8.7 C
New York

Chati|Sekta ya Utalii ilivyochanua 2015-2021

Published:

AMA hakika utalii ni sekta nyeti nchini, kama ilivyo kwa madini, kilimo, na nyinginezo zinazotegemewa kuchangia pato la Taifa. Ndiyo, sekta ya utalii huchangia hadi zaidi ya asilimia 10 ya pato la Taifa na ndiyo maana haishangazi kuona ikipewa kipaumbele.

Kwa miaka mitano ya hivi karibuni (2015-2021), sekta ya utalii nchini imeonekana kuwa kwenye kiwango chake kizuri, pongezi kwa Wizara husika (Wizara ya Maliasili na Utalii) kwa mikakati ya kila uchwao. Ndiyo, ndani ya kipindi kifupi hicho, sekta ya utalii ilipokea jumla ya watalii 7,615,551.

Iko hivi; takwimu za mwaka 2015 zinaonesha wazi kuwa jumla ya watalii 1,137,182 waliziacha nchi zao na kuingia Tanzania kutembelea vivutio mbalimbali.

Mwaka uliofuata, kwa maana ya 2016, sekta ya utalii iliendelea kufanya vizuri kwani idadi hiyo iliongezeka mara dufu na kuishuhudia Tanzania ikipokea watalii 1,284,279.  Hali ilikuwa nzuri pia mwaka 2017, ambapo watalii 1,327,143 waliingizia kipato sekta ya utalii.

Aidha, kwa mwaka 2018, sekta ya utalii ilizidi kuchanua kwani kuliwa na watalii 1,505,702, idadi ambayo haikutofautiana kwa kiwango kikubwa na ile ya mwaka 2019 (1,510,151).

Hata hivyo, mwaka 2020 haukuwa mzuri kwenye sekta ya utalii, kama ilivyo kwa mwaka huu, yote hiyo ikisababishwa na janga la Corona lililosababisha watalii wengi kubaki kwenye nchi zao kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Mwaka 2020, sekta hii ilipokea watalii 620,867. Kwa mwaka huu, takwimu zilizokomea Machi zinaonesha ni watalii 230,227 waliokuwa wametembelea vivutio lukuki vilivyomo nchini.

Mwisho, unapozungumzia siri ya sekta ya utalii nchini kuchanua, kuna matatu utalazimika kuyagusa kwa namna moja au nyingine. Mosi, ni utitiri wa vivutio, kuanzia hifadhi hadi Mlima wa Kilimanjaro.

Pili, pasi na kukwepa, utagusia tunu ya amani inayowafanya watalii wasihofie kuja nchini, wakiamini watakuwa usalama kwa kipindi chote cha safari yao kwenye vivutio.

Mwisho, ni sera za Serikali juu ya utalii na mikakati imara inayozalishwa kila uchwao, pongezi zikipaswa kwenda kwa wizara husika; Wizara ya Maliasili na Utalii.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img