1.6 C
New York

Infographic: Kulinda ndoa kunavyofifisha ndoto za Wasichana Kilosa

Published:

NA FARAJA MASINDE

“Ukifika kwenye eneo la ukatili wa kingono na ubakaji wanafunzi wanakuuliza…Madamu kwa mfano sasa ndio umebakwa umepata ujauzito, naweza nikarudi shule kusoma? Hili ni swali fulani linaloumiza sana ambalo tumekuwa tukikutana nalotunapokuwa tunatoa elimu kwa wasichana walioko shule.

“Lakini pia wengi wanapewa ujazito na baba zao wa kufikia huku mama akishuhudia, lakini anakana kutoa taarifa sababu ya kulinda ndoa,” anasema Tumaini Geugeu ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro nchini Tanzania.

Swali hilo tata analoulizwa Geugeu wakati anapokuwa anatoa elimu hiyo, ndilo lililoko kwenye kichwa cha Zamaradi Asna Mohammed binti wa miaka (17) ambaye hivi sasa haelewi ni upi mustakabari wake katika elimu.

Kwa sasa Zamaradi hayuko tena shule na hajui ni kwa namna gani atazifikia ndoto zake za kuwa miongoni mwa wanajeshi mahiri wa kike wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hapo baadaye.

Zamaradi anakiri kwamba siyo kwamba alibakwa la hasha! Bali yeye amejikuta kwenye njia panda hiyo kutokana na ugumu wa maisha aliyokuwa akiishi.

Binti huyu mwenye siha njema anayeishi ndoto yake kwa muonekano wake wa ukakamavu, alibainisha kuwa amejikuta akinasa katika mtego huo wa kupata ujauzito wakati akihangaika kusaka elimu yake ya sekondari katika shule ya Dendego iliyoko kaskazini mwa mji wa Kilosa.

ILIKUWAJE?

“…nililazimika kuacha shule Machi, mwaka huu nikiwa kidato cha nne baada ya kupimwa na kubainika kuwa nilikuwa na ujauzito wa miezi miwili, hivyo nikawa sina sifa tena za kuendelea na shule,” anasema Zamaradi.

Aidha, anaendelea kusema kuwa chanzo cha kukwaa ujauzito huo akiwa shule ni vishawishi kutoka kwa mwanaume aliyemlaghai kwa kupitia duka na njaa yake.

“Wanaume wanavishawishi vingi, kama unavyojua baba yangu (Asna Mohammed (74) anafanya kazi ya kuuza kuni ambazo anahangaika kuzisaka porini, na mara nyingi mauzo yake yalikuwa siyo zaidi ya Sh 2,500 mpaka 5,000 kwa siku.

“Sasa hapo ilikuwa ni changamoto kwangu mimi kuweza kufanikisha mahitaji yangu ya kila siku na kuhakikisha kuwa nazifikia ndoto zangu nikiwa na mahitaji muhimu,” anasema Zamaradi.

Zamaradi ambaye ni mtoto wa mwisho katika ya watoto wa tano wa Mzee Mohammed na mkewe Hadija Rashid (69), anasema kuwa muuza duka ndiye aliyemlaghai kwa kuanza kumpatia Sh 5,000 ya matumizi kila alipohitaji kwa ajili ya shule.

“…Kwanza alinitongoza nikakataa lakini baadaye alianza kunishawishi kwa kunipatia fedha Sh 5,000 ambayo wakati mwingine ndiyo ilitumika kununua chakula nyumbani, hivyo kulingana na hali mbaya ya nyumbani nilijikuta nimenasa kwenye mtego wake nikawa nimetembea naye mara moja na kupata ujauzito,” anasema Zamaradi.

MAISHA BAADA YA UJAUZITO

Zamaradi anasema baada ya kupata ujauzito huo na kisha kufukuzwa shule, maisha yalizidi kuwa magumu zaidi ikiwamo kulala njaa baada ya aliyempachika mimba kukimbia.

“Baada ya kupata ujauzito na kufukuzwa shule, niliwaeleza wazazi wangu wakasema basi tena inabidi nikae tu nyumbani kwani hakuna cha kufanya tena.

“Nilimwendea mhusika kumweleza kuwa nimefukuzwa shule sababu ya ujauzito wako, aliniambia nirudi nyumbani ili aangalie cha kufanya, lakini kesho yake alikimbia kabisa. Hiyo ilikuwa ni baada ya kutishiwa na watu kwamba angeweza kutiwa nguvuni na kutupwa jela miaka 30, hivyo akawa hapatikani kabisa.

“Hivyo nilibaki kupambana na wazazi wangu ikiwamo kulala bila kula siku wazazi wangu wanapokuwa hawana fedha ya kumudu chakula,” anasema Zamaradi.

NDOTO YA SHULE

Zamaradi anasema pamoja na kwamba anajutia kilichotokea, lakini bado haijawa mwisho wa ndoto zake, kwani anatamani kuona akiendelea na masomo mara baada ya kujifungua.

“Najuta sana kupata huu ujauzito kwani sijui ni kwa namna gani nitaendelea na masomo, lakini iwapo itapatikana fursa nyingine ya kuendelea na shule baada ya kujifungua nipo tayari kufanya hivyo.

“Sihitaji kabisa kusikia jambo la kuolewa, ninachotamani ni kuona ndoto yangu ya kuwa Mwanajeshi ikitimia tu japo sijajua nitaitimizaje, ila nikijifungua nikiambiwa nisome niko tayari kwa sababu nitamuachia baba na mama wamlee mwanangu,” anasema Zamaradi.

MWAMKO WA ELIMU NDANI YA FAMILIA

Zamaradi ambaye anawakilisha jamii kubwa ya wasichana wa Kitanzania wanaokosa elimu kwa sababu ya ujauzito, anasema kuwa kukosa msukumo wa elimu kutoka kwa ndugu zake waliomtangulia ni moja ya sababu iliyomfanya kushawishika kirahisi.

Kati ya ndugu zake wanne aliozaliwa nao ni mmoja tu aliyebahatika kufika ngazi ya chuo kikuu huku wengine wakiishia darasa la saba.

AFISA USTAWI WA JAMII KILOSA

Tumaini Geugeu ni Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro ambaye moja ya jukumu lake ni kusimamia watoto au vijana wa kike na  kiume.

Anasema kwa namna hali ilivyo changamoto zipo kwa pande zote mbili, lakini kwa watoto wa kike zinakuwa zaidi sababu zinaonekana moja kwa moja.

“Mfano kwenye mimba za utotoni au za (ma) shuleni kwa upande wa Kilosa changamoto hiyo ipo kulingana na mila au hali ya kimaisha iliyopo ambayo inaleta mkanganyiko pia kwenye malezi ya watoto wa kike.

“Unakuta familia ina hali duni hivyo uwezekano wa mzazi kumtimizia binti mahitaji yote ya msingi inakuwa changamoto badala yake anamwambia ‘si ukatafute’ sasa ukisema hiyo inakuwa ni chanzo cha mimba.

“Lakini pia kuna masuala ya mila na desturi zilizopo ambapo watoto wanaozeshwa ili wazazi waweze kupata mali na kupunguza mzigo wa malezi kutokana na umaskini. Hivyo inakuwa chanzo cha mimba na kukatisha ndoto za watoto wengi,” anasema Geugeu.

Aidha, anasema kuwa kwa wanafunzi ambao wako shuleni wapo ambao wanapata ujauzito kwa kufanyiwa ukatili wa kingono ambao ni kubakwa.

“Wengi wanabakwa na hawasemi hivyo hata kama ile mimba ingeweza kuzuilika inakuwa ni vigumu tena.

“Lakini kuna ngoma za vigodoro ambazo pia zimekuwa chanzo cha mimba. Ikumbukwe kuwa jamii nyingi ya huku inalelewa na mzazi mmoja au bibi na babu hivyo inakuwa ni ngumu kupata udhibiti.

“Tunachofanya ni kutembelea shule mbalimbali kwa kushirikiana na wadau kwa ajili ya kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana na masuala ya ukatili wa kijinsia.

“Sasa wanafunzi ukiwaeleza ukifika kwenye eneo la ukatili wa kingono na ubakaji wanafunzi wanakuuliza…Madame kwa mfano sasa ndio umebakwa umepata ujauzito, naweza nikarudi shule kusoma? Hili ni swali fulani linaloumiza sana ambalo tumekuwa tukikutana nalotunapokuwa tunatoa elimu kwa wasichana walioko shule. Sisi tunaawambia kuwa wanapopatwa na changamoto hiyo wawe wawazi ili kupata msaada.

Geugeu anasema kuwa watoto wengi kulelewa na mzazi mmoja au na wazee ni changamoto. Inafika wakati mama anamkataa mtoto wake aliyeingiliwa na baba wa kufikia ili kulinda ndoa au boma.

“Mama anakwambia nalinda boma afisa ustawi nafanyaje, na hiyo unakuta mtoto wake anaingiliwa na baba wa kufikia. Akimwambia atafukuzwa kwa hiyo anavumilia tu kwa sababu ya ndoa jambo ambalo linasababisha changamoto kubwa.

“Kuna kesi nyingi ambazo zinafika hata sita za mzazi kumshuhudia binti yake aikiingiliwa na baba wa kufikia, lakini hawezi kusema sababu ya kulinda ndoa hivyo wanawakana watoto.

“Lakini ukweli ni kwamba ukatili mwingi kwa mabinti unafanywa na watu wa karibu, kwa hiyo kesi hizo zinaishia kifamilia, na mkwamo mkubwa unaotukwamisha kuzuia hizi kesi ni hizi, kwani wengi wanalinda sifa ya familia ilihali binti ndoto zimepotea.

“Akienda hospitali binti ataeleza aliyempatia ujauzito, lakini ikifika mahakamani au polisi binti anakana kutoa ushahidi na baada ya muda binti anatoweka kwa maana anafichwa… na familia inasema wamekubaliana atamuoa,” anasema Geugeu.

HALI NI MBAYA SEKONDARI

Geugeu anakiri kuwa hali ya ujauzito kwa wanafunzi ni mbaya zaidi kwa shule za sekondari, huku vitendo vya ukatili vikifanyika zaidi kwa wanafunzi wa elimu ya msingi.

“Ripoti ya ujauzito inaonyesha sekondari ndiko kwenye changamoto, lakini kwenye eneo la ukatili wa kingono msingi nako kuna changamoto ile ile,” anasema Geugeu.

Hakuna shaka kwamba hali duni ya uchumi wa familia, Ufukara na hali ngumu ya kiuchumi ya familia ni kisababishi kikubwa cha wasichana kukatisha masomo.

SERIKALI YALETA NEEMA

Mei 11, mwaka huu, Selikali kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, akiwa katika shule ya Sekondari ya Kibasila jijini Dar es Salaam alisema serikali imekuja na utaratibu maalumu wa kusaidia wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni.

Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako mfumo huo wa elimu mbadala unafadhiliwa na serikali ya Uingereza.

“Tumeweka utaratibu kwa watoto ambao wanapata ujauzito kuendelea na masomo yao kupitia njia ya elimu mbadala.

“Katika mfumo huo itategemea mwanafunzi ameacha shule akiwa kiwango gani, lakini kama ameacha kwa mfano akiwa kidato cha kwanza anaweza akasoma kupitia mfumo wa elimu mbadala na akifanya mtihani wake wa kidato cha pili akafaulu basi kidato cha tatu ataendelea katika mfumo wa kawaida (rasmi).

“Vilevile kwa kidato cha tatu akifanya mtihani wa kidato cha nne katika mfumo usio rasmi na akafaulu basi atapangiwa shule yoyote kwenye utaratibu rasmi.

“Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kuwa tunasimamia elimu kwa watoto wa kike na kuondoa vikwazo ambavyo vinasababisha watoto wa kike wasifanye vizuri katika masomo yao sambamba na kuboresha elimu kwa ujumla ili watoto wa kike na wakiume wapate elimu iliyobora,” alisema Prof. Ndalichako.

Kauli hiyo ya serikali ni kielelezo kuwa sasa kuna mwanya mwingine wa kutimiza ndoto kwa watoto wa kike wa Tanzania ambao wamekuwa wakikosa haki yao ya msingi ambayo ni elimu kutokana tu na kupata ujauzito wakiwa shule.

Hali ngumu ya kiuchumi katika familia inasababisha wazazi kushindwa kuwatimizia watoto wa kike mahitaji yao ya msingi ya kimasomo kama ilivyo kwa Zamaradi hapo juu.

Watoto wa kike wanakuwa na mahitaji maalumu ya kijinsia wakati wote, pale mahitaji hayo yanapokosekana huathirika kisaikolojia. Aidha, baadhi huamua kuacha shule na kubaki nyumbani ama kuolewa ili angalau wapambane na maisha wakiwa nje ya mfumo wa shule.

Wazazi nao wamekuwa wakitumia watoto wa kike kama vitega uchumi, baadhi ya kaya masikini zimekuwa na tabia ya kuwatumia watoto wa kike kama chanzo cha mapato kama vile kuwaozesha ili kupata mahari kwa kulipwa ng’ombe na fedha.

Elimu ni haki muhimu kwa binadamu yeyote, kwani ndiyo humsaidia kuyakabili mazingira yake. Ni kwa maana hiyo kila mtoto iwe ni msichana au mvulana ana haki ya kupata elimu ili imnufaishe. Ni kupitia elimu watoto hufikia matarajio na malengo ya maisha yake.

Elimu inafungua fursa za ajira za kujiajiri na kuajiriwa, ubunifu na fikra za kuthamini na kufanya kazi kwa manufaa ili kuzalisha kipato cha mtu mmoja mmoja, familia na taifa.

Kadhalika elimu humwezesha mtu kupanga maisha ya familia anayoitaka yenye afya na ustawi, humwezesha mtu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamiii, kuinua uchumi wake na kushiriki kikamilifu kwenye amali za taifa na masuala ya utamaduni.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img