa kuweza kupata elimu ya ufundi wa kushona nguo.

Wito

Consolata anasema kuwa anaifurahia hali yake hiyo na kutokana na elimu aliyoipata kwa sasa ana hata uwezo wa kumeza dawa akiwa ndani ya basi huku akiwasishi wanaoweka usiri.

“Hivyo nimepitia unyanyapaa wa aina tofauti kwani wapo waliowahi kuniita marehemu, na hata mimi nilikuwa najificha, lakini kwa sasa nimepata elimu ya kutosha kutoka NYP+ hivyo najiamini.

“Wito wangu kwa wanaotumia dawa kwa siri, kufanya hivyo kuna madhara kwako kwani unaweza kukutana na mpezi au mwezi na uspomwambia unaweza kumuambukiza VVU jambo ambalo ni dhambi hata mbele za Mungu, hivyo kwa hiyo mimi kwa sasa niko huru na naweza kumuelimisha mtu yeyote, jambo la msingi vijana tujitambue, walioko shule wazingatie masomo,” anasema Consolata.

Hata hivyo, tunatambua kwamba simulizi ya Consolata ni moja ya mifano michache tu ya ina ya maisha wanayokutana nayo vijana wa kitanzania.

Kauli ya Serikali kuhusu Unyanyapaa

Desemba Mosi (2021) akihutubia katika kwenye Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo Kitaifa yalifanyika katika Uwanja wa Ruanda-Nzovwe mkoani Mbeya yakiwa na Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Zingatia Usawa. Tokomeza UKIMWI. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimuwakilish Rais Samia Suluhu Hassan aliaziagiza mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuwanyanyapaa na kuwabagua Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kwa kuwa vitendo, kauli au mitazamo ya unyanyapaa na ubaguzi kwa kundi hilo havikubaliki.

“Kumekuwa na madai kuwa watumishi wa afya wana tabia za unyanyapaa na kuvujisha siri za WAVIU wanapotoa huduma katika vituo vyetu vya tiba na matunzo kwa WAVIU. Vitendo na tabia hizi ziripotiwe mara moja pindi vitakapotokea,” aliagiza Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema nchi ina sheria ya UKIMWI ambayo imefanyiwa marekebisho kadhaa ili kuhakikisha kuwa huduma za VVU na UKIMWI zinamfikia kila mlengwa. “Ninaelewa kuwa unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU bado ni changamoto kubwa katika jamii zetu.

“Hii inatukwaza na kurudisha nyuma juhudi za mwitikio wa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini. Mfano baadhi ya watu wanaoishi na VVU wanaona aibu kutumia huduma za VVU na UKIMWI zilizopo kwa sababu ya unyanyapaa na ubaguzi, hasa katika maeneo ya vijijini,” alisema Majaliwa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img