1.4 C
New York

Visual| Uchumi wa Buluu; Maajabu ya bahari kiuchumi

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

TAFITI zimebaini kuwa asilimia 71 ya uso wa dunia ni maji na asilimia 97 ya maji hayo ni bahari. Ikimaanisha, eneo la nchi kavu ni asilimia 29 tu ya uso wa dunia. Hiyo inamaanisha nini?

Kama bahari itatumika ipasavyo, basi kuna uwezekano wa uchumi wa dunia kutotegemea kwa kiasi kikubwa rasilimali zilizoko nchi kavu. Kama ambavyo imekuwa ikionekana, matumizi ya bahari yamekuwa na tija na mchango mkubwa kwenye uchumi wa mataifa mbalimbali duniani kote.

Mathalan, unaweza kuona namna shughuli za uvuvi, uchimbaji mafuta, utalii na uchukuzi na usafirishaji zinavyoiingizia fedha za kigeni Tanzania, achana na kuwa chazo kizuri cha ajira.

Kwa kudokeza tu, zipo tafiti za kuaminika zinazoeleza kuwa shughuli zihusianzo na bahari huchangia takribani Dola za Marekani Trilioni 2.5 katika uchumi wa dunia. Katika kuhusianisha bahari na maendeleo ya kiuchumi, ndipo inapoibuka dhana ya Uchumi wa Buluu. Ni kitu gani hicho?

Uchumi wa Buluu ni nini, ulitokea wapi?

Kwa ufupi, unaweza kuutafsiri Uchumi wa Buluu kuwa ni matumizi ya maeneo ya bahari kwa ajili ya faida za kiuchumi. Kwamba lengo ni kuhakikisha kunakuwapo na uwanja mpana wa uelewa wa watu juu ya fursa lukuki zinazopatikana kupitia bahari na vyanzo vingine vya maji (mito na maziwa).

Dhana hiyo iliibuliwa kwenye Kongamano la Umoja wa Mtaifa (UN) la mwaka 2012 huko Rio De Janeiro, Brazil, ambako nchi wanachama zilikutana kujadili Uchumi wa Kijani.

Zikiwa kwenye Kongamano hilo, nchi zinazofaidika na bahari ziliibua hoja, kwamba utajiri huo uzungumziwe, kama si kuwekwa kuambatanishwa na Uchumi wa Kijani kwa maendeleo endelevu.

Bahari inavyopiga bao usafirishaji

Tafiti zinaonesha takribani asilimia 80 ya mizigo na biashara duniani husafirishwa kwa njia ya maji, kwamba usafirishaji kwa njia ya ardhi na anga hutumika kwa asilimia 20 pekee.

Katika hilo, utafiti wa mwaka 2015 ulionesha kuna meli za kibiashara zipatazo 68,723 zinazofanya kazi kimataifa. Pia, bandari kubwa duniani zinapakia na kupakua hadi tani milioni 744 za shehena kwa mwaka.

Mfano wa bidhaa zinazosafirishwa sehemu mbalimbali duniani ni nafaka, vyombo vya usafiri (magari, pikipiki n.k), mitambo, mafuta, gesi na kemikali.

Fursa za wavuvi

Kama hufahamu, watu zaidi ya bilioni moja duniani kote hutegemea samaki kuwa chanzo kikuu cha protini, virutubisho vya kujenga mwili. Ripoti ya FAO inaonesha kuwa uzalishaji wa samaki ulimwenguni ulifikia jumla ya tani milioni 175 mwaka 2018. FAO walifafanua kuwa tani milioni 156 zilitumika kwa chakula (chanzo cha protini), huku zilizobaki zikielekezwa kwenye utengenezaji wa mafuta na matumizi mengine.

Aidha, FAO walieleza namna uchumi wa dunia ulivyojiingizia Dola bilioni 401 kutokana na mauzo ya samaki, huku mahitaji yakitabiriwa kuongezeka zaidi.

Uchumi wa Buluu na utalii

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2018, shughuli za meli za kitalii ziliingiza Dola bilioni 150 katika uchumi wa dunia. Zipo meli za kitalii zinazoweza kubeba hadi watalii 8,000 kwa pamoja. Kuona ni kwa namna gani utalii wa bahari umekuwa na tija kiuchumi, nchi za Umoja wa Ulaya (EU) ziliingiza Euro bilioni 183 kwa mwaka 2011 pekee.

Ajira zinavyochomoza Uchumi wa Buluu

Katika soko la ajira duniani, kazi zinazotegema bahari, mathalan wahudumu wa hoteli za kitalii, zimetoa ajira kwa watu zaidi ya milioni 31 duniani kote. Kuziweka sawa takwimu hizo, meli moja ya kitalii huweza kuwa na wafanyakazi hadi 2,000.

Huku mabaharia wanaofanya kazi katika meli za kibiashara wakitajwa kufikia milioni 1.6, bado kuna uhaba wa wengine 67,500.

Vipodozi, tiba ‘dili’ jipya

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameibua fursa ya utengenezaji wa vipodozi na tiba zitokanazo na viumbe vya baharini. Kufikia mwaka 2011, kulikuwa na dawa zaidi ya 36 zilizotengenezwa kwa rasilimali zitokazo humo.

Hata hivyo, takwimu zinaonesha wazi kwamba mahitaji ya soko la dunia yamefikia Dola bilioni 4.6 na yanatarajiwa kuongezeka mara dufu.

Tanzania na Uchumi wa Buluu

Taifa hili limepakana na Bahari ya Hindi kwa umbali wa kilometa 1424. Mikoa iliyo karibu zaidi na bahari hiyo ni mitano; Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara. Aidha, bandari kubwa nne zilizoko Bahari ya Hindi ni Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na Malindi.

Ikumbukwe kuwa Bandari za Tanzania zinazihudumia nchi za Zambia, Burundi, Uganda, Rwanda, DRC na Malawi.

Jumla ya tani milioni 16.2 ya shehena za mizigo ilihudumiwa katika bandari za mwambao na bandari za maziwa makuu kwa mwaka 2017-2018.

Juu ya namna Tanzania inavyonufaika na soko la ajira kwenye Uchumi wa Buluu, takwimu zinaonesha kuwa baharia wa Kitanzania aliyeajiriwa huko ng’ambo huliingizia Taifa kiasi cha Dola milioni 27.6 kila mwaka.

Vilevile, utalii una nafasi kubwa Tanzania kutokana na uwapo wa maeneo kama Zanzibar, Kilwa, Mafia na Pangani ambayo ni vivutio vya baharini vinavyotoa fursa kwa wananchi kunufaika kiuchumi.

Mwisho, bado nchi za Mauritius, Visiwa vya Shelisheli na Afrika Kusini zimeendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi zingine Afrika kwa namna zilivyowekeza vilivyo kwenye Uchumi wa Buluu.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img