Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Saratani ni mabadiliko ya ukuaji wa seli au chembechembe hai na yaweza tokea sehemu yoyote ya mwili (seli hukua na kuongezeka idadi kwa haraka sana).
Aidha, kuna aina nyingi ya za saratani ikiwamo ile ya mlango wa kizazi ambapo tafsiri ya Wizara hiyo inasema kuwa Saratani ya mlango wa kizazi (cervix) ni mabadiliko ya ukuaji wa seli za mlango wa kizazi.
Kwa mujibu wa wataalamu, aina hii ya saratani inaweza kusambaa na kuweza kushambulia kibofu cha mkojo, uke na sehemu ya chini ya utumbo mkubwa na baadaye figo, ini na sehemu zingine za mwili na kusababisha kifo.
Huku kwa Tanzania ndiyo saratani inayoongoza kusababisha vifo kwa wanawake wengi ambapo asilimia 70 huripoti wakiwa wamechelewa sana.
Visababishi vyake
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, miongoni mwa visababishi vya saratani hiyo ni kuanza kujamiana katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuwa na ndoa za mitala, kuzaa watoto wengi na uvutaji sigara.
Dalili za Saratani
Dalili za saratani ya mlango wa kizazi ni pamoja na kutokwa damu bila mpangilio au kutokwa damu baada ya kujamiana kwa wanawake, maumivu ya mgongo, miguu na au kiuno, kuchoka, kupungua uzito na kupungikiwa hamu ya kula.
Dalili nyongine ni kutokwa na uchafu kwenye uke wa majimaji, uliopauka wa rangi kahawia au wenye damu na kuvimba mguu mmoja huku dalili mbaya zaidi zinazoweza kujitokeza zikiwa ni kuishiwa damu, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na fistula, na uvimbe wa tezi.
Kinga
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kinga ya awali ni pamoja nakupata chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV vaccine), kubadili tabia, kuepuka ngono katika umri mdogo, kuepuka uvutaji wa sigara ikiwemo pia kuepuka kubeba mimba katika umri mdogo na kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu.
Hata hivyo changamoto ni kwamba siyo wanawake wote wenye uwezo wa kuelewa dalili hizo na namna ya kujikinga na saratani hii ya mlango wa kizazi.
Hii ni kutokana pengine na ukosefu wa elimu, uzembe, changamoto za kifedha na sababu nyingine na hivyo kujikuta kwamba taifa likipoteza watu wengi kila mwaka sababu ya saratani hii ya mlango wa kizazi.
Changamoto hiyo ndiyo inaisukuma Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Akina Mama Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi mkoani Kagera (AMWAVU) chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Uwezeshaji wa Wanawake (UN-WOMEN) kuja na mradi wa kuhamasisha wanawake wanaoishi na virusi vya ukiwmi (WVVU) kupima saratani ya mlango wa kizazi na kupata matibabu stahiki mapema katika mkoa wa Kagera.
Zaidi angalia infographic yetu kuhusu saratani ya mlango wa kizazi.