21 C
New York

Balozi Njenga: Kila mmoja anadeni la kutunza mazingira

Published:

*Asisitiza upandaji miti kwa ajili ya heshima ya Wangari

Na Faraja Masinde, Gazetini

“Katika mambo ambayo Wangari alihimiza na kuzingatia ni kwamba sisi tuna wajibu kama kizazi kilichopo sasa kupanda mti ili kukisaidia ama kutunza mazingira na hali ya maisha ya vizazi vijavyo”

Balozi wa Kenya nchini Tanzania,Balozi Isaac Njenga.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Balozi Isaac Njenga amesema kila mmoja analo deni na jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba anatunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Balozi Isaac Njenga akizungumza katika zoezi la upandaji miti 300 kwa heshima ya Mazingira ya Afrika na Siku ya Wangari Maathai katika Hifadhi ya Mazingira ya Pugu Kazimzumbwi mkoani Pwani leo Machi 16, 2024.

Amesema mazingira ambayo tunajivunia hivi sasa ni sababu ya kuwapo kwa watangulizi ambao walijitoa kwa kupanda miti na kuitunza na leo inasaidia kuzalisha chakula, maji na mahitaji mengine.

Balozi Njenga ameyasema hayo leo Jumamosi Machi 16, 2024 wakati wa hafla ya kupanda miti 300 katika Hifadhi ya Mazingira ya Kazimzumbwi iliyoko wilayani Kisarawe mkoani Pwani.

Hafla hiyo ya upandaji Miti kwa heshima ya Mazingira ya Afrika na Siku ya Wangari Maathai ambayo huadhimishwa Machi 3, kila mwaka umeshirikisha Wafanyakazi wa Ubalozi wa Kenya jijini Dar es Salaam, Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Balozi Isaac Njenga akipanda mti katika zoezi la upandaji miti 300 kwa heshima ya Mazingira ya Afrika na Siku ya Wangari Maathai katika Hifadhi ya Mazingira ya Pugu Kazimzumbwi mkoani Pwani leo Machi 16, 2024.

Hata hivyo kwa mwaka huu siku hiyo ilisogezwa mbele baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia Februari 29, 2024.

“Tumeiadhimisha siku ya leo ya Wangari Maathai Day na siku ya Mazingira Afrika badala ya Machi 3, kutokana na msiba wa Mzee wetu, Hayati Ali Hassan Mwinyi, tunashukuru kuona kwamba kumekuwa na watu wengi wakiwamo wahisani wetu Benki ya KCB na hiki ni kielelezo kwamba wanaona umuhimu wa kutunza mazingira.

“Katika mambo ambayo Wangari alihimiza na kuzingatia ni kwamba sisi tuna wajibu kama kizazi kilichopo sasa kupanda mti ili kukisaidia ama kutunza mazingira na hali ya maisha ya vizazi vijavyo.

“Hivyo, kila mmoja wetu ana jukumu na deni la vizazi vijavyo katika utunzi wa mazingira, kwani haya tunayojivunia sasahivi ni sababu kulikuwa na watu waliopanda miti na kuitunza na ndiyo sasahivi tunapata maji, hali ya hewa nzuri na chakula, hiyo ndiyo sababu inayotukutanisha katika siku yake na kuzingatia mambo aliyoyatilia mkazo siyo Kenya peke yake bali Afrika na Duniani kwa ujumla,” amesema Balozi Njenga.

Akimzungumzia zaidi Wangari, Balozi Njenga amemwelezea kama mtu naliyejitioa kwa ajili ya kupigania mazingira kwa zaidi ya miaka 40 huku akisisitiza kuwa watu wanapaswa kuiga mfano huo.

“Wangari maisha yake yote alizingatia utuanzaji wa mazingira hadi kuwa mwanamke wa kwanza kushinda tuzo ya Nobel kutokana na juhudi yake, mwaka 1977 alianzisha vuguvugu la kutetea mazingira (Green Bert Movement) kwa ajili ya kutetea haki za binadamu na kutunza mazingira,” amesema Balozi Njenga.

Awali, akizungumza katika siku hiyo iliyobebwa na kauli mbinu ya Panda mti, Okoa Dunia, Naibu Kamishna wa Uhifadhi TFS, Caroline Malundo, amesema miti iliyopandwa katika hifadhi hiyo ni ile inayostahimili ukame huku akiitaja baadhi yake kuwa ni migunga na mkangazi ambayo huoteshwa kando ya mto.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Sware Semesi akizungumza katika zoezi la upandaji miti 300 kwa heshima ya Mazingira ya Afrika na Siku ya Wangari Maathai katika Hifadhi ya Mazingira ya Pugu Kazimzumbwi mkoani Pwani leo Machi 16, 2024.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Sware Semesi, amesema mti ni mmoja ya kiungo cha dunia kinachoiwezesha kuishi kwani inaleta hewa, mvua, chakula na kulinda ardhi.

“Hivyo, siku ya leo tunaisherehekea hii siku kama Afrika ikiwamo Tanzania kwa mchango mkubwa wa Kenya ambayo inasimamia Jumuiya ya Kimataifa inayoshughulikia mazingira, pia tunamsherehekea Mama Wangari ambaye alikuwa kinara Tanzania kutokea Kenya katika nyanja ya utunzaji wa mazingira na alikuwa kinara katika upandaji miti kwa mtu mmoja mmoja ndani ya Bara letu la Afrika na ni mwanamke wa kwanza kupewa tuzo ya Nobel rekodi ambayo haijawahi kuvunjwa.

“Kama Afrika na familia ya Afrika lazima tuwe kinara kuhakikisha kwamba mazingira yetu yako safi, yako hai na tunashughulikia hali ya mabadiliko ya tabianchi, tunadhibiti hatari yakutokea kwa jangwa, hivyo hali hii ikiendelea hivi ilivyo hivi sasa tutashindwa kuishi sababu mti ni uhai,” amesema Dk. Immaculata.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img