1.6 C
New York

Visualization| Kwanini Ronaldo ameondoka Juve, ametua Man United?

Published:

BAADA ya maneno kuwa mengi juu ya hatima yake katika klabu ya Juventus, hatimaye staa wa soka, Cristiano Ronaldo (36), akamaliza utata kwa kurejea Manchester United kwa mkataba wa miaka miwili.

Hatua ya kutua Old Trafford imeshitua wengi kwani taarifa za kuhusishwa na Manchester City ndizo zilizokuwa zimesambaa mitandaoni. Awali, ilisemekana kulikuwa na mazungumzo yanaendelea kati ya wakala wa Mreno huyo na mabosi wa Man City.

Taarifa zinadai Man United waliwazidi kete majirani zao hao wa jijini Manchester wakitumia Pauni 21.3.

Alichokifanya Juventus

Juventus hawawezi kujutia Pauni milioni 105 walizotumia kumsajili Ronaldo mwaka 2018 na kumpa mkataba wa miaka minne. Kwa misimu mitatu aliyokaa klabuni hapo, mshindi huyo mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or amefunga mabao 101 na kutoa ‘asisti’ 22 katika mechi 134 alizocheza.

Hata hivyo, kwa kuwa amebakiza miezi 12 katika mkataba wake, ni wazi Juventus wako makini kuona wanapata mkwanja endapo atalazimisha kuondoka kipindi hiki.

Ni kwa sababu hawataambulia chochote endapo atatimka wakati wa usajili wa kiangazi, mwakani, kwani tayari atakuwa amemaliza mkataba wake na kuwa mchezaji huru.

Kwanini ameondoka?

Huenda sababu zipo nyingi lakini kubwa ni kwamba Ronaldo haoni jipya kwenye soka la Italia kwani ameshafanikisha kila alichokitaka. Akiwa Juventus, ametwaa mara mbili taji la Ligi Kuu (Serie A), moja la Supercup na jingine la Coppa Italia.

Kwamba kwa misimu mitatu, nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno ameshabeba vikombe vinne, pia akinyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa Serie A (Paolo Rossi Award).

Mwisho, Ronaldo ni mchezaji mwenye kiu ya mataji, hasa Ligi ya Mabingwa, lakini haioni Juventus ikiwa hivyo. Ronaldo akiitazama Juventus, bado haioni kwenye ukubwa wa Chelsea, Man City, PSG na Bayern Munich, hasa linapokuja suala la kuwania ‘ndoo’ ya Ligi ya Mabingwa.

Mshahara wake Old Trafford

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini England, Ronaldo ndiye atakayekuwa mchezaji anayelipwa mshahara mnono zaidi Man United kwani atakunja Pauni 480,000 (zaidi ya Sh bil 1.5 za Tanzania) kwa wiki.

Kile kinachoweza kuakisi mapenzi yake makubwa kwa Man United, Ronaldo ameshusha mshahara wake kwani alipokuwa Juventus alikuwa akivuna Pauni 1,000,000 (zaidi ya Sh bil 3 za Tanzania) kwa wiki.

Hata hivyo, mshahara wake mpya Man United unakwenda kumwacha mbali kipa David de Gea, ambaye kabla ya usajili wa Ronaldo ndiye aliyekuwa akipokea mshahara mnono zaidi Old Trafford, Pauni 375,000 (zaidi ya Sh bil 1.1 za Tanzania) kwa wiki.

CR7 ametokea wapi?

Jina lake kwenye soka la Ulaya lilianza kuibuka mwaka 2003, alipotua Manchester United akitokea Sporting CP, enzi hizo akiwa na umri wa miaka 18. Mashetani Wekundu walitumia Pauni milioni 12.24, hivyo kuweka rekodi ya kuwa kinda wa bei mbaya zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu ya England.

Akiwa Old Trafford, alitwaa mataji saba (Ligi Kuu (3), Ligi ya Mabingwa, FA, na Kombe la Ligi (2). Vilevile, alitwaa tuzo yake ya kwanza ya Ballon d’Or, bila kusahau kwamba alifunga jumla ya mabao 118 katika mechi 292.

Ilipofika mwaka 2009, mkali huyo alitimkia Real Madrid kwa ada iliyovunja rekodi ya usajili duniani, Pauni milioni 80. Aliitumikia Madrid misimu tisa, ambapo aliipa mataji nane (Ligi ya Mabingwa (4), La Liga (2) na Copa del Rey (2) akifunga jumla ya mabao 451 katika mechi 438.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img