4.2 C
New York

Mvua yaua watu 50, nyumba 1,000 zabomolewa

Published:

Na Nora Damian, Gazetini

Zaidi ya watu 50 wamefariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini.

Vifo 28 zimeripotiwa kutokea katika halmashauri nane za Mkoa wa Morogoro, vifo 19 vimeripotiwa na jeshi la polisi katika Mikoa ya Lindi, Njombe, Tanga, Pwani, Morogoro, Manyara, Geita na Rukwa na vitano vimetokea katika Wilaya za Kibiti, Rufiji na Kisarawe mkoani Pwani.

Takwimu hizo zimetolewa leo Aprili 12,2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.

“Mafuriko yalitabiriwa na kutangazwa na athari zake haziepukiki, bado tunaendelea kukusanya taarifa katika maeneo mbalimbali ya nchi yaliyokumbwa na mafuriko.

“Si kweli kwamba Bwawa la Nyerere limesababisha mafuriko bali limepunguza kwa kiasi kikubwa. Wingi wa maji haufikii maji yaliyokuwa yanapita mwaka 1974…kama kusingekuwa na bwawa mafuriko yangeanza kusumbua tangu Oktoba mwaka jana,” amesema Matinyi.

Amesema katika Mkoa wa Pwani mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa mazao mengi ya chakula, makazi na miundombinu ya barabara ambapo kata 12 zimeathiriwa na watu 1,014 wameokolewa.

Kwa mujibu wa Matinyi, katika Mkoa wa Morogoro nyumba 1,035 zimebomolewa, nyumba 6,874 zimezingirwa na maji, ekari 34,970 zimeharibiwa na mifugo 1,644 imeathiriwa.

Msemaji huyo amesema hatua ya kufungulia maji katika Bwawa la Nyerere ilichukuliwa kwa kuangalia vipimo vya kitaalam na kwamba halijasababisha mafuriko.

Kuhusu mradi wa Bonde la Msimbazi amesema utaanza kutekelezwa Aprili 15,2024 na utasimamiwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA).

Amesema tayari Serikali imelipa fidia Sh bilioni 52.61 kwa wananchi 2,155 na sasa wanakamilisha malipo kwa wananchi 446 ambao walikuwa bado hawajafanyiwa tathmini.

Amesema mradi huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano unagharimu Sh bilioni 675 pia utahusisha ujenzi wa miundombinu ya kukabiliana na mafuriko, daraja la jangwani na karakana ya mabasi yaendayo haraka.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img