TUNAWEZA kukubaliana kuwa matukio ya wapendwa wetu kujiua yamekuwa yakiacha simanzi kubwa kwenye jamii, labda kuliko hata vifo vingine vya ghafla.
Ni changamoto ya maisha, migogoro ya ndoa, au matatizo ya akili? Tafiti mbalimbali zimekuwa zikiyataja hayo kuwa yanachangia kwa kiasi kikubwa hatua ya mtu kufikia kujitoa uhai.
Katika utafiti wake wa hivi karibuni, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) lilibaini kuwa kila mwaka dunia hupoteza watu takribani 800,000 kutokana na matukio ya kujiua.
Huenda ikaonekana ni wachache ukilinganisha na idadi ya watu duniani, lakini inashitua zaidi kuona ni wastani wa mtu mmoja kujiua kila baada ya sekunde 40.
Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha vifo 10 kati ya 100,000 viliyokana na matukio ya kujiua. Aidha, asilimia 79 ya matukio ya kujiua kote duniani yalitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, huku nchi za kipato cha juu zilikuwa na viwango vya juu kwa watu 11.5 kati ya watu 100,000.
Ni kwa utafiti huo, sasa kujiua kunatajwa kuwa sababu ya pili ya vifo vinavyotokea duniani kila mwaka.
Hata hivyo, kile kinachoonekana kushitua zaidi, ni nchi 38 pekee duniani ndizo zenye mikakati ya kukabiliana, kama si kumaliza, janga hilo la watu kujiua.
Ni nani kati ya wanawake na wanaume hujiua zaidi?
Ripoti ya WHO pia imeendelea kueleza kuwa kwa viwango vya wastani vya kujiua ulimwenguni kwa mwaka 2016 visa vya kujiua kwa wanaume wa nchi zilizoendelea ilikuwa ni mara tatu ya wanawake katika nchi hizo, huku ikiwa tofauti katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambapo viwango vya visa kati ya wanawake na wanaume vinalingana.
Kujiua kulikuwa sababu ya pili baada ya ajali za barabarani inayosababisha vifo miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 29. Miongoni mwa barubaru wa umri wa miaka 15 hadi 19, kujiua ilikuwa sababu ya pili ya vifo miongoni mwa wasichana ikitanguliwa na sababu za vifo zinazosababishwa na masuala ya ujauzito, na sababu ya tatu inayosababisha vifo miongoni mwa wavulana baada ya ajali za barabarani na ugomvi miongoni mwao.
Sababu za watu kujiua
Katika utafiti wake, WHO iliibua sababu kuu nne za watu wakujitoa uhai. Kwa mujibu wa ripoti, wapo ambao hujiua kutokana na wivu wa mapenzi. Wengine hukatisha uhai wao baada ya kuvurugwa na migogoro ya familia zao.
Aidha, wapo sababu ya matatizo sehemu za kazi (mathalan mishahara kuchelewa) nayo si ya kupuuzwa. Vilevile, ugumu wa maisha umekuwa moja ya sababu za watu kujiua.
Nini kifanyike?
Njia ambayo imezoeleka zaidi kwa watu kujitoa uhai ni kujinyong’a, kunywa sumu ya kuulia wadudu na matumizi ya silaha. Njia ambazo zimeonesha kusaidia kupunguza visa vya kujiua ni pamoja na kuzuia kuweza kufikia vitu vya kutumia kujiua, kuelimisha vyombo vya habari kuhusu namna ya kuripoti matukio ya kujiua, kufanya programu miongoni mwa vijana katika kujenga stadi zinazowawezesha kukabiliana na msongo wa mawazo katika maisha, utambuzi wa mapema, pia jinsi ya kuwafuatilia watu walioko hatarini kujiua.
Ripoti ya WHO iliyotolewa hii leo pia imeonesha kuwa udhibiti wa manunuzi ya sumu za kuulia wadudu unasaidia sana kupunguza uwezekanoi wa watu kujiua ikitolewa mifano ya nchi kama Sri Lanka ambako visa vya kujiua vilishuka kwa asilimia 70 na inakadiriwa maisha ya watu 93,000 waliokolewa kati ya mwaka 1995 na 2015.