1.4 C
New York

Ripoti| Utatuzi migogoro changamoto maeneo ya kazi

Published:

RIPOTI ya mwaka huu ya Haki za Binadamu na Biashara imebainisha kuwa bado hakuna mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kampuni, hasa kwenye maeneo ya kazi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki Binadamu (LHRC), ni asilimia 53 pekee ya kampuni 160 ndizo zilizokuwa na mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kazi.

Ripoti hiyo imefafanua kuwa baadhi ya wafanyakazi waliohojiwa walilalamika kuhusu kutokuwapo mifumo ya utatuzi wa migogoro katika ngazi ya kampuni.

“Ni 53% pekee ya kampuni zilidai kuwa na mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kazi, sababu kuu za migogoro katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni pamoja na kukataliwa/kunyimwa likizo na kutolipwa baada ya kufanya kazi muda wa ziada.

“Pia, kutowasilisha michango ya hifadhi ya jamii, kucheleweshewa mishahara, kuchelewesha malipo ya fedha za kujikimu wakati wa safari (hasa kwa madereva wa mabasi na malori), kukiuka mkataba, makato ya mishahara, kufanya kazi zaidi ya muda wa juu wa kufanya kazi, na likizo bila malipo,” imeeleza ripoti hiyo.

Aidha, imeendelea kufafanua kuwa migogoro ya kazi iliyosajiliwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) iliongezeka kutoka 14,777 mwaka 2018/19 hadi 16,269 mwaka 2019/20, huku kampuni tano kati ya 10 zina mifumo ya utatuzi.

“Utafiti uligundua kwamba Janga la Corona lilichangia kuongezeka kwa migogoro kwa kuwa waajiri walichukua hatua mbalimbali kukabiliana na hasara iliyosababishwa na janga hilo, ikiwemo kushuka kwa uzalishaji, faida, na uhitaji wa bidhaa na huduma.

“Migogoro mingi ya kazi iliyosajiliwa na CMA kwa kipindi cha 2018/19 na 2019/20 iliwahusisha wafanyakazi katika sekta za usafirishaji, ulinzi binafsi na ukarimu.  Migogoro mingi ya kazi iliyosajiliwa na CMA katika miaka ya 2018/19 (38.5%) na 2019/20 (39.5%) ilihusu mwisho au usitishaji wa ajira,” imeeleza ripoti hiyo ya LHRC.

Wakati ripoti hiyo ikibainisha hayo, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 na Sheria ya Taasisi za Kazi, pia ya mwaka 2004, zilianzisha na kutambua mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kazi, hususani Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na Kitengo cha Kazi cha Mahakama Kuu.

Vilevile, ukiacha mifumo hiyo ya utatuzi wa migogoro ya kazi, ambayo ni ya Serikali, kuna mifumo isiyo ya kiserikali ya utatuzi wa migogoro hiyo, ikiwemo katika ngazi ya kampuni.

UELEWA KUHUSU SHERIA ZA KAZI, HAKI NA WAJIBU

Kwa upande wa uelewa kuhusu sheria za kazi, haki na wajibu, mambo makubwa yaliyoibuliwa ni:  

Kama ilivyokuwa katika utafiti uliopita, wafanyakazi saba kati ya 10 (73%) hawakuwa na uelewa kuhusu sheria na kanuni za kazi. Ni 12% pekee ya wafanyakazi walisema wana uelewa kuhusu sheria na kanuni hizo, ikiwemo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.

Mkoa wa Tabora uliongoza kwa kuwa na asilimia kubwa zaidi ya wafanyakazi wasio na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni za k azi (92%). Mikoa mingine (70% kwenda juu) ni pamoja na Mbeya (83%), Shinyanga (82%), Mara (81%), Tanga (78%), Dodoma (76%), Singida (73%), Mtwara (72%)

Kuhusu uelewa juu ya haki za msingi za mfanyakazi, zaidi ya nusu ya wafanyakazi (52%) walidai kwamba wana uelewa kuhusu haki hizo, huku 39% wakisema hawana uelewa, na 9% wakisema wana uelewa kidogo.

Katika utafiti uliopita, 58% ya wafanyakazi walidai kuwa na uelewa kuhusu haki zao, hivyo ukilingalisha na utafiti huu ni punguzo la 6%.

Miongoni mwa wafanyakazi waliodai kuwa na uelewa kuhusu haki zao (52%), ni 15% pekee waliweza kutaja angalau haki tatu kwa ufasaha, sawa na ongezeko la 2% ukilinganisha na utafiti uliopita. Pia, 58% kati yao waliweza kutaja haki mbili kwa ufasaha.

Wakati sheria ikiwataka waajiri kuweka waraka wa haki za binadamu katika sehemu ambayo wafanyakazi wote watauona vizuri mahala pa kazi, ni 16% ya waajiri waliotembelewa (kampuni) walisema wamefanya hivyo.

Waajiri pia waliulizwa kama wanazijua Kanuni za Umoja wa Mataifa za Biashara na Haki za Binadamu za mwaka 2011. Ni 11% ya waajiri walidai kuzijua Kanuni hizo, sawa na ongezeko la 5% ukilinganisha na utafiti wa mwaka 2019.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img