1.6 C
New York

Makala: Utoro waondoa wanafunzi 90,607 shuleni

Published:

NA FARAJA MASINDE, DAR ES SALAAM

WAKATI Serikali ikielekeza nguvu nyingi zaidi ili kila motot wa Kitanzania apate elimu bure walau kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.

Idadi ya wanafunzi waoacha shule kwa sababu mbalimbali inatajwa kuwa moja ya vikwazo vya kufanikisha lengo la elimu bure nchini.

Kwa mujibu wa Takwimu za Msingi za Elimu zinazotolewa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI- (BEST) za mwaka 2020 inayochamba mahudhurio shuleni mwaka 2019.

Wanafunzi 98,949kutoka Sekondari za s na binafsi waliacha shyle kwa sababu mbalimbali.

Aidha, kati ya hao, wanafunzi 90,607 wameacha shule kutokana na utoro sawa na asilimia 92 ya wote walioacha shule.

Utoro umetajwa kama sababu namba moja kwa wanafunzi kuacha shule nchini ikifuatiwa na ile ya mimba ambayo ni asilimia 5.5 na vifo asilimia 0.6.

Kiwango hicho ni asilimia 4.2 ya wanafunzi walioandikishwa sekondari. Kwa lugha nyingine ni sawa na kusema kwamba katika kila wanafunzi 24 wa sekondari mmoja aliacha shule mwaka 2019.

Mgawanyo wa kijinsia unaonyesha kuwa katika idadi hiyo ya wanafunzi walioacha shule kwa utoro wasichana ni 42,061 huku wavulana wakiwa ni 48,546.

Hata hivyo, pamoja na idadi ya wavulana kuwa kubwa, lakini ukweli ni kwamba wasichana ndio wamekuwa kwenye changamoto kubwa zaidi, kwani wengi wao wameshindwa kabisa kurejea shule badala yake wamekuwa wakitumbukia kwenye mimba na ndoa katika umri mdogo.

Utafiti unaonyesha kuwa pamoja na wavulana kuongoza kwa utoro, lakini wamekuwa wakijiendeleza kwenye ujuzi mbalimbali ikiwamo veta na taaluma mbalimbali.

Hata hivyo katika takwimu hizo, changamoto imekuwa kubwa zaidi kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili.

Kwani kwa mwaka 2019 wanafunzi 31,486 wa kidato cha kwanza waliacha shule kwa utoro.

Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kidato cha pili kwani  wanafunzi 36,894 waliacha shule kwa utoro. Kwa upande wa kidato cha tatu wanafunzi 16,135 ndio walioripotiwa kuacha shule kwa utoro na kidato cha nne wanafunzi 5,778.

Kidato cha tano ilikuwa ni wanafunzi 179 na kidato cha sita wanafuzi 135. Hii ina maana kwamba changamoto kubwa imekuwa ni kwa kidato cha kwanza hadi cha nne.

Hali inaonekana kuwa mbaya zaidi kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo inawanafunzi zaidi ya 3,000 kwenye takwimu hizo walioacha shule kutokana na utoro.

Pia kuna mikoa yenye wanafunzi 2,000 hadi 3,000, huku mikoa yenye unafuu ikiwa ni Arusha, Pwani na Katavi ambayo ina wanafunzi chini ya 2,000 walioacha shule sababu ya utoro.

Kulingana na takwimu serikali inapaswa kujitafakari ili kujua kama sera ya elimu bure kwa kika mtoto wa Kitanzania itakuwa na manufaa chanya au la, hivyo kubuni mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa kundi hili ambalo linatazamwa kama taifa la kesho linarejea shule na kupata maarifa.

Miongoni mwa mipango inayotarajiwa kutatua tatizo hili ni mpango mbadala ulioahidiwa na serikali kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako kwa kushirikiana na serikali ya Uingereza.

Mpango huo utanza kutekelezwa ili kuhakikisha mabinti wanaoacha masomo, ama kwa mimba au sababu nyigine wanapatiwa fursa nyingine ya elimu.

Tayari serikali kupitia Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dk. Leonard Akwilapo imesema kufikia mwaka 2022 mpango wa wasichana waliokatisha masomo kwa ujauzito kwa ujauzito kurejeshwa shuleni utakuwa umeanza kutekelezwa.

Mkakati mwingine wa kurejesha wanafunzi shuleni ni ule uliosisitizwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Juni 9, mwaka huu, kwa kuwataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanafufua madarasa kwa ajili ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA) ili kusaidia kupunguza ongezeko la watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.

Majaliwa alitoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la kuadhimisha miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania.

“Naagiza madarasa ya MEMKWA yahuishwe. Wakuu wa Mikoa na Wilaya suala la elimu ya watu wazima liwe sehemu ya ajenda zenu mnapofanya ziara. Fuatilieni kuiona elimu ya watu wazima inahuishwa ili kupunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa tatizo la kutokujua kusoma na kuandika,” alielekeza Majaliwa.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Ndalichako amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kutoa mafunzo ya elimu kwa watu wazima wanaohitaji kujiendeleza kitaaluma na kitaalam.

Pia alitoa tamko la wasichana waliopata ujauzito kuanza kujengewa mazingira ya kurejea masomoni.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img