Tanzania ilisaini na kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu ambao pamoja na mambo mengine unazitaka nchi wanachama kuchukua hatua katika kutimiza wajibu wake kwa kuondoa ubaguzi kwa misingi ya ulemavu katika maeneo yote ya ajira kwani watu wenye ulemavu wana haki ya kufanya kazi sawa na watu wengine.
Kulingana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2012, watu wenye ulemavu nchini ni asilimia 5.9, aidha tafiti za 2008 (Disability Survey) zinaonyesha watu wenye ulemavu ni asilimia 7.8.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kwamba asilimia 10 ya watu katika kundi lolote la jumuiya wana ulemavu wa aina fulani.
Licha ya Tanzania kuchukua hatua mbalimbali kama kutunga Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, kuwawezesha watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mikopo inayotolewa na halmashauri kupitia katika mapato yake ya ndani na nyingine bado watu wenye ulemavu wanaendelea kukabiliwa na vikwazo.
Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya Mwaka 2010 inaelekeza kila taasisi yaani za umma na binafsi iajiri asilimia tatu ya watu wenye ulemavu lakini kumekuwa na changamoto za kutotimizwa kwa takwa hilo la kisheria.
Baadhi ya watu wenye ulemavu wanasema takwa hilo la kisheria kwa kiasi kikubwa linatekelezwa serikalini lakini katika sekta binafsi bado hali hairidhishi.
Msafiri Mhando ni Ofisa Uhusiano wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), anasema yeye hajawahi kuomba ajira serikalini lakini ameshiriki kuwasaidia baadhi ya watu wenye ulemavu na wengine wakaajiriwa katika kada ya ualimu.
“Serikalini kwa namna fulani wanatekeleza hii sheria ila sekta binafsi haitekelezwi ipasavyo, maono ya awamu za marais pia yanachangia kuwapo kwa changamoto za utekelezaji wa sheria,” anasema Mhando.
Mhando anashauri Serikali kupitia idara ya kazi isimamie sheri hiyo kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha utekelezaji wake huku akiishauri pia Wizara ya Uwekezaji kuhakikisha wawekezaji nao wanazingatia sheria hiyo.
Naye Mwanasheria kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Novath Rukwago, anasema kutungwa kwa sheria hiyo lilikuwa mojawapo ya sharti lililobainishwa katika mkataba ambao ulisainiwa Mei 20, 2010.
“Sheria imeeleza haki na wajibu kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu, inagusia kuzuia kuongezeka kwa ulemavu, kuzuia athari kubwa, tutambue aina ya ulemavu na kuona jinsi gani tunaweza tukawasiliana nao na kusimamia yale yote ambayo tumekubaliana,” anasema Rukwago.
Hata hivyo anasema kuna changamoto kwani si watu wote wana uelewa wa masuala ya haki za watu wenye ulemavu.
Anasema haki ya ajira imefafanuliwa katika kifungu cha 31 hadi 34 cha sheria hiyo ambacho kinaeleza kila taasisi yenye waajiriwa kuanzia 20 asilimia tatu wanapaswa kuwa watu wenye ulemavu.
Kifungu cha 33 (3) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 kinatamka kuwa mwajiri yeyote anayembagua mtu yeyote aliye na ulemavu kuhusiana na ajira anafanya hatia.
Aidha kulingana na vifungu hivyo mwajiri anapaswa kuweka mazingira rafiki kwa mtu mwenye ulemavu, ajira zao zilindwe na waajiri wote wanapaswa kila mwaka kuwasilisha taarifa kwa kamishna wa kazi juu ya ajira za watu wenye ulemavu katika taasisi zao.
Mwanasheria huyo anasema anayekiuka sharti lolote la sheria hiyo anatenda kosa na kwamba ikiwa ni shirika au taasisi itaadhibiwa kulipa faini isiyopungua Sh milioni 2 au kifungo cha miaka miwili au adhabu zote kwa pamoja.
ULEMAVU SI KUTOJIWEZA
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Josephine Lyengi, anasema kipo kitengo maalumu cha kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu chini ya ofisi hiyo na kuna waratibu wa madawati kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu yanapewa kipaumbele katika kila wizara.
Anasema mwaka 2006 Tanzania ilisaini Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu, mwaka 2009 iliridhia mkataba huo na ule wa nyongeza (option Protocol), mwaka 2004 ilitengenezwa Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu na mwaka 2010 ilitungwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu.
Lyengi anasema yapo mafanikio ambayo yanaondoa dhana iliyokuwa imejengeka kwamba kuwa na ulemavu si kutojiweza kama vile kuongezeka kwa watu wenye ulemavu wasomi,viongozi na wafanyabiashara.
“Ipo mifano kadhaa ya naibu mawaziri, naibu makatibu wakuu, mabalozi, madaktari wa falsafa, wakurugenzi, majaji na mawakili, wabunge na wengine wengi.
“Mafanikio mengine ni kuwepo kwa shule jumuishi na kupungua kwa shule maalumu, kuongezeka kwa watu wenye ulemavu katika ushiriki na ushirikishwaji wa masuala yanayowahusu katika njanja mbalimbali za maamuzi, kuongezeka kwa majengo fikivu, kutambuliwa kwa lugha ya alama kama lugha ya mawasiliano na kadhalika,” anasema Lyengi.
Hata hivyo pamoja na mafanikio hayo anazitaja baadhi ya changamoto kuwa ni unyanyapaa kwa jamii, mila na desturi, kutojiamini, elimu duni, ajira, umaskini, miundombinu, kutoeleweka kwa sababu za ulemavu, vifaa vya kujimudu, afya na mafunzo ya ufundi.
Katika bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni Waziri mwenye dhamana, Mohamed Mchengerwa, alisema wanatarajia kuajiri watumishi 44,096.
Kulingana na waziri huyo kada ya elimu itaajiri watumishi wapya 10,297, afya 11,215, kilimo 1,383, mifugo 1,250, uvuvi 733, Jeshi la Polisi 1,782, Magereza 843, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji 512 na watumishi wapya hospitali za mashirika ya kidini na hiari 1,240.