1.6 C
New York

Infographic| Tanzania inavyopambana kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI 2030

Published:

NA FARAJA MASINDE

MALENGO ya Dunia ni kuhakikisha kuwa janga la Virusi vya UKIMWI linabaki kuwa historia ifikapo 2030.

Tanzania nayo kama mwananchama wa Umoja wa Mataifa ni miongoni mwa nchi zinazotamani kuona ndoto hiyo ikitimia.

Katika kulifanikisha hilo jitihada mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na nchi kupitia mamlaka inayoshughulikia Ukimwi ambayo ni Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS).

Hatua hizo za kimkakati ni pamoja na kutoa elimu ikiwamo kuwajengea uwezo maofisa Maendeleo ya jamii nchini na wadau wengine muhimu wakiwemo taasisi na kundi la Waandishi wa Habari.

Hali ya Ukimwi nchini

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na TACAIDS kupitia ripoti yake iliyoangazia HALI YA VVU NA UKIMWI DUNIANI NA NCHINI hadi kufikia Desemba 2019 ilikadiliwa kuwa jumla ya watu 1,705,301 walikuwa wakiishi na virusi vya Ukimwi nchini Tanzania.

Aidha, kati ya hao, ilikadiliwa kuwa watu wazima (miaka 15 na zaidi) walikuwa takribani 1,612,301. Wanawake wakiwa 983,471, Wanaume 628,830 na watoto chini ya miaka 15 ilikuwa 93,000.

Maambukizi ya VVU 2019

Ripoti hiyo ya TACAIDS inachambua juu ya maambukizi ya VVU kwa mwaka 2019 kuwa idadi ya watu wazima (miaka 15 na zaidi) ilikuwa takribani 68,484.

Kati ya hao wanawake ni 39,614 na wanaume ni 28,870. Aidha, watoto (chini ya miaka 15) 8,600, hivyo kufanya idadi yote kuwa 77,084.

Upande wa vifo vitokanavyo na Ukimwi nchini kwa mwaka 2019 pekee vilikuwa 27,429 ambapo kati ya hivyo watu wazima miaka 15 na zaidi 21,529.

Kati ya hao wanaume 12,225 na wanawake 9,304 huku watoto chini ya miaka 15 wakiwa 5,900.

Akichambua ripoti ya utafiti uliofanyika juu ya maambukizi ya VVU Tanzania (Tanzania HIV Impact Survey) 2016-2017

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Lucas Shija Kitula, anasema hali ya upimaji wa VVU nchini bado ni panda shuka na kwamba jitihada za makusudi za kutoa elimu zinahitajika.

Kwa mujibu wa Kitula, asilimia 29.2 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 na kuendelea hawajawahi kupima VVU huku kiwango kikiwa kikubwa zaidi kwa wanaume wenye umri sawa na huo ambao ni asilimia 40.8.

“Lakini pia tukija kwenye upande wa umri wa vijana ni miaka 15 hadi 19 hali ya upimaji nako bado siyo ya kuridhisha.

“Kwani wavulana ambao hawajawahi kupima VVU ni asilimia 79 huku upande wa wasichana wakiwa ni asilimia 61.4.

“Upande mwingine tunaona kuwa elimu imekuwa na msaada kwani takwimu zinaonyesha kuwa upimaji wa VVU kwa watu wenye elimu ya chuo kikuu ni asilimia 89.3 ikilinganishwa na asilimia 54.4 ya wale ambao hawajasoma,” anasema Kitula.

Wenye maambukizi

Kitula anaendelea kufafanua zaidi kuwa wanawake wanaoishi na VVU nchini wenye umri kati ya miaka 45 hadi 49 ni asilimia 12, huku upande wa wanume wenye umri wa miaka kati ya 40 hadi 44 ni asilimia 8.4.

“Ukiangalia upande wa Vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanaoishi na VVU ni asilimia 2.1 kwa wasichana na asilimia 0.6 kwa wavulana.

“Utaona kwamba kiwango cha maambukizi ya VVU kwa wanawake wenye umri kuanzia 15-39 ni mara mbili ya wanaume wenye miaka 15 hadi 39,” anasema Kitula.

Hii ni sawa na kusema kwamba katika kila kundi la wanawake wanne basi mmoja kati yao anaishi na maambukizi ya VVU.

Hali ya VVU duniani

Ripoti hiyo inabainisha kuwa watu wanaokadiriwa kuwa milioni 1.7 (milioni 1.2-2.2 milioni) ambao walipata VVU ulimwenguni mnamo 2019 walionyesha kupungua kwa asilimia 23 kwa maambukizo mapya ya VVU tangu 2010.

“Ulimwenguni, idadi ya kila mwaka ya maambukizo mapya imekuwa ikishuka kwa kasi zaidi kati ya wanawake na wasichana (kupungua kwa asilimia 27 tangu 2010) kuliko wanaume na wavulana ambao kasi ya kupungua ni asilimia 18.

“Kulikuwa na maambukizo mapya machache mwaka 2019 ulimwenguni kati ya wanawake na wasichana (asilimia 48 ya jumla ya maambukizo) kuliko wanaume na wavulana (asilimia 52).

Aidha, kwa mujibu wa Kitula, mwaka 2019 kulikuwa na maambukizo mapya machache ulimwenguni kati ya wanawake na wasichana ambayo ilikuwa asilimia 48 ikilinganishwa na wanaume ambayo ilikuwa asilimia 52.

Watoto wenye umri kati ya miaka 0 hadi 14 walichangia asilimia 9 ya maambukizo mapya mwaka 2019 huku asilimia 84 ya maambukizo ya watoto yakitokea Kusini na Mashariki mwa jangwa la Sahara.

Hii ni sawa na kusema kwamba kiudini mwa Jwanga la Sahala ndiko kuliko na changamoto zaidi ya maambukizi ya VVU ikilinganishwa na sehemu nyingine duniani.

Huduma za VVU nchini

“Asilimia 65.2 ya watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea waliripoti kuwa wamewahi kupima VVU ambapo kati yao (asilimia 59.2 ni wanaume na asilimia 70.8 ni wanawake).

“Kwa ujumla asilimia 31.3 ya watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea waliripoti kuwa wamepimwa VVU katika miezi kumi na mbili iliyopita kabla ya utafiti kufanyika ambapo asilimia 29 ni wanaume na asilimia 33.5 ni wanawake.

“Pia Asilimia 15.7 ya waliopima na kugundulika na VVU hawakuwahi kupima VVU kabla ya utafiti.

ambapo asilimia 19.7 ni wanaume na asilimia 13.7 ni wanawake,” anasema Kitula.

JUHUDI ZA TACAIDS

Judith Luande ni Mratibu wa Masuala ya Ukimwi kwa Mtazamoa wa Kijinsia kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) ambapo anafafanua kuwa katika kuhakikisha kuwa wanafikiandoto ya kumaliza VVU ifikapo 2030 jitihada za maksudi zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo makundi maalumu.

Makundi hayo ni Maofisa Jamii na Jinsia nchini ngazi ya Wizara na Mikoa na Halmashauri kwa ajili ya kujengeana uwezo utakaochochea mabadiliko katika mwitikio mzima wa Ukimwi kwa mtazamo wa kijinsia.

“Unajua tunapoongelea unyanyapaa, ubaguzi na lugha nyungine kama hizo hiyo yote inatokana na mtazamo hasi ambao upo katika jamii nah ii ni kutokana tu na watu kutokuwa na elimu.

“Hivyo Tacaids tumekuwa na mkakati wa kukutana na makundi haya maalumu yakiwamo ya wanahabari ambao watatoa taarifa sahihi zitakazoshawishi kuleta mabadiliko ndani ya jamii.

“Lengo ni kuona tunafikia asilimia 0 kwenye Vifo, maambukizi mapya na unyanyapaa,” anasema Judith.

UNYANYAPAA NI KIKWAZO

Jacob Kayombo ni Mratibu wa Programu zinazohusu masuala ya Ukimwi na Saratani kwa Wanawake katika Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanwake (UN WOMEN) ambaye anasema kuwa mwarobani wa kufikia ndoto ya 0 ifikapo 2030 ni kubadili mitazamo.

“Tunapenda kuona jamii ikibadilisha mtazamo wa kijamii kuhusu mila na desturi, kwani kwa muda mrefu unyanyapaa na mila hatarishi au zisizofaa vimekuwa vikiongelewa katika lugha ambayo tunadhani vinahusu watu waliko vijijini sana jambo ambalo siyo kweli.

“Kwani tumekuja kubaini kwamba mila hizi ambazo hazifai kama ukeketaji au ndoa za utotoni zipo kwenye maeneo mengi sana hata mijini na maeneo mengine ya mikoani yapo.

“Mfano tumeona masuala kama unyanyapaa ambayo kwa huko nyuma tulidhani kuwa yanatajwa kwenye maeneo machache sana ya VVU na Ukimwi lakini kumbe ni kinyume badala yake yanagusa watu wengi, yanaongelea sehemu pana na unaweza ukakuta mazingira ya kila kaya yapo na ndiyo maana tunasema kubadilisha mtazamo ni muhimu,” anasema Kayombo na kuongeza kuwa:

“Kama mwanzo tulikuwa tunaelewa unyanyapaa uko vipi au changamoto za mila na desturi ziko vipi na tukawa tumesahau mambo ambayo baada ya muda sasa yanajionesha sasa katika jamii zetu ni vizuri sasa tubadili mtazamo na kuona ni namna gani mambo haya yanatoa changamoto katika udhibi wa VVU katika mazingira ya leo na ya hapo baadae.

“Pia ni muhimu kuona ni mbinu gani ambazo zinakuwa ni stahiki kwa ajili ya kukabiliana na hizi changamoto ndio maana tumekuja na faslsafa ya kuona kwamba hizi changamoto ziondolewe kwa kusihirikisha jamii kwa kutumia mikakati ileile ambayo ipo kwenye maeneo husika ambazo zitatengenezwa na jamii yenyewe.

“Lakini pia suala jingine ni utandawazi ambao umeingilia masuala yale ambayo huko nyuma yalionekana ni ya kitamaduni hivyo kuna kizazi kipya ambachokimeingia, mfano sasahivi simu inaweza kusaidia kufikisha taarufa kueleza matendo yaleyale ambayo huko nyuma yalikuwa yakifanywa na watu, hivyo mambo kama haya ndiyo yanayotusukuma kubadili mtazamo wetu,” anasema Kayombo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img