MICHUANO ya Olimpiki inaendelea huko Tokyo, Japan, huku ikitarajiwa kufikia ukomo wake Agosti 8, mwaka huu. Ikumbukwe ni mashindano yaliyopaswa kufanyika mwaka jana lakini janga la Corona likasababisha ipigwe kalenda.
Hata hivyo, wakati wanamichezo wakiendelea kuzipa heshima nchi zao kwa kunyakua medali, ‘ishu’ ya baadhi yao kutumia dawa za kuongeza nguvu imeonekana kuchukua sura yake.
Hivi karibuni, mwanariadha wa Nigeria, Blessing Okagbare, alipigwa aliondoshwa kwenye michuano hiyo baada ya kukutwa ametumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni, tena akifanya hivyo saa chache kabla ya kuingia mbio za meta 100 za hatua ya nusu fainali kwa upande wa wanawake.
Okagbare mwenye umri wa miaka 32, alibeba medali ya fedha katika michuano ya Olimpiki ya mwaka 2008, pia akitwaa medali ya aina hiyo na ile ya shaba aliposhiriki mashindano ya Dunia miaka mitano baadaye.
Hata kabla ya michuano kuanza mwezi uliopita, zaidi ya wanamichezo 20 walishakumbana na adhabu ya kuondoshwa Olimpiki aidha kwa kubainika kutumia dawa zisizoruhusiwa michezoni au kushindwa kufuata taratibu za vipimo zilizowekwa.
Nigeria hoi Olimpiki 2021
Kati ya hao zaidi ya 20 waliosukumwa nje ya mashindano ya mwaka huu, 10 ni Wanigeria, watatu wanatokea Ukraine na Belarus, wawili ni wanamichezo wa Morocco na Ethiopia. Awali, wanamichezo wawili wa Kenya walishaondoshwa lakini ilikuwa mapema, hivyo nafasi zao zikajazwa.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999, Shirika la Kukabiliana na Dawa zilizokatwa Michezoni (WADA) limekuwa likipambana na wanamichezo ‘wanaojiongeza’ kwa mtindo huo.
Kilichowakuta Urusi
Katika kutangaza onyo kali, mwaka juzi WADA ilitaka bendera ya Urusi kutopepea kwenye michuano ya Olimpiki kwa miaka minne, adhabu iliyopungua hadi miaka miwili na sasa itafikia ukomo hapo mwakani.
Hatua ya WADA ilikuja baada ya wanamichezo wa Urusi kuwa ndiyo nchi iliyozoa medali nyingi zaidi (30) kwenye michuano ya Olimpiki ya mwaka 2019.
Hadi Urusi inashukiwa na rungu hilo la WADA, ilishanyakua medali za dhahabu 149, fedha 125, na shaba 152.
Si kwamba Urusi haitapeleka wanamichezo, bali kama ilivyo kwenye Olimpiki ya mwaka huu, hawatavaa mavazi ya kuiwakilisha nchi na watakosa haki ya kupigiwa wimbo wa taifa lao.
Tabia hii ilianzia wapi?
Utamaduni wa wanamichezo kutumia dawa za kuongeza nguvu ulianzia kwenye michuano ya Olimpiki ya mwaka 1904 baada ya mwanariadha Thomas Hicks kukiri kutumia dawa aina ya Strychnine na Brandy.
Baada ya huyo, hapo ndipo lilipoibuka kundi kubwa la wanamichezo wanaotumia dawa za kuongeza nguvu, akiwamo Hans-Gunnar Liljenwall, kwa nia ya kupandisha viwango wakati wa mashindano.
Mwishoni mwa miaka ya 1990, ndipo Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) ilipokuja na wazo la kuanzisha WADA.